Samatta afurahia sare na Napoli

0
725

GENK, UBELGIJI

NAHODHA wa timu ya K.R.C Genk, Mbwana Samatta, amewapongeza wachezaji wenzake na kufurahia sare ya bila kufungana dhidi ya timu ya Napoli kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, uliopigwa juzi nchini Ubelgiji.

Mchezo huo ulikuwa wa pili katika hatua ya makundi, ambapo mchezo wa kwanza K.R.C Genk ilikubali kichapo cha mabao 6-2 dhidi ya RB Salzburg wiki mbili zilizopita, huku Napoli wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mabingwa watetezi wa taji hilo Liverpool.

Samatta ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, amekuwa akiaminiwa kwenye kikosi hicho na sasa amepewa jukumu la kuwaongoza wenzake uwanjani, hivyo mchezo huo wa juzi amedai ulikuwa muhimu sana kwao na furaha yao ni kufanikiwa kupata pointi moja.

“Tumecheza na moja kati ya timu bora na timu ngumu nchini Italia, lakini kitu muhimu ni kwamba tumeonesha ushindani wa hali ya juu ikiwa tofauti na mchezo wetu wa kwanza ambao ulikuwa mbaya kwetu.

“Jambo muhimu ni kutoka sare na hatukuweza kuruhusu bao, tulipata nafasi ya kufunga mabao lakini tulishindwa kuzitumia, hata hivyo tulikuwa na bahati kwa kuwa na wao walitengeneza nafasi nyingi ila tuliweza kuokoa mipira ya hatari,” alisema Samatta.

Msimu huu mchezaji huyo amefanikiwa kufunga jumla ya mabao sita katika michezo 11 aliyocheza ikiwa pamoja bao moja kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kibarua kingine ambacho K.R.C Genk watakutana nacho ni dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool, mchezo ambao K.R.C Genk wataanza nyumbani Oktoba 23, kabla ya kuwafuata Anfield, Novemba 5, mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here