27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

SAGCOT YAPONGEZWA KUFANIKISHA MKATABA ZAO LA VIAZI

 

Na MWANDISHI WETU, MBEYA


SERIKALI imepongeza mpango wa nchi ya Uholanzi kupitia balozi wake hapa nchini kwa kuamua kuingia mkataba wa makubaliano wa kuendeleza kilimo cha zao la viazi mviringo na Tanzania na  kuhimiza mpango huo pia usiishie katika zao la viazi, bali ulenge na mazao mengine.

Pongezi hizo zimetolewa juzi jijini hapa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais (Tamisemi), Josephat Kandege ambaye alishuhudia utiliwaji wa saini wa mkataba wa nchi za Tanzania na Uholanzi uliofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mathew Mtigumwa na Balozi wa Uholanzi nchini, Jeroen Verheul, katika kilele cha siku ya wakulima ya Nanenane.

Alisema pia Serikali inaupongeza mpango wa kuendeleza kilimo nchini unaoendelezwa na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini (Sagcot) kwa kuwezesha nchi ya Uholanzi kuingia mkataba na Tanzania katika kuendeleza kilimo cha zao la viazi, lakini pia alishauri mazao mengine yaangaliwe ili kuchochea kasi ya uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.

Uholanzi na Tanzania zimeingia makubaliano ya ushirikiano katika kuendeleza zao la viazi, baada ya Uholanzi kuleta makampuni nane kutoka nchini humo ya watu binafsi ambayo yanakuja kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani.

Akizungumza kwenye kilele cha kuhitimisha Maonyesho ya Nanenane, Naibu Waziri Kandege alisema makubaliano hayo yamekuja wakati mwafaka katika awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ambayo inasisitiza wakulima na wananchi kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii ili kukuza uchumi wa taifa kwa kupitia uchumi wa viwanda.

“Nimeshuhudia tukio la uwekaji saini la makubaliano baina ya Tanzania na Uholanzi kuhusu kutengeneza mnyororo wa thamani wa zao la viazi, hii ni moja kati ya jitihada zilizofanywa na Sagcot Center Ltd, napenda kuipongeza Sagcot Center kwa kuendelea kushirikisha wadau na tayari kongani ya Ihemi kwa mikoa ya Iringa na Njombe inaendelea vizuri.

“Na kwamba Kongani ya Mbarali yenye mikoa ya Mbeya na Songwe tayari imezinduliwa, naupongeza uongozi wa Sagcot kuendelea kufanya kazi na Serikali ya mikoa na halmashauri ili kuhakikisha mkulima mdogo anaongeza tija katika uzalishaji,” alisema.

Kwa upande wake Balozi wa Uholanzi hapa nchini, Jeroen Verheul, alisema kupitia Sagcot wamefanya makubaliano hayo kwa lengo la kuleta tija katika zao la viazi kwa nia ya kuongeza uzalishaji wa viazi utakaowainua kiuchumi wakulima.

Alisema katika mpango huo wa kuendeleza zao hilo, Uholanzi imeweza kushirikiana na Sagcot kupitia mradi wa Stawisha (CD PIT) ambao ni mmoja wa wadau wa (Sagcot), watajenga kituo mahiri cha kuendeleza zao la viazi mviringo eneo la Uyole, jijini Mbeya sambamba na kuweka shamba darasa la viazi hivyo.

Naye Mkurugenzi wa Sagcot, Geoffrey Kirenga, alisema kuingia makubaliano kati ya Tanzania na Uholanzi kutatoa fursa kwa makampuni hayo nane kuwekeza katika sekta ya kilimo kwa kutatua changamoto iliyokuwepo kama upande wa mbegu ambapo jawabu limeshapatikana.

“Kwenye mbegu tulikuwa na aina tatu, sasa tunazo aina 11 za mbegu za viazi, kuna tatizo la viazi, wakulima wakivuna nusu vinabaki chini ya ardhi, hatuna majembe ya kuvunia viazi, lakini kuna majembe yamekuja hapa yatakuwa yanapatikana wakulima wetu na wataalamu watafundishwa namna ya kutumia,” alisema Kirenga.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles