NA YAHYA MSANGI – LOME-TOGO
AJIRA kwenye Umoja wa Mataifa na taasisi zake au mashirika mengineyo ya kimataifa inategemea sana mambo haya: Elimu, ujuzi na uzoefu, msimamo wa nchi husika na uzalendo.
Ukilinganisha nchi za Afrika Magharibi, Afrika Mashariki na Kusini utaona kuwa katika Umoja wa Mataifa na taasisi zake na mashirika ya kimataifa wenzetu wa Afrika Magharibi wako wengi kuliko sisi wa huku Afrika Mashariki na Kusini.
Jaribu kutazama mashirika ya UN, FAO, IFAD, WB, WHO utauona ukweli huu. Pia watazame waliowahi kuwa wakurugenzi wakazi wa FAO, WHO, UNDP, UNCEF, WFP, ILO, WB nchini Tanzania utaona ukweli.
ELIMU, UJUZI NA UZOEFU
Ni lazima mtu awe na sifa zinazostahili pale nafasi ya kazi inapotangazwa. Tanzania ina wasomi waliokubuhu haswa, ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika. Kipindi cha awamu ya kwanza iliwekwa misingi mizuri sana ya elimu ambayo ilitoa wataalamu wa ngazi za kimataifa.
Kwa hili si kikwazo kwa Tanzania. Katika elimu kikwazo kikuu kwa Tanzania na nchi za Kusini mwa Afrika ni lugha! Nchi zetu zilipuuza sana elimu ya lugha za kigeni, hasa Kifaransa, Kireno na Kihispania.
Tatizo hili liko kila lililokuwa koloni la Mwingereza. Ni kosa la kutawaliwa na mkoloni ambaye lugha yake ndiyo lugha ya dunia. Hata UN japo kuna lugha kuu 6, lakini Kiingereza ndiyo lugha kuu.
Ripoti yoyote ya UN inatoka kwanza kwa lugha ya Kiingereza, ndipo inatafsiriwa kwenye lugha hizo nyingine! Mwingereza aliiweka sokoni lugha yake hasa kiasi haiepukiki kimataifa. Hiki ndicho kilifanya alitutawala tulemae!
Hatukupata kikwazo popote tuendapo, hasa UN. Wenzetu waliotawaliwa na Mfaransa, Mhispania na Mreno walilazimika kujifunza walau Kiingereza cha kuombea maji. Hata mitaani utakuta watu wanajua walau ‘How are you my friend’. Sisi ukimwambia mtu aseme hivyo kwa Kifaransa, Kireno au Kihispania utacheka hadi mbavu zichomoke! Tulilemazwa na mkoloni!
Nakumbuka nilipokuwa sekondari tulikuta somo la Kifaransa. Mwalimu alikuwa Mhaya mmoja akiitwa Kamugisha, alikuwa anaongea Kifaransa kwa mbwembwe hasa utadhani Jenerali Charles De Gaulle.
Ila alitufanya na sisi tupende Kifaransa. Enzi zile kulikuwa na ziara za matembezi katika shule za Ashira, Machame, Assumpta, Kibosho, Kibo hadi Jangwani Girls. Bahati mbaya Wizara ye Elimu ikapiga marufuku somo la Kifaransa mashuleni.
Nakumbuka siku Mwalimu Kamugisha alipokuja kutupa taarifa kuwa hakutakuwa na somo la Kifaransa tena badala yake kipindi kitakuwa cha kujifunza Kiingereza, ilikuwa kama tumefiwa.
Kisa hiki kinaakisi uzembe wetu wa kutojifunza lugha mbali ya Kiingereza, Kiswahili na Kipare. Ukitazama tangazo la nafasi ya kazi UN hutakosa kuona sehemu wanataka ujaze ufahamu wako wa lugha zinazotambulika UN. Hakuna Kichaga, Kimachame wala Ki-uru! Watu wetu wakifika hapo wanakwama au wanaogopa watakuja kuumbuka kwenye usaili.
Kama unawafahamu wakurugenzi wakazi waliowahi kuwapo Tanzania utakumbuka walau wanajua Kiingereza na Kifaransa. Ikiwa tunataka watu wetu waajiriwe UN na mashirika ya kimataifa, lazima serikali na wazazi wahimize vijana kujifunza lugha. Lugha haitawapa kuajiriwa bali kujiajiri pia. Anayejua Kiingereza, Kifaransa, Kireno na Kihispania hawezi kufa njaa. Ni ajira tosha. Siyo kila kijana anasukumwa kusoma kilimo, uhandisi, ugavi na biashara. Ukisoma lugha eti unachekwa!
MSIMAMO WA NCHI
Hii ni sababu ya pili. Mgawo ndani ya UN si kwa maeneo ya bahari au kura peke yake. Hata ajira zina mgawo zake! Lazima kuwe na uwiano wa ajira miongoni mwa nchi wanachama. Japo kuna baadhi ya taasisi wakubwa wamehodhi nafasi za juu, mathalani Benki ya Dunia, Shirika la Fedha, UNDP na wengine.
Sasa hivi kuna mshikemshike wa kumpata mkurugenzi mtendaji wa UNDP. Mama aliyepo anamaliza muda wake. Je, Tanzania hatutaki nafasi hii? Lakini hii haizuii nchi zetu kuulizia au kuhoji au kutaka nafasi.
Pia kuna nchi hazikubali kuletewa mkurugenzi mkazi asiye raia. Imewahi kutokea Nigeria, Ghana na baadhi ya nchi. Hivi Mtanzania atachaguliwa awe mkurugenzi mkazi Ukraine nao wakubali? Utaondoka tu na mabegi yako!
Sisi tukubali tumezembea kwa kiasi fulani na tumefeli kigezo cha lugha, hivyo imebidi tuwe wapole. Lakini tukiamua kama nchi hatushindwi kupata raia mwenye sifa. Pia hatushindwi kumkataa mteule toka New York au Geneva.
UZALENDO
Ukitazama wenzetu kuna uzalendo wa hali ya juu kuhusu hizi ajira, Mmoja akipata ajira 'anavuta' wenzake. Sisi tuna tatizo, mtu akipata basi anataka awe yeye tu peke yake aabudiwe. Na pia mtu akipata walio nyumbani badala ya kushirikiana naye wanamgeuza ni adui!
Matokeo yake wenzetu ndio wamejaa UN na mashirika ya kimataifa! Hii pia inatokana na serikali kutokuwa na orodha au kumbukumbu sahihi za raia wake walio UN na mashirika yake au ya kimataifa.
Wenzetu balozi zao huwaweka jirani na kuandaa vikao na kuweka mikakati ya namna ya kuvuta raia wao wengine. Niliwahi kuona balozi wetu mmoja aliyekuwa London, Mheshimiwa Sharrif akiandaa vikao vya aina hii enzi alipokuwa Uingereza. Lazima balozi zetu zipewe maelekezo kuangalia namna ya kuongeza waajiriwa wa UN katika maeneo yao.
Wizara yetu ya mambo ya nje itafute nafasi na kuzitangaza ili Watanzania wenye sifa watume maombi na wizara iwe refarii wao! Siyo kukalia taarifa za ajira ili waombe wao au ndugu zao tu. Natumai umejifunza kitu kama u mzalendo.