23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Sallehe Ngwasa: Nimechangia damu kwa miaka 21

Na  AVELINE  KITOMARY 

NI dhahiri kuwa wakati wa kupigani uhai wa mtu wako wa karibu utaweza kujitoa kwa kadiri ya uwezo wako bila kujali matokeo  ya baadae.

Hii imeonekana kwa kijana ambaye alianza kuchangia damu akiwa na umri wa miaka 16 ili kuokoa maisha ya mtu muhimu kwake. 

Umri huo hauendani kabisa na viwango vilivyowekwa na mpango wa damu salama lakini kutokana na uhitaji wa damu ilimlazimu kufanya hivyo.

Sallehe Ngwasa ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 37 ni mzaliwa wa  Mkoa wa Pwani,Wilaya ya Bagamoyo  anasimulia ni jinsi alivyojitoa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mama yake mzazi  ambaye alikuwa mahututi na kuhitaji kuongezewa damu.

Sallehe Anasema kwake jambo hilo halikuwa rahisi   kutokana na wasiwasi na  uwoga ambao alikuwa nao  lakini alifanikiwa kufanya  hivyo ili kuokoa maisha ya mama yake.

“Kwa wakati huo nilikuwa ndio kwanza nimemaliza darasa la saba huko Butete Rufiji,mama yangu anasumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya meno hivyo amekuwa akipata tatizo la kuishiwa na damu mara kwa mara.

“Nakumbuka siku niliyofika hospitali nikaambiwa kuwa mama yuko mahututi na akiendelea kukaa bila kuongezwa damu anaweza kupoteza maisha ,hospitali aliyolazwa ilikuwa haina damu kwa wakati huo kulikuwa hakuna ndugu yangu mwingine.

“Japo kwa wakati huo uelewa wangu ulikuwa mdogo Daktari akanitia moyo kuwa naweza kuchangia damu bila kupata madhara, basi kwa jinsi nilivyomwona mama ana hali mbaya nikaamua kutoa damu na wakati huo ndio nilijiunga na chama cha wachangia damu Rufiji,”anasimulia Salleh.

Anasema  tangu kipindi hicho alipotoa damu hakuishia hapo  hadi sasa imekuwa desturi yake kutoa damu kila mwaka.

“Baada ya mama kuongezewa damu afya yake iliimarika hadi leo ni mzima ukizingatia anaugua ugonjwa wa saratani .

“Tangu mara ya kwanza nilipotoa damu nimeendelea na zoezi hilo na sasa ni miaka 21, kwa mwaka naweza kutoa damu mara moja hadi mbili nafanya hivyo ili kuokoa maisha ya watu wanaohitaji kuongezewa damu,”anabainisha.

DAMU YAKE ILIVYOLETA MSAADA

“Uchangiaji  damu ni tendo la upendo”; anasema Sallehe hicho ndicho kinachomvutia zaidi kufanya hivyo.

Anasema damu yake anayoichangia haijaishia tu kumsaidi mama yake mzazi bali na ndugu zake ambao wamekumbwa na matatizo mbalimbali hivyo kuhitaji kuongezewa damu. 

“Unajua sisi binadamu tuna leo na kesho ,mimi nina familia ya watoto watano na wake wawili ,mtoto wangu akiumwa na kuhitaji kuongezewa damu hatutaanza tena kuhangaika kutafuta damu kwasababu huwa nachangia hiyo itamsaidia.

“Kwa kadri nilivyoendelea kutoa damu  ndugu zangu wengine walianza kunufaika kama mama yangu mkubwa kuna kipindi aliugua akahitaji kuongezewa damu  nikaatumia kadi yangu,mjomba pia aliongezewa damu lakini pia mdogo wangu alipata ajali akatumia damu yangu lakini kwa bahati mbaya alifariki lakini kwa wote damu yangu ndio iliyotumika,”anaeleza Sallehe.

MITAZAMO HASI HUKWAMISHA UCHANGIAJI

Sallehe anasema jamii yake imekuwa na mitazamo tofautitofauti  kuhusu zoezi analofanya la kuchangia damu mara kwa mara.

Anasema mitazamo hasi imekuwa changamoto kwake  huku akisisitiza  elimu ya damu salama kutiliwa mkazo hasa katika maeneo ya vijijini. 

“Kwa jamii yangu kila mtu anamitazamo yake, kuna wengine wananibeza na wengine wananisifia kwa wasio na uelewa  wengine wanaamini kuwa ile sindano unayotobolewa kutoa damu wanatumia watu wengi hivyo wanahofu ya kuambukizwa  ugonjwa .

“Wapo wanaohofia kuwa wakitaka kwenda kutoa damu watapimwa na HIV hii inawafanya watu wengine kutotaka kuchangia damu dhana ambayo sio kweli,”anasema. 

Anasema kuwa pia wapo wanaoaamini kuwa hata leo akichangia damu siku akienda hospitali ataambiwa alipie damu aliyoitumia kitu ambacho pia sio kweli.

“Kila mchangia damu anakadi maalum mbayo anapewa na kadi hii kazi yake ni kuonesha kwa hospitali yoyote anayokwenda, hii itamsaidia kupata damu bila kuchangia tena kwahiyo jamii wabadilishe mitazamo yao wachangie damu,”anasisitiza.

ASHAURI HAYA

Sallehe anasema uchangiaji damu kwa maeneo ya vijijini ni hafifu kutokana na elimu na mwamko mdogo wa jamii.

Anashauri uwepo wa kampeni za elimu na uchangiaji wa damu kwani hiyo itaweza kusaidia kuongeza kiwango cha ukusanyaji damu.

“Kiwango cha elimu hasa vijijini  kwa maeneo ninayokaa bado ni kidogo  ni kwasababu hakuna kampeni ,mtu anaenda kuchangia damu hospitali wakati ndugu yake akiwa mgonjwa kama huna mgonjwa huwezi kusikia kama kuna huduma hii lakini huku mjini afadhali kidogo hivyo nashauri nguvu kubwa iwekwe vijijini. 

“Kwa watu ambao hawana mwamko wa kuchangia damu labda niwashauri tu kwamba zoezi la uchangiaji damu ni muhimu kwani unaishi na damu mwilini lakini huwezi kujua unaweza kupata tatizo hiyo damu ikakusaidia au ndugu yako akipata inaweza kumsaidia,”anaeleza . 

SIKU YA  WATOA DAMU

Katika siku ya maadhimsho ya watoa  damu duniani Juni 14, Sallehe anasema anaungana na wachangia damu kote duniani huku akiahidi kuendelea kutoa damu siku zote za maisha yake.

Maadhimisho ya siku hii yanayoadhimishwa leo hulenga  kuwashukuru watoaji damu  kwa hiari  katika kusaidia maisha ya wahitaji.

Tukio hilo pia  linalenga  kuhamasisha  na kuhakikisha  ubora,usalama  na uwezekano wa damu kupatikana kuwa  mkubwa ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji kwa haraka zaidi.

Licha ya malengo hayo, Juni 14 pia ni siku aliyozaliwa  mvumbuzi wa makundi  ya damu ABO,raia wa Australia Dk. Karl Landsteiner ambaye alizaliwa  mwaka 1868.

Uvumbuzi aliofanya hadi sasa umesaidia damu kuweza kutumika katika makundi na kuepusha hatari ambayo ilikuwepo mwanzo ya mtu kuongezewa damu na kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) watu milioni 92   wanatoa damu kwa hiari kila mwaka huku karibu  asilimia 50  ya watu wanaochangia damu wanatoka katika nchi zilizoendelea.

Kila mtu mmoja anayechangia damu anaweza kuokoa maisha ya watu watatu huku uhifadhi wa mazao ya damu ukiwasaidia wagonjwa wengine kama wa saratani ya damu, moyo,figo na wengine.

Hapa nchini , Mpango wa Taifa wa Damu Salama umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha damu inapatikana kwenye hospitali zote ili wagonjwa wa dharura na wale wasio wadharura waweze kupata  kwa haraka.

Hatua hii imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya wagonjwa hasa wale dharura.

Ukusanyaji wa damu umekuwa ukizingatia  mambo kadhaa kama usalama katika upatikanaji,uhifadhi,usambazaji   na ubora unaofaa kwaajili ya matumizi ya binadamu ukizingatia makundi. 

Kwa mwaka huu  2020,Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsi,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu atakuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo huku kauli mbiu ikiwa ni “Damu Salama Inaokoa Maisha”(Safe Blood Saves Lives).

Kauli mbiu hiyo inaonesha mshikamano katika uchangiaji damu  pia inalenga mambo muhimu ambayo yanaonyesha thamani ya mwanadamu kama heshima, huruma, wema na  kuwajali wengine vitu hivyo  ndio msingi wa kuendeleza uchangiaji damu wa hiari bila malipo yoyote.

Uchangiaji damu ni zoezi ambalo halina mwisho hivyo kila siku watu wanatakiwa kujitokeza kwa hiari kuchangia na inapotokea kuwa hakuna damu hali huwa mbaya  kwa wahitaji.

 UHITAJI WA DAMU NI MKUBWA

Licha ya ongezeka  la asilimia 60 kutoka 40  ya kiwango cha damu kwa kipindi cha mwaka jana hadi Januari mwaka huu , hivi sasa  ongezeko hili limeporomoka kutokana na kiwango cha uchangiaji damu kushuka.

Kushuka kwa kiwango cha uchangiaji damu kumefanya kiwango cha uhitaji damu kuongezeka katika hospiatali mbalimbali hapa nchini hasa zile kubwa.

Kwa sasa kila kukicha hospitali kadhaa zimekuwa zikihamasisha watu kujitokeza kuchangia damu huku wakitaja kuzingatia maelekezo ya wahudumu wa afya katika kujikinga na Covid-19.   

