Samia asisitiza ulipaji ada CCM

0
820

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewataka viongozi wa CCM Mkoa wa Magharibi kuwahimiza wanachama kulipa ada za chama.

Akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi jana, Samia alisema ulipaji wa ada ni hatua muhimu ya kumfanya mwanachama kuwa hai ndani ya CCM, hivyo kila mwanachama anatakiwa kutekeleza wajibu huo.

Samia alitoa wito huo kwenye ukumbi wa Utengamano (Peace Building Center) uliopo Welezo, Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja akiwa katika ziara yake mikoa ya CCM kwa upande wa Unguja.

Aliongeza kuwa katika mkoa huo kiwango cha malipo ya ada ya wanachama yapo chini na kwamba hakiridhishi.

Alisema kuna baadhi ya viongozi na wanachama wamekuwa na tabia ya kulipa ada kila ikikaribia kipindi cha uchaguzi jambo linalohatarisha uhai wa uanachama wao.

Mbali na hilo, Samia alisema kuna tabia ya baadhi ya viongozi wanajitafutia kura zao binafsi na si za chama na kwamba hawafanyi kazi za chama badala yake wanajiandaa kutafuta nafasi za uongozi kuelekea uchaguzi.

Aliwataka viongozi hao kukisemea chama na kukiombea kura na si kujiombea kura binafsi na jambo hilo linaweza kuchangia kuzorotesha ushindi wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

“Viongozi, watendaji na wanachama wote muendelee kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha mnaandaa vyema mazingira rafiki ya chama kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” alisisitiza Samia.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja, Mgeni Mussa Haji alisema uongozi wa mkoa huo umejipanga vizuri kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

Mgeni alisema CCM imejipanga kushinda katika uchaguzi huo kwenye shehia zote za Mkoa wa Magharibi ikiwemo wadi 26 na majimbo 13.

Alisema uongozi wa mkoa huo umejipanga kimkakati katika kuhakikisha majimbo yote yanakwenda CCM katokana na kuwa upo vizuri.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here