Na Mwandishi Wetu-ZANZIBAR
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi-CCM- Taifa ambaye pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama na viongozi wa CCM katika Mkoa Kaskazini Unguja wadumishe na kuimarisha ushirikiano miongoni mwao.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliyasema hayo juzi Wilaya ya Kaskazini (B) Unguja wakati akizungumza kwenye kikao kilichojumuisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho kwa ajili ya kujadili mipango na mikakati ya kuimarisha chama hicho.
Mjumbe huyo alisisitiza kuwa kama viongozi wa chama hicho watadumisha ushirikiano na kuondoa tofauti zao watakijenga chama na kuongeza idadi kubwa ya wanachama wapya ikilinganishwa na hali ilivyo kwa sasa katika eneo hilo.
“Baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu kazi iliyopo kwa sasa kwa viongozi wa CCM katika ngazi zote ni kuweka mipango na mikakati madhubuti itakayoweza chama hicho kuendelea kushika dola,” alisema Samia.
Makamu huyo wa Rais ambaye pia ni mlezi wa CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, alisema ana imani kubwa kuwa kuanzia sasa viongozi hao watajipanga ili kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa 2020.
Kuhusu uimarishaji wa jumuiya za chama hicho, Samia aliwataka viongozi wa CCM katika Mkoa wa Kaskazini Unguja waimarishe jumuiya hizo ili ziweze kutekeleza majukumu ya kichama katika kila ngazi.