Samia aongoza waombolezaji msiba mtoto wa Mkuu wa Majeshi

0
1260

Waandishi wetu-Dar es salaam

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameongoza mamia ya waombolezaji kuuaga mwili wa aliyekuwa rubani wa ndege wa Kampuni ya Auric, Nelson Mabeyo ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo.

 Nelson alifariki dunia Septemba 23, mwaka huu katika ajali ya ndege iliyoanguka uwanja mdogo wa ndege wa Seronela uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Msiba huo ulihudhuriwa na viongozi wa dini, Serikali, wastaafu pamoja na wa vyama vya upinzani.

Viongozi hao ni pamoja na Makamu wa Rais Mstaafu, Dk. Mohamed Gharib Bilal, mke wa Rais Mstaafu, mama Sitti Mwinyi, Spika wa Bunge mstaafu Anne Makinda, Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Dk. Agustino Mahiga na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu (Muungao na Mazingira), George Simbachawene.

Wengine ni Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo.

Misa ya kuuaga mwili huo iliongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa akisaidiwa na Paroko wa Parokia ya Kawe, Padri Peter Shayo.

Akizungumza baada ya misa hiyo, baba wa marehemu,  Jenerali Mabeyo, alisema Nelson alikuwa ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini ameamua kumchukua akiwa na makusudi yake.

Alisema Nelson alikuwa na ndoto zake za kuendesha ndege kubwa na kwamba alichaguliwa kwenda kwenye mafunzo ya kurusha ndege hizo nchini Canada.

“Nilikuwa napata sifa nyingi sana za Nelson, kwamba alikuwa na bidii katika kazi yake na alikwishaomba kazi ATCL (Shirika la Ndege la Tanzania) ili atimize ndoto yake kuendesha ndege kubwa,” alisema Jenerali Mabeyo.

Mwili wa Nelson umesafirishwa jana kwa ndege maalumu kuelekea kijijini kwao Masanza mkoani Mwanza kwa maziko.

Ndege hiyo iliyoanguka Jumatatu wiki hii ilikuwa ikiendeshwa na marubani vijana, Nelson na Nelson Orutu, ambao wote walipoteza maisha katika ajali hiyo.

Kaka wa marehemu Kelvin Orutu, alinukuliwa na gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) akisema mdogo wake alikuwa ahitimu mafunzo ya urubani.

Alisema alikuwa katika likizo ya mafunzo kwa vitendo, alikuwa akifanya safari za kujifunza kuendesha ndege ambapo hadi anapata ajali alikuwa amebakiza saa 30 kutimiza mafunzo yake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here