30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Salma Kikwete: Mchinga msirudie kosa kuchagua wapinzani

Mwandishi Wetu, Lindi
 
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mchinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwalimu Salma Kikwete, amewataka wapiga kura wa jimbo hilo wasirudie makosa walioyafanya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuwachagua wagombea wa upinzani badala yake wanatakiwa kuchagua mafiga matatu kwa kumchagua Mgombea Urais, Dk. John Magufuli, yeye na madiwani wote wa chama hicho ifikapo Oktoba 28, mwaka huu.
 
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya kampeni zake zilizofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na jana katika Kijiji cha Namapwiya kilichopo Kata ya Mipingo, Kijiji cha Makangara kilichopo Kata ya Rutamba, Kijiji cha Milola Magharibi kilichopo Kata ya Milola na vijiji vya Kitohavi na Likwaya vilivyopo Kata ya Matimba.
 
“Waswahili wanasema kufanya kosa sio kosa bali kurudia kosa ndiyo kosa, tumekuja kuwasihi kwamba wana Mchinga msirudie kufanya kosa kama lile la mwaka 2015, ile likizo mliyokaa inatosha, nawasihi, nawaomba tuchague CCM, mkichagua diwani wa CCM atafikisha kero zenu katika vikao vya halmashauri na mbunge atazifikisha bungeni, kero na changamoto zote za Mchinga zitashughulikiwa na madiwani, mimi na Rais Magufuli pindi tutakapochaguliwa Oktoba 28, 2020.
 
“Mkichagua mafiga matatu changamoto zenu zitapungua lakini msipofanya hivyo na kuchagua wagombea mchanganyiko mtapata tabu na kukosa atakayewaunganisha, kwa miaka mitano mliteseka na kukosa maendeleo kwa sababu mlichagua mtu ambaye bajeti za maeneo yenu zikiwa zinajadiliwa yeye alikuwa anatoka nje, huo ndiyo ukweli wenyewe na wala hatupigi propaganda au bla bla,” amesema Mwalimu Salma.
 
Pia amewataka wananchi wa jimbo hilo wasidanganyike na maneno ya propaganda yanayotolewa na wagombea wa upinzani kwamba hakufanya kitu alipokuwa Mke wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.
 
“Msije kudanganywa hapa eti Mwalimu Salma Kikwete alikuwa Mke wa Rais hakufanya kitu, hayo ni maneno ya watu waliofilisika sera, kwani nilipokuwa mke wa Rais mliniona hapa? Hamkuniona kwa sababu haikuwa dhamana yangu bali ile ilikuwa ni dhamana ya Rais wa Awamu ya Nne lakini pale ilipobidi nilifanya tena sio sehemu moja tu bali kwa Mkoa wote wa Lindi.
 
“Nilitoa msaada kwa kuhakikisha huduma za afya Hospitali ya Mkoa wa Lindi ya Sokoine zinaboreshwa kwa kutoa msaada wa vifaa tiba ili kila mtu wa Lindi akienda pale apate huduma nzuri inayostahiki, nikashiriki katika ujenzi wa shule na pia halmashauri ikapatikana,” amesema Mwalimu Salma.
 
Katika hatua nyingine akiwa Kijiji cha Namapwiya, Kata ya Mipingo alitoa ahadi ya kujenga darasa la awali litakaloanza kutumika mwakani baada ya kukutana na mtoto Amina Kamlanje mwenye umri wa miaka 12 akiwa hajaanza shule kwa kuwa kijijini hapo hakuna shule.
 
“Tuchagueni CCM tuanze kazi, lazima watoto waanze darasa la awali, lazima tushirikiane, tufyatue matofali tujenge shule na mwakani ianze, hili nitalisimamia mimi mwenyewe ama nichaguliwe kuwa mbunge au nisichaguliwe lakini darasa lazima lijengwe.
 
“Hii ni ahadi yangu binafsi na kizazi changu, darasa la awali lazima lianze hapa Namapwiya, nisipojenga mimi nina wanangu watajenga, wasipoweza wanangu nina Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) nawakabidhi hii kazi ya ujenzi wa darasa na watajenga, mimi mwenyewe nitasimamia ujenzi wake ili huyu mtoto Amina Kamlanje na wenzake wasome ifikapo mwakani,” amesema Mwalimu Salma.
 
Akiwa katika vijiji vya Kitohavi na Likwaya, Kata ya Matimba, amesema akichaguliwa kuwa mbunge ifikapo Oktoba 28, 2020 ana dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo ya jimbo hilo kwa kuhakikisha huduma za fya zinaboreshwa katika zahanati na vituo vya afya, elimu nayo inaboreshwa, atashughulikia miundombinu ya barabara, atasimamia shughuli za kilimo, uvuvi na ufugaji na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi katika maeneo yanayokosa.
 
Pia amesema vipaumbele vyake vinakusudia kugusa maisha ya kila siku ya wananchi wa jimbo hilo ili kupatikane mabadiliko katika maendeleo yanayokuja kwa kuwa ana mipango na mikakati thabiti ya kuitekeleza.
 
Amesema kero na changamoto za jimbo hilo zitapungua kwa kupatiwa ufumbuzi kwa kuwa ana uwezo wa kuwafikia wakubwa wote serikalini kwa kuanzia kwa Rais Dk. Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wote wenye dhamana na kuwaeleza jambo lolote la maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles