NA BADI MCHOMOLO-DAR ES SALAAM
KWA kipindi cha wiki kadhaa zilizopita habari kubwa iliyotikisa vichwa vya habari za michezo mitandaoni na katika vyombo vikuu vya habari hapa nchini ni ile ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye anakipiga katika klabu ya K.R.C Genk kule nchini Ubelgiji.
Ukubwa wa habari zake ulianza mara baada ya kufanya vizuri nchini humo na kufanikiwa kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora mwenye asili ya Afrika kwa wale wanaocheza soka la kulipwa nchini humo, tuzo hiyo inajulikana kwa jina la Ebony Shoe Award.
Kwa klabu ya Genk, Samatta ni mchezaji wa tatu kutwaa tuzo hiyo, awali iliwahi kuchukuliwa na Souleymane Oulare raia wa Guinea ambaye alishinda tuzo hiyo mwaka 1999 baada ya kucheza soka kwa kipindi cha miaka mitatu tangu 1996.
Mchezaji mwingine ni Moumouni Dagano raia wa Burkinafaso aliyeshinda tuzo hiyo 2002 baada ya kuitumikia timu hiyo tangu mwaka 2001 hadi 2003 na sasa ni Samatta, lazima habari iwe kubwa hapa Tanzania na katika klabu ya Genk yenyewe kutokana na ushindani kwa wachezaji hao wa kiafrika.
Habari kubwa nyingine ambayo ilitikisa ni kuipa Genk ubingwa wa Ligi Kuu baada ya timu hiyo kusubiri tangu mwaka 2011, lakini jambo lingine ni mchezaji huyo kumaliza Ligi huku akiwa kinara wa ufungaji mabao wa timu hiyo.
Mungu hakuweza kumpa vyote, Watanzania wengi na hata mashabiki wa Genk waliamini kuwa mchezaji huyo atamaliza nafasi ya kwanza kwa kupachika mabao.
Kutokana na ushindani aliokutana nao akamaliza nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao mawili, Samatta akiwa na mabao 23, huku mpinzani wake Hamdi Harbaoui wa klabu ya Zulte Waregem akiwa na mabao 24.
Hayo ni mafanikio makubwa sana kwa mchezaji huyo kujivunia pamoja na Taifa kwa ujumla kwa kuwa anapeperusha vizuri bendera ya nchi.
Alianza kufanya hivyo baada ya kujiunga na TP Mazembe ya nchini Congo akitokea klabu ya Simba, akiwa TP Mazembe alikuwa mmoja kati ya wachezaji waliotoa mchango wa ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika mwaka 2015, lakini alikwenda mbali zaidi na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa wachezaji wa ndani.
Akiwa katika klabu hiyo ya TP Mazembe jina lake lilikuwa kubwa sana, mashabiki wa soka nchini humo walikuwa wanamfanya mchezaji huyo kama mfalme, hivyo aliifanya bendera ya Tanzania kupepea vizuri nchini humo.
Alichokifanya Congo sasa anakifanya Ulaya, huko nchini Ubelgiji, ameweza kuwafanya mashabiki waimbe jina lake katika michezo mbalimbali kutokana na huduma anayowapa.
Thamani ya Samatta wanaijua vizuri mashabiki wa Genk inawezekana ikawa tofauti na ile ambayo waliijua Simba pamoja na TP Mazembe.
Akiwa Mazembe alikuwa kama mfalme, lakini hakuimbiwa nyimbo kama wanavyofanya Genk, Simba hawakufanya kabisa kwa kuwa hakutumia muda mwingi kuonesha makali yake.
Mashabiki wengi wa klabu ya Genk wamekuwa wakinunua jezi ya Samatta na wengi wanaonekana mitaani wakivaa pamoja na jezi za Tanzania, Taifa Stars, hivyo bendera ya Tanzania inapepea vilivyo huko nchini Ubelgiji.
Hii ni sifa pekee ambayo Samatta ameweza kuileta kwa Taifa la Tanzania na bado ana nafasi ya kuendelea kufanya hivyo kwa misimu mingine.
Tumekuwa tukiona mashabiki wa soka Ulaya wakiwa na mabango kuomba jezi ya staa kama vile Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Neymar, Ronaldinho na wengine, lakini kwa Samatta na yeye ameweza kuwafanya mashabiki wabebe mabango ya aina hiyo.
Moja ya bango ambalo lilikuwa limebebwa na shabiki wa Genk uwanjani katika moja ya mchezo wao, liliandika SAMATTA 77 CAN I HAVE YOUR SHIRT PLEASE??? Akiwa na maana ya kuomba jezi ya mchezaji huyo wa kitanzania.
Shabiki huyo aliguswa na kiwango anachokionesha mchezaji huyo, hivyo ni kitu cha furaha kwake kuvaa jezi yenye jina la Samatta mgongoni.
Mbali na Samatta, wapo wanamichezo wengine ambao wanafanya vizuri na kuitangaza Tanzania katika mataifa mbalimbali kama vile Hasheem Thabeet, ambaye alitikisa nchini Marekani katika mchezo wa kikapu kwenye klabu mbalimbali ikiwemo Memphis Grizzlies, Oklahoma City Thunder na zingine nyingi.
Anachokifanya Samatta ni fundisho kwa wachezaji wengine wenye ndoto za mafanikio kwenye michezo, itakuwa faida kwao pamoja na taifa kwa ujumla.
Huu ni mfano wa kuigwa. Sasa baada ya kumaliza Ligi nchini Ubelgiji tunatarajia kumuona kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, lakini ikiwa huku ni mbali, tunatarajia kumuona akiibeba timu ya taifa, Taifa Stars kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika huko nchini Misri kuanzia mwezi ujao.