24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 31, 2023

Contact us: [email protected]

Samia awaonya wafanyakazi TRA

Na Upendo Mosha, Moshi

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameonya tabia ya baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wanaojiita kikosi kazi kinachowatisha wafanyabiashara ili walipe kodi.

Pia ameitaka kufanya kazi zake kwa kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kujenga uhusiano bora na wafanyabiashara wa kada zote ili waweze kulipa kodi kwa uhuru na uadilifu bila vitisho.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kumpokea kwa ajili ya kuanza ziara ya siku tano ikiwamo kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alisema vikundi hivyo vya watumishi wa TRA na wafanyabiashara, wanasema wanatekeleza maagizo ya Serikali.

“Wanasema wanatekeleza maelekezo kutoka juu, huo ni uongo na hakuna maelekezo kutoka kwa viongozi wa ngazi za juu walioelekeza kushurutishwa kwa wafanyabiashara kulipa kodi,” alisema na kuongeza: “TRA haina sababu ya kujenga uadui na wafanyabiashara wa kada zote kwa kuwapa vitisho ili kuwashurutisha kulipa kodi, jambo hilo si msimamo wa Serikali.”

Pia alisema Serikali inahitaji kila mfanyabiashara alipe kodi lakini isingependa kutumia vitisho bali kinachohitajika ni elimu kwa wafanyabiashara ili walipe kodi kama wazalendo wa kweli na si vinginevyo.

“Vitisho vitasababisha baadhi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao na jambo hilo litainyima Serikali mapato yake,” alisema.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali ipo katika mchakato wa kufanya maboresho ya Kiwanda cha Mashine Tools na Kituo cha Maendeleo ya Viwanda Mkoa wa Kilimanjaro (KIDT), ili vizalishe vipuri katika viwanda vyote.

Alisema Serikali imeelewa dhamira ya ujenzi wa viwanda hivyo atawasilisha ombi hilo katika ngazi stahili ili kuhakikisha uimarishwaji wa viwanda hivyo unakuwa msaada katika kuleta mapinduzi ya viwanda nchini.

“Tunaweza kukiwezesha Kiwanda cha Machine Tools na KIDT ili viendeleze kusudio lake la maendeleo ya viwanda hapa nchini kwa sababu vina uwezo wa kuzalisha vipuri kwa ajili ya viwanda vingine vya hapa nchini,” alisema.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alisema kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 walikusudia kukusanya Sh bilioni 188.6 na makusanyo halisi kwa kipindi hicho ni Sh bilioni 173.1 sawa na asilimia 92.

“Kwa mwaka 2018/2019 mkoa umelenga kukusanya shilingi bilioni 202.8 kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2018 na hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 31.8 kimekusanywa ambacho ni sawa na asilimia 16 ya makusanyo,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,208FollowersFollow
567,000SubscribersSubscribe

Latest Articles