29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Samatta ala kiapo Misri

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Samatta, amesema kuwa wamejipanga kufa na Algeria katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon2019).

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumatatu usiku kwenye Uwanja wa 30 June, jijini Cairo, ukiwa ni wa tatu kwa Stars, baada ya kuvaana na wababe wa Afrika, Senegal na Kenya waliotarajiwa kucheza nao jana saa tano usiku.

Katika mchezo wa kwanza, Stars ilifungwa na Senegal mabao 2-0, matokeo yaliyowagawa watanzania, baadhi wakimlaumu kocha wa timu hiyo, Emmanuel Amunike, huku wengine wakikiri timu hiyo ya Tanzania ilistahili kufungwa kwani kikosi cha wapinzani wao hao, wachezaji wake wote wanakipiga klabu kubwa za Ulaya.

Ni kutokana na kufahamu hilo, Samatta anaamini hata kama watakuwa wameaga michuano hiyo, kuna kitu wamejifunza, huku akiahidi wachezaji wa Stars kupambana kadri ya uwezo wao Jumatatu ili kuacha majina yao Misri.

Akizungumza jijini Cairo, jana, Samatta alisema: “Tunafahamu tunakwenda kukutana na timu ngumu yenye wachezaji wakubwa kama Mahrez (Riyad), hilo halitutishi, tutafanya kitu kitakachowashangaza.

“Binafsi, nafahamu hii ni nafasi ya mwisho kudhihirisha ubora wangu, hilo lipo kwa wachezaji wenzangu wote, lazima tufanye kitu, hii ni nafasi ya kipekee kwa kila mmoja wetu kujenga jina lake, hakika tutapambana kwa uwezo wetu wote japo kuna maneno yalitolewa ya kututatisha tamaa,”

Aliwataka Watanzania kuendelee kuwapa sapoti ili wapate nguvu ya kupambana uwanjani na kupata kile ambacho wanakihitaji kwa maslahi yao binafsi na soka la Tanzania kwa ujumla.

Katika michuano hiyo iliyofunguliwa Juni 21, mwaka huu, Taifa Stars ipo Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Kenya ‘Harambee Stars’.

Tanzania inashiriki Afcon kwa mara ya pili katika historia ya nchi hiyo, mara ya kwanza ikiwa ni mwaka 1980, kipute hicho kilipofanyika nchini Nigeria, huku Stars ikipangwa Kundi A pamoja na wenyeji Nigeria, Misri na Ivory Coast na kushika mkia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles