27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA RUZUKU YA CUF LATUA BOT, TAKUKURU

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad, akiwasalimia wananchi wa Jimbo la Dimani, Zanzibar jana wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za ubunge wajimbo hilo
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharrif Hamad, akiwasalimia wananchi wa Jimbo la Dimani, Zanzibar jana wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za ubunge wajimbo hilo

Na ASHA BANI – dar es salaam

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, amemwandikia barua Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu, ili achukue hatua za kulishughulikia sakata la fedha za ruzuku zinazodaiwa kukwapuliwa na CUF upande wa Mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahimu Lipumba.

Maalim Seif ameandika barua hiyo yenye kumbukumbu namba CUF/HQ/AKM/003/017/01 na nakala nyingine kuzituma kwa mamlaka mbalimbali, ikiwamo kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), wanasheria wa chama hicho na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika barua hiyo, Maalim Seif ameambatanisha na barua alizoziita ni za njama za ufunguaji wa akaunti zilizoelezwa kufanyika NMB Tawi la Ilala na Temeke zilizofanikiwa kuingizwa kiasi cha Sh milioni 360.

Pia ameambatanisha barua ya kufukuzwa uanachama Lipumba katika vikao vya uamuzi vya chama kulikofanywa na Baraza Kuu.

Ameambatanisha pia barua ya kusitisha ruzuku yenye kumbukumbu namba HA.322/362/14/17 ya Oktoba 10, mwaka jana iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na kile alichokiita mgogoro ndani ya chama, hivyo hawezi kutoa fedha hadi hapo utakapoisha.

Katika barua hiyo kwa Profesa Ndulu, pia Maalim Seif ameambatanisha kumbukumbu za miamala ya fedha iliyofanyika.

Pia amesema chama hicho kinaendelea na taratibu za kukamilisha hatua za kisheria ili kuwafikisha mahakamani wahusika wote walioshiriki katika kuchukua fedha hizo, akiwamo Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi.

Alisema hiyo itakuwa kesi ya pili, ya kwanza ikiwa ni ile iliyokuwa mahakamani ikimshtaki Jaji Mutungi na Profesa Lipumba sambamba na wanachama wengine waliofukuzwa uanachama na vikao vya Baraza Kuu.

Maalim Seif alisema katika kesi ya pili, Jaji Mutungi atashtakiwa kutokana na madai ya kushirikiana na walalamikiwa wale wale kwa kufungua akaunti mpya ili wapewe ruzuku.

Alisema Jaji Mutungi amefanya hivyo huku akifahamu kuwa kuna kesi ya msingi iliyopangwa kusikilizwa Februari 2, mwaka huu mbele ya Jaji Kihiyo.

“Gavana, baada ya muhtasari huo wa utangulizi, kwa masikitiko makubwa leo nakuandikia barua hii kukujulisha kuwa njama za kuiba fedha za ruzuku ya CUF-Chama cha Wananchi zimefanikiwa kwa kufanya muamala wa jumla ya shilingi 369,378,502.64 toka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwenda akaunti namba 2072300456 ya NMB tawi la Temeke Januari 5, mwaka huu.

“Akaunti ambayo imetumika katika wizi wa fedha hizo ilifunguliwa Agosti Mosi, 2002 na viongozi wa CUF Wilaya ya Temeke kwa ajili ya kupokelea fedha zinazopangwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF,’’ alisema Maalim Seif.

Alisema ifahamike kuwa kila wilaya ya kichama ya CUF inayo akaunti inayotumika kupokelea fedha zinazopangwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa na hazihusiani na kupokea ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Hivi karibuni, CUF upande wa Maalim Seif ililalamikia hatua iliyochukuliwa na Jaji Mutungi kuwapa CUF upande wa Profesa Lipumba zaidi ya Sh milioni 360 za ruzuku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles