Samia amwakilisha JPM mkutano Uganda

Na Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameondoka nchini jana kwenda Kampala, Uganda kushiriki mkutano wa mwaka 2019 wa ‘Africa Now Summit’ unaotarajiwa kufanyika leo na kesho.

Samia anamwakilisha Rais Dk. John Joseph Magufuli katika mkutano huo ambao utafunguliwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye ndiye mwenyeji.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Makamu wa Rais jana, ilisema mkutano huo utakuwa na mada mbalimbali, ikiwamo ya uongozi unaohitajika kuchochea mabadiliko ya kijamii na uchumi Afrika ambayo itatolewa na Samia.

Taarifa hiyo ilisema viongozi wengine watakaotoa mada ni Rais wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Abdel Fattah el Sisi, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Naibu Rais wa Kenya, William Ruto na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Ahmed Abiy.

Kwamba  mada zote zitajikita kwenye kuonesha chachu ya  uongozi katika kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.

Mkutano  huo utaanza na hotuba kutoka kwa Rais wa Somalia, Mohamed Abdullahi na baadae kufungwa rasmi na mwenyeji wake, Rais Museveni.

Samia ataambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here