30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Mtaka: Simiyu hatutatumia hoteli kuwahifadhi wagonjwa wa corona

Derick Milton -Busega

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, amesema mkoa huo hautatumia hoteli kuhifadhi watu watakaobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19) badala yake watatumia shule za sekondari za bweni.

Alisema uamuzi huo ni katika kuwapunguzia gharama za kuishi siku zote ambazo watakuwa karantini wagonjwa hao, lakini hautawafunga watu wenye uwezo ambao watapenda kwenda hotelini.

Mtaka alitoa kauli hiyo jana wakati akipokea msaada wa vifaa vya ujenzi wa Shule ya Sekondari Mtaka iliyoko Kijiji cha Lukungu wilayani Busega kutoka kwa viongozi wa umoja wa makanisa 21 ya Kikristo Tanzania (CCT), Kata ya Lamadi.

Alisema kuwa tayari kila wilaya imetenga shule yenye vitanda vya kutosha na mazingira mazuri kwa washukiwa wa ugonjwa huo, huku akiwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari.

“Kama mkoa, tumeamua kuwa hatutatumia hoteli kumhifadhi mtu yeyote ambaye atabainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona.

“Tumeamua kuwa tutatumia shule za sekondari za bweni, labda mtu mwenyewe aamue kupelekwa hotelini na tayari hoteli zenyewe tumezihainisha,” alisema Mtaka.

Alisema kutokana na shule zote kufungwa, waliona sehemu sahihi ni kwenye shule hizo, ambazo hazina wanafunzi wala mwingiliano wa watu wengine ikiwa pamoja na kutohitaji gharama ya kulipia hifadhi.

Katika hatua nyingine, Mtaka amewataka wazazi wa wanafunzi wa madarasa ya mitihani mkoani humo kuhakikisha wanawasimamia kujisomea katika kipindi hiki shule zimefungwa kutokana na ugonjwa huo.

Aliwataka wazazi kutotumia nafasi ya shule kufungwa na kuwafanyisha kazi za nyumbani muda mrefu wanafunzi na badala yake wawape muda wa kutosha na kuwasimamia kujisomea.

Alisema kuwa ingawa shule zimefungwa, lakini mitihani ya kitaifa itafanyika kwa ratiba ambayo itapangwa na Serikali, hivyo aliwataka wazazi kuhakikisha wanawasisitiza watoto wao kujisomea.

 “Shule zimefungwa, lakini mitihani ipo pale pale labda ratiba inaweza kubadilika, niwatake wazazi wote Mkoa wa Simiyu kuhakikisha wanawasimamia watoto wao wanajisomea, wanaweza kujiunga hata wawili au watatu wakajisomea,” alisema Mtaka.

Mbali na hilo, aliwataka wananchi kutotumia nafasi ya ugonjwa huo kuwaachia watoto wao wajiingizw kwenye mambo ambayo hayana msingi, ikiwemo kupata mimba na badala yake wahakikishe wanawalinda muda wote.

Akiongea kwa niaba ya makanisa hayo, Mchungaji wa Kanisa la TAG Lamadi, Emmanuel Edward, alisema kuwa waliamua kutoa msaada huo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika shughuli za maendeleo.

Alisema kuwa msaada ambao wametoa ni pamoja na saruji mifuko mitano, pamoja na tripu 10 za mchanga.

Msaada huo wenye thamani ya Sh 600,000 umetolewa kupunguza tatizo la ukosefu wa madarasa ya kutosha katika shule hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,396FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles