23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

SADC-DFRC KUFADHILI UTEKELEZAJI MAENDELEO VIWANDA

Na LEONARD MANG’OHA



BAADA ya nchi zote za Afrika kupata uhuru kutoka kwa wakoloni, jumuiya mbalimbali zilizaliwa na zikiwa na jukumu la kuhakikisha zinapambana na matatizo ya ndani ya bara hilo kwa lengo la kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi wa watu wake.

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) iliamua kuunda chombo kinachofahamika kama……..SADC-DFRC kilichopewa jukumu la kuhakikisha kinazisaidia taasisi za fedha za maendeleo (DFI) katika mataifa wanachama kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Mbali na kujenga uwezo, pia ina jukumu la kufanya tafiti mbalimbali, kusaidia kupatikana sera wezeshi na rafiki za uwekezaji na kusaidia kutoa mafunzo kwa wataalamu wa taasisi za fedha za nchi wanachama ili kuwawezesha kutoa mafunzo kwa watu walio tayari kuwekeza.

Kwa sasa mtandao huo umeweza kujitanua kwa kufikisha jumla ya wanachama 37 (taasisi za fedha za maendeleo) katika mataifa yanayounda SADC.

Wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Taasisi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, wajumbe walipata nafasi ya kujadili kuhusu namna ya kuelekea uchumi wa viwanda kwa maendeleo endelevu na jumuishi na wajibu wa DFIs ndani ya SADC.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa SADC-DFRC, Stuart Kufeni, anasema wamejikita