26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SAIDA KAROLI: SITAFANYA MAKOSA TENA KWENYE MUZIKI WANGU

Na GLORY MLAY


MWANAMUZIKI mahiri katika muziki wa asili, Saida Karoli ambaye amepitia changamoto kubwa tangu alipopotea kwenye ramani ya muziki anaofanya hadi kuja kuibuka upya na kutamba tena kupitia wimbo wake wa ‘Salome’ uliorudiwa na mkali wa muziki wa Bongo Fleva, Diamond na Rayvan.

Saida Karoli ni mpambanaji kwani ameweza kupitia vikwazo kadhaa hadi kufanikiwa kurudi upya katika sanaa ya muziki na sasa anatamba na wimbo wa ‘Orugamba’ ambao ndiyo unaobeba jina la albamu yake ya kwanza yenye jumla ya nyimbo 17.

Juzi Saida alitembelea ofisi za New Habari (2006) na katika mahojiano yake na MTANZANIA ni kama ifuatavyo;

Mtanzania: Unadhani ulikosea nini kiasi kwamba ukashuka sana kisanii?

Saida Karoli: Mikataba mibovu ndiyo iliyonifanya nishuke kiasi hicho; nilikuwa nikipewa mikataba ya kiingereza wakati sikuwa nikijua kusoma wala kuandika, hivyo sikuwa nikijua kilichokuwa kikiandikwa kwenye mikataba ile.

Mtanzania: Inadaiwa kwamba ulidanganywa na mapromota wengine ukaachana na meneja wako wa kipindi hicho ukaenda kwao kuna ukweli?

Saida Karoli: Hapana kilichonirudisha nyumbani Bukoka kipindi hicho ni kuisha kwa mkataba, mimi nilikuwa sijui kusoma wala kuandika na meneja wangu aliniambia mkataba umeisha na hakutaka kuniongezea ningefanyaje ilibidi nirudi nyumbani kwetu.

Mtanzania: Mwanzo mikataba yako iliandikwa kwa kiingereza, ya sasa ikija tena kwa kiingereza itakuwaje?

Saida Karoli: Kwa sasa najua kusoma na kuandika vizuri lakini pia nafahamu kiingereza, mtu akizungumza naelewa lakini namjibu kwa Kiswahili pia hakuna ulazima wa mikataba kuwa kwa Kiingereza, nitaomba waiweke kwa Kiswahili.

Mtanzania: Sasa ni nini kinakufanya ujiamini kwamba hautashuka tena kisanii?

Saida Karoli: Kwanza sifikirii kusaini mkataba bila kujua faida yake na namna nitakavyoweza kunufaika na kazi yangu na pia nimeshajua makosa na udhaifu wangu wa kipindi hicho.

Mtanzania: Kwa hiyo kwa sasa upo chini ya uongozi gani?

Saida Karoli: Kwa sasa nipo chini ya uongozi ambao bado hatujakubaliana chochote isipokuwa wameamua kunisaidia ili nirudi kwanza kwenye chati yangu kisha ndio tutaangalia namna ya kufanya kazi nao.

Lakini pia wapo ambao hawapo tayari kujiweka wazi kwa sasa kwa kuwa hatujakubaliana chochote zaidi ya kunisaidia kimuziki.

Mtanzania: Kipindi hiki unachosema hamjakubaliana na uongozi mpya, sasa familia yako wakiwemo watoto wako wanaendelea kucheza kwenye kundi lako ama wanasoma?

Saida Karoli: Wanasoma nimewahamishia Dar es Salaam wanasomeshwa kwenye shule za hao viongozi wangu wapya, huku mipango mingine ikiendelea, awali walikuwa wakisoma Mwanza na Bukoba.

Mtanzania: Hivi ulipewa kiasi gani na Diamond baada ya kuurudia wimbo wako wa ‘Chambua kama karanga’?

Saida Karoli: Ni swali zuri, unajua hadi leo bado watu wanachanganya haya mambo mimi niliporomoka kisanii, Diamond aliponiomba arudie wimbo wangu sikuona ubaya nilifurahi kwa kuwa nilijua akiimba yeye kwa kuwa yupo juu ataweza kunirudisha, watu wakanikumbuka na waandishi wakanitafuta na kweli baada ya wimbo ule kama nimerudi upya na waandishi mnanitafuta mara kwa mara lakini sikulipwa fedha yoyote.

Mtanzania: Una mpango wowote wa nyimbo zako kufika kimataifa?

Saida Karoli: Ninao na juhudi zimefanyika, wimbo wangu umefika mbali huko duniani na kwenye filamu moja uliwahi kutumika ingawa sikupata chochote, lakini pia nimeona wasanii wa Uganda na Kenya baadhi yao wanatumia sehemu za nyimbo zangu huko nchini kwao.

Lakini pia napenda wasanii wa nje ndiyo waje kunifuata watake kushirikiana na mimi na si mimi niwafuate huko kwa kuwa muziki huu ni wa asili, una ladha yake tofauti na miziki yao.

Mtanzania: Ukikutana na Rais Magufuli utamwambia nini?

Saida Karoli: Napenda kumwambia rais atuunge mkono wasanii wa nyimbo za asili kama anavyofanya kwa wasanii wa nyimbo nyingine, mimi nimeenda nchi mbalimbali ikiwamo Burundi, Afrika Kusini na Kenya kwa ajili ya kuutambulisha muziki huu tukipata sapoti utazidi kujulikana zaidi ndani na kimataifa.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles