30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SAKATA LA BILLICANAS, NHC yagonga mwamba kwa Mbowe mahakamani

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi imetupa pingamizi lililowasilishwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) la kuitaka isisikilize maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ya kutaka arudishwe katika jengo alilonyang’anywa maarufu kama Billicanas.

NHC na Kampuni ya Udalali ya Poster and General Traders, waliwasilisha pingamizi la awali wakidai kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwasababu hakuna kesi ya msingi.

Hatua hiyo ya NHC na kampuni hiyo ya udalali ilikuja baada ya kampuni ya Mbowe inayofahamika kama Mbowe Hotels Limited, kuwasilisha maombi chini ya hati ya dharura ikiomba  mahakama iamuru wadaiwa wamrudishe katika ghorofa namba 007 lililopo Plot No. 725-726/24  Mtaa wa Mkwepu/Indira Gandhi (Makunganya), Manispaa ya Ilala yenye hati namba C. T No. 186018/15 and C. T No. 186018/10 kwani walimwondoa kimakosa.

Mahakama hiyo ilitoa zuio la muda la kupigwa mnada mali za Mbowe hadi hapo uamuzi wa pingamizi lililowasilishwa na NHC kuhusu maombi ya Mbowe utakapotolewa.

Jana mbele ya Jaji Sivangilwa Mwangesi, mahakama hiyo ilitupilia mbali pingamizi la NHC na kampuni ya udalali.

Kesi ya msingi ya Mbowe imepangwa kusikilizwa katika mahakama hiyo Septemba 27, mwaka huu mbele ya Jaji Mwangesi.

Katika kesi hiyo, Mbowe anawakilishwa na Wakili Peter Kibatala na Omari Msemo, wakati NHC inawakilishwa na Wakili Aloyce Sekule na Mariamu Mungula.

Kibatala katika kesi ya msingi anadai wadaiwa wote wawili Septemba mosi bila ridhaa ya mahakama walimwondoa mteja wake wakati usuluhishi ukiendelea kuhusu mkataba wa ubia walioingia Mbowe Hotels Limited na NHC kuhusu jengo hilo.

Kampuni ya udalali ilipewa na NHC kazi ya kumwondoa Mbowe katika jengo hilo kwa madai ya kushindwa kulipa kodi ya pango Sh bilioni 1.2.

Mbowe aliondolewa kwenye jengo hilo Septemba mosi, siku chache tu baada ya  NHC kutangaza orodha ya wapangaji wake ambao ni wadaiwa sugu ikiwemo kampuni hiyo ya Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles