28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

SADC yataka nguvu ya pamoja kuikabili corona

NORA DAMIAN – DAR ES SALAAM

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), zimetakiwa kuungana pamoja kukabiliana na ugonjwa wa corona na kuhakikisha mwenendo wa uchumi hauyumbi.

Akizungumza jana wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo, Katibu Mtendaji wa SADC, Dk. Stergomena Tax, alisema kushindana na janga hilo kunahitaji juhudi za pamoja. 

Mkutano huo ulifanyika kwa njia ya mtandao (video conference) kama hatua ya kupambana na ugonjwa huo na kuzingatia ushauri uliotolewa na mawaziri wa afya wa SADC waliokutana kwa dharura hapa nchini Machi 9.

“Corona ni janga la kidunia, pamoja na kupongeza Serikali zetu kwa jitihada ambazo wamechukua kupambana na ugonjwa huu, kushindana na janga hili kunahitaji juhudi za pamoja, wananchi wote wa SADC walichukulie janga hili kwa umuhimu stahiki na kutekeleza yale yote ambayo yanatolewa na wataalamu katika nchi mbalimbali,” alisema Dk. Stergomena.

Akifungua mkutano huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alizitaka nchi wanachama kuendelea kufuata taratibu za afya ili kudhibiti na kuzuia maambukizi ya corona.

“Hii ni vita kubwa, ambayo itagusa na kuathiri maendeleo yetu kwenye ukanda wa SADC na ni lazima tupambane nayo kwa kufuata kanuni zote za afya ili kuondokana na maambukizi.

“Imelazimu kuandaa mkutano huu kwa njia ya mtandao kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na mawaziri wa afya wa SADC walioshauri kupunguza mikutano ya ana kwa ana kupunguza uwezekano wa homa ya mapafu ambayo inasambaa kwa kasi kubwa sehemu mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na kwenye kanda yetu,” alisema Majaliwa. 

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi, alizitaka nchi wanachama kuendelea kushirikiana kuhakikisha mwenendo wa uchumi, biashara, uwekezaji na masoko ya fedha hayayumbi kutokana na hofu ya mlipuko wa ugonjwa huo.

KUHUSU MKUTANO

Waziri Mkuu Majaliwa alizitaka nchi wanachama kutobweteka na mafanikio yaliyopatikana badala yake ziongeze kasi ya utekelezaji wa maazimio mbalimbali kuhakikisha malengo ya SADC yanafikiwa.

“Tunaendelea kupiga hatua kubwa hadi sasa, lakini tunapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha malengo ya SADC yanafikiwa,” alisema Majaliwa.

Kwa mujibu wa Majaliwa, SADC pia iko katika maandalizi ya kuwa na mkakati mpya wa utekelezaji yale yote wanayoridhia kwa miaka 10 ijayo yaani 2020–2030, ambao utahakikisha unafikia malengo ya dira ya SADC ya 2020–2050.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Profesa Kabudi, alisema mpango mkakati elekezi wa kanda wa 2015/20 na awamu ya pili ya mpango mkakati wa asasi ya siasa, ulinzi na usalama inafikia ukomo wake mwaka huu, hivyo akaitaka sekretarieti kuanza maandalizi ya mipango mingine.

Kuhusu dira ya 2050 ya jumuiya hiyo, Profesa Kabudi aliitaka sekretarieti kuharakisha mchakato huo na kusisitiza ushirikishwaji wa wadau upewe kipaumbele katika kila nchi wanachama wakiwemo kutoka sekta binafsi, asasi za kiraia, taasisi za kitafiti na elimu.

“Ni muhimu tukatafakari ni kwa jinsi gani dira hiyo itakuja kutatua changamoto za jumuiya na zile zinazoikabili dunia kama vile upatikanaji wa ajira kwa vijana, jamii yenye mahitaji maalumu na kuwezeshwa kiuchumi kwa wanawake.

“Tuandae dira itakayoongeza kasi ya utekelezaji wa masuala ya mtangamano na itakayowezesha ufadhili endelevu wa miradi ya jumuiya kwa ajili ya ustawi wake,” alisema Profesa Kabudi.

Alisema jumuiya hiyo bado inakabilwia na changamoto za migogoro ya kisiasa, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya asili, ongezeko la idadi ya watu, ukuaji wa miji, elimu, afya pamoja na kupungua kwa kasi ya uchumi na masuala ya utawala.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles