33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Samatta aongeza mzuka Stars

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

NAHODHA wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta, ameongeza hamasa katika kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa kuikabili Uganda ‘Cranes’, mchezo wa mwisho wa marudiano wa Kundi L utakaopigwa Jumapili hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mandela, Kampala nchini Uganda, timu hizo zilitoka suluhu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Meneja wa Taifa Stars, Dan Msangi, alisema kikosi cha timu hiyo tayari kimekamilika, baada ya wachezaji wote kuwasili akiwemo nahodha Samatta.


“Kikosi kimekamilika pia ujio wa nahodha wetu Samatta umeleta hamasa kwa wachezaji wengine na leo (jana) tumefanya mazoezi asubuhi Uwanja wa Boko Veteran, lakini na jioni Uwanja wa Taifa,” alisema Msangi.

Alisema wachezaji wote wa kikosi hicho wako timamu kimwili isipokuwa kipa Suleiman Salula ambaye anasumbuliwa na majeraha baada ya kuumia katika mazoezi ya juzi.

Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo huo ili kufufua matumaini ya kufuzu fainali hizo zitakazofanyika nchini Misri, lakini pia ikiombea matokeo mabaya ya Lesotho itakayoumana na Cape Verde, jijini Praia, katika mchezo mwingine wa mwisho wa Kundi L.

Uganda tayari imefuzu fainali hizo, baada ya kufikisha pointi 13 na kuongoza kundi, wakati Lesotho inakamata nafasi ya pili ikiwa na pointi tano sawa na Tanzania iliyoko nafasi ya tatu,  huku Cape Verde ikiwa na pointi nne.


Timu mbili zinatakiwa kufuzu kutoka kundi hilo na kama Lesotho itaifunga Cape Verde, hata Taifa Stars itaifunga Uganda haitafuzu kwa kuwa katika mechi mbili kati ya timu hizo, Taifa Stars ililazimishwa suluhu nyumbani na kuchapwa ugenini.

Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaichapa Uganda na kukata tiketi hiyo.

“Tunaendelea vizuri na maanadalizi, wachezaji wote wamefika na kila mmoja yuko kwenye hali nzuri, tunafahamu ugumu wa mchezo wenyewe, lakini hatuna namna zaidi ya kushinda, tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa nguvu ili tushinde na kufuzu Afcon,” alisema kocha huyo raia wa Nigeria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles