28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Samia aagiza kuundwa Mfuko wa Mazingira

Mwandishi Wetu – Tabora

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza kuundwa kwa Mfuko wa Mazingira mkoani Tabora kusaidia usimamizi wa shughuli za mazingira katika mkoa huo.

Akizungumza wakati akihitimisha kongamano la mazingira la mkoa huo jana, Suluhu alisema kuundwa kwa mfuko huo kutasaidia ushiriki wa wananchi na viongozi wa Serikali katika utunzanji wa mazingira, ili kunusuru mkoa huo kuingia katika jangwa.

Alisema kwa kuanzia Serikali ya mkoa inaweza kuainisha mfumo huo kwa kuwashirikisha wananchi, lakini pia iwapo wataona inafaa, viongozi wanaweza kuamua kuunda mfuko huo katika wilaya ili kurahisisha usimamizi.

“Nikiangalia idadi ya watu wa Tabora ambao ni wafugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku kwa wingi, kila mtu hapa akitoa angalau kuku wawili na thamani yake ikaingizwa katika Mfuko wa Mazingira mnaweza kupata kitu kikubwa. Hata kama haiwezekani kwa kila mtu, angalau kila familia ikisema itoe kuku wawili na thamani yake ikaingizwa katika Mfuko wa Mazingira ni suala linalowezekana,” alisema.

Alisema kuhusu utajiri wa ng’ombe walio nao wakazi wa mkoa huo ni suala jema, lakini kutokana na matokeo hasi kwa mazingira, hasa wanyama hao wanaposababisha uharibifu kwa kuharibu ikolojia ya maeneo hayo, ipo haja ya wafugaji kuthaminisha mifupo yao kwa kuiuza na kubaki na michache kulingana na maeneo yao.

Samia alisema ipo haja ya kuchukua hatua zote muhimu za kulinda mazingira kwa kuwa hatua yoyote inayofanyika katika kuyaharibu inayasababisha yatoe adhabu kali kwa binadamu hadi watakaporudi na kuwa rafiki kwa kuyalinda.

Awali, akifungua kongamano hilo, Suluhu alisema mji huo wa Tabora unapendeza kwa kuangalia nje, hasa unapopita katika barabara kuu, lakini ukiingia ndani ni kuchafu.

Katika kongamano hilo lililokuwa likiongozwa na kaulimbiu ya ‘utunzaji wa mazingira kwa maendeleo ya Tabora’, Suluhu alisema uongozi wa mkoa huo na wananchi wake wamejitahidi kuipendezesha Tabora, hasa kwa kupanda miti kwenye barabara za manispaa hiyo, lakini hali hiyo ni tofauti ukiingia ndani ya mji huo.

“Kupanda miti haitoshi, bali tupendezeshe na maeneo ya ndani. Mimi huwa nina jicho la umbea ambalo wakati mnanipitisha barabarani nilikuwa nikiangalia na kuyaona haya, nje kunapendeza lakini kwa ndani ni kuchafu.

“Mkiona jicho langu limelegea, lakini linaona mbali kwelikweli. Huu usafi usiishie katika barabara tu, bali tuufanye hadi tunakotoka,” alisema.

Alitoa mfano wa hali hiyo na wanawake katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, ambao wamekuwa wakiishi katika maeneo yenye mitaro ya maji machafu yaliyojaa funza, lakini hawajishughulishi kuyasafisa, ila ukikutana nao barabarani kwa jinsi walivyopendeza huwezi kudhani kuwa ndio waliotoka katika maeneo hayo.

“Huwa nawaambia Dar es Salaam kuna maeneo machafu, maji ya mitaro yanatoka hadi funza, lakini utakuta wanawake wameweka vivukio kwenye hiyo mitaro, unakuta mtu amevaa vitu vya thamani ya hadi shilingi laki saba anatoka anavuka tu anakwenda zake,” alisema.

Alisema kwa Tabora, hatua wanazochukua katika upandaji miti barabarani ni jambo la kujivunia na amekuwa akiitumia kama mfano katika hilo kote anakokwenda nchini, lakini wanatakiwa kujirekebisha kwa kuhakikisha wanasimamia usafi katika maeneo ya ndani.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano kwa viongozi kuhakikisha wanafanikisha maendeleo ya mkoa huo kwa kuwa viongozi ni watu wa kupita ila manufaa yake yanabaki kwa wananchi wa maeneo husika.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Muungano na Mazingira, January Makamba, alisema maendeleo ya nchi na mazingira ni mambo yaliyofungamana na hayawezi kutenganishwa, kwa kuwa utajiri wa maliasili zilizopo katika mazingira ndio unaochangia kuinua uchumi wa nchi.

“Uharibifu wa mazingira umekuwa ukichangia kushuka kwa ukuaji wa uchumi hivyo kuna tishio kubwa la utajiri wa nchi iwapo hatutadhibiti mazingira yetu,” alisema.

Alisema kutokana na uharibifu wa mazingira katika baadhi ya maeneo, Tanzania kwa sasa inashuhudia wakimbizi wa ndani ambao wanakimbia maeneo yao ya asili baada ya kuharibu mazingira na kwenda kutafuta hifadhi katika maeneo mengine.

“Kwa sasa hivi tunaona Mkoa wa Tabora kidogo bado uko salama katika mazingira yake, lakini jangwa linazidi kusogea kutoka Simiyu na Shinyanga ambako wameharibu sana mazingira yao. Ni vyema kulinda sifa ya ulinzi wa mazingira katika mkoa huu,” alisema.

Alieleza kuwa kupanda miti ni jambo moja, kuzuia watu kukata miti ni jambo jingine muhimu na kwamba iwapo itabidi kukata miti hatua stahiki zinatakiwa kuchukuliwa kuhakikisha kwamba miti inayokatwa inakuwa tayari ina mbadala wake.

Katika majumuisho, walifikia makubaliano kadhaa ambayo ni Serikali kusimamia upunguzaji wa bei ya gesi ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuimarisha usimamizi wa sheria za mazingira, maeneo ya miradi yarejeshewe uasili wake mara miradi inapomalizika na wananchi waelimishwe kuhusu upandaji miti yenye faida inayoweza kutoa matunda na kutumika kibiashara.

Pia walikubaliana kila halmashauri itenge fedha kununua mitambo ya mkaa mbadala itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana, kutolewa kwa elimu ya sheria ya mazingira kwa wananchi na Serikali kuu iangalie uwezekano wa kuingiza somo la mazingira kwenye mitalaa ya shule za msingi na sekondari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles