Derick Milton, Simiyu
Siku moja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga kutoa siku saba kwa watumishi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakikisha wanachanga kufidia mashine ya Ultrasound iliyoibiwa hospitalini hapo, Katibu Tawala wa Mkoa, Jumanne Sagini ametengua uamuzi huo.
Sagini ametoa uamuzi huo leo Alhamisi Agosti 15, alipokutana na watumishi wa hospitali hiyo, ambapo ameeleza uamuzi wa Mkuu huyo wa Wilaya unawaonea baadhi ya watumishi waliokuwa likizo, wasiokuwepo kazini, wagonjwa au ambao walikuwa na ruhusa.
“Haiwezekani watumishi wote wahusike na wizi huo, kwani serikali ina vyombo vyake vya ulinzi na vina wafanyakazi wanaolipwa mishahara kwa kazi ya kuchunguza, hivyo suala hilo liachiwe vyombo hivyo ili viweze kufanya kazi yake na kumpata mhusika wa wizi wa kifaa hicho,” amesema.
Sagini amesema uamuzi wa mkuu wa wilaya ulikuwa sahihi kutokana na presha ya jambo lenyewe, lakini pia kitendo cha watumishi kushindwa hata kumtaja mhusika kupitia kura za maoni zilizopigwa juzi asubuhi ikiwa pamoja na kutokurejesha mashine kwa muda mrefu toka wizi umetokea Agosti 5.
“Kama Mkuu wa watumishi Mkoa, nilishtushwa na uamuzi wa mkuu wa wilaya hivyo nisingenyamaza kuona yanafanyika wakati kuna watalaamu ambao kazi yao ni kufanya uchunguzi kwa matukio kama hayo na kufanikisha mashine ipatikane.
“Hata mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama tulishtuka kidogo juu ya uamuzi wa DC, lakini tuliona alikuwa sahihi kutokana na nyie kushindwa kutoa ushirikiano ili mashine hii irudishwe, wengine mkaamua kwenda kulalamika kwenye vyama vyenu vya wafanyakazi,” amesema Sagini.
Jana Agosti 14, Kiswaga akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo aliwataka watumishi hao kuchanga kila mmoja kulingana na mshahara wake kufidia mashine iliyoibwa hospitalini hapo Agosti 5, mwaka huu.