Sakata la kutafuna posho………..Vigogo wengine watatu wasimamishwa polisi

Projest Rwegasira
Projest Rwegasira
Projest Rwegasira

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

SAKATA la tuhuma za kufanya malipo hewa ya Sh 305,820,000 ambazo ni posho ya chakula (ration allowance) kwa watu ambao si askari lililosababisha kusimamishwa kazi kwa Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, Frank Msaki, limewageukia vigogo wengine watatu wa jeshi hilo.

Waliosimamishwa baada ya malipo hayo hewa kubainika kutokana na uchunguzi maalumu wa mkaguzi wa ndani unaoendelea hadi sasa ni Mhasibu Daraja la II, Damian Bupamba, Mhasibu Daraja la I, Ida Moyo na Mkaguzi Msaidizi wa jeshi hilo, Milambo Milambo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, vigogo hao walisimamishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara hiyo ilisema  Rwegasira alisema hatua hiyo ni mwendelezo wa uchunguzi wa tuhuma za kufanya malipo hewa ya kiasi hicho cha fedha zilizosababisha Msaki ambaye hakuwa askari kusimamishwa kazi.

“Kwa Mamlaka ya Katibu Mkuu chini ya Kanuni ya 35(2)(b) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003 zikisomwa pamoja na Kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, kuanzia Julai 13, 2016, amewasimamisha kazi Bupamba na Moyo kwa makosa ya kufanya malipo ya posho ya chakula kwa watu wasiostahili kwa kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha wa 2013/2014 hadi 2015/2016,” ilisema taarifa hiyo.

Pia taarifa hiyo ilisema kwa Mamlaka ya Katibu Mkuu chini ya Kifungu cha 7(4) cha Sheria namba nane ya Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi na Magereza  ya mwaka 1990 kama ilivyorekebishwa na Sheria namba nane ya mwaka 2015, kikisomwa pamoja na Kanuni C.23(1)(b) ya Kanuni za Utumishi wa jeshi hilo za mwaka 1995 zilizorekebishwa mwaka  2013, kuanzia Julai 13, mwaka huu, amemsimamisha kazi Milambo kwa makosa kama hayo.

Ilisema watumishi wote watatu wamehusika kufanya malipo hayo jambo ambalo ni kinyume na Kanuni F.9 ya Kanuni za Utumishi wa jeshi hilo za mwaka 1995 kama zilizovyorekebishwa mwaka 2013.

Taarifa hiyo ilisema Rwegasira amewasimamisha wahusika ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.

Sakata hilo la utumbuaji wa vigogo hao lilianza wiki iliyopita baada ya Msaki kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za madai ya kufanya malipo hayo hewa kwa kulipa posho ya chakula kwa watu ambao si askari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here