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji wa Mpango wa damu salama, Dk Avelina  Mgasa,   katika kipindi hiki  cha mlipuko wa homa kali ya mapafu  inayosababishwa na virusi vya corona(Covid-19)  kiwango cha uchangiaji damu kinaendelea kushuka siku hadi siku. 

Dk  Mgasa anasema takwimu zinaonesha kupungua kwa makusanyo ya damu kuanzia kipindi cha mwezi Aprili ambapo Mpango huo ulikusanya jumla ya chupa 22,044 ikilinganishwa na chupa 25,737 mwezi Machi na 31,502 mwezi Februari.

“Hali hii imechangiwa  na kufungwa kwa shule, vyuo, kukosa fursa ya kukusanya damu katika ofisi mbalimbali kwani kupitia haya makundi tulikuwa tunapata damu nyingi.

“Kitu kingine ambacho kimepunguza kiwango cha uchangiaji damu ni baada ya serikali kuweka zuio la mikusanyiko katika kukabiliana na corona hata mtu mmoja mmoja wanaogopa kufika kwasababu ya hofu,”anasema Dk. Mgasa . 

MIKAKATI YA KUONGEZA UCHANGIAJI DAMU 

Dk. Mgasa anasema kwasasa wamejipanga kuhakikisha uwepo wa uchangia wa damu ulio salama  kwa kuweka mikakati  mbalimbali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona katika vituo vya kuchangia damu

Anasema  hatua za kiafya zinazotumika ni uwepo wa maji tiririka na sabuni kwaajili ya kunawa mikono,vitakasa mikono,vifaa kinga kwa watumishi kama barakoa, apron/koti, gloves na Thermo scanner kwaajili ya kupima joto la mwili kwa kila mchangiaji damu.

“Tahadhari zingine tutakazozichukua ni kutakasa vitanda na vifaa vinavyotumiwa na wachangia damu,tutaweka mpangilio unaozingatia umbali kati ya mtu na mtu (social distance),”anaeleza.

Anasema katika utaratibu huo mpya watazingatia hatua muhimu sita kwa watumishi wa mpango wa damu salama ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanavaa vifaa kinga ambavyo ni pamoja na gloves na koti maalum.

“Mchangia damu ataelekezwa mahali pa kunawa mikono yake kwa maji tiririka na sabuni au kutakasa mikono yake kwa vitakasa mikono kabla ya kuchangia damu hii ikiwa ni pamoja na kupimwa joto la mwili.

“Mchangia damu  atapitishwa kwenye fomu yenye maswali mbalimbali yakiwemo maswali yanayohusu Covid -19 na mtumishi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama atajaza majibu katika fomu hiyo.

“Anayechangia damu  atafanyiwa vipimo vya awali ikiwemo kuangaliwa hali yake (physical assessment), msukumo wa damu (blood pressure) na kiwango cha damu (haemoglobin level) ili kuhakikisha kabla ya kuchangia awe  ana afya njema,”anabainisha Dk Mgasa . 

JE MWENYE CORONA ANARUHUSIWA KUCHANGIA DAMU?

Wataalamu wa afya wanathibitisha kuwa virusi vya corona huambukizwa kwa njia ya mfumo wa hewa na hatimaye kuathiri mapafu.

Virusi hivyo huweza kuingia mwilini kwa kupitia pua,mdomo na macho endapo mtu atakuwanavyo katika mikono yake.

Na hii ndio sababu hasa kwa wataalamu wa afya kusisitiza unawaji wa mikono wa mara kwa mara.

Dk Mgasa anasema hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha kuwa  virusi vya Corona vinaweza kuenea kwa njia ya damu.

MALENGO YA KAMPENI

Katika maadhimisho ya Mwaka huu , Mpango wa damu salama umeandaa timu za Halmashauri, Mikoa na Hospitali za Kanda huku kila moja ikitakiwa  kukusanya chupa 100, jumla ya  chupa 22,000 zinatarajiwa kukusanywa na timu za Kanda.

Dk Mgasa anasema maeneo yaliyokusudiwa katika kukusanya damu hizo ni Vyuo,Kambi za jeshi,Sehemu za wazi na maofisini.

“ Katika kampeni hizo pia tutawafundisha watumishi wa afya juu ya matumizi sahihi ya damu kwa wajawazito na wakati wa kujifungua.

“Mahitaji kwa mwaka 2020 ni chupa 550,000 ambayo ni asilimia 1 ya idadi ya wananchi kwa makadirio ya takwimu za mwaka 2020 au chupa 10 kwa kila wananchi 1000

“Tunalenga  kukusanya chupa 375,000 ambazo ni asilimia 70 ya mahitaji kwa mwaka huu, kwa kipindi kilichopita kuanzia  Juni mpaka Julai mwaka 2018 hadi 2019 chupa 309,376 zikusanywa na katika kipindi cha Juni   mwaka 2019 mpaka 2020 chupa za damu 322,693 zilikusanywa,”anafafanua Dk. Mgasa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,460FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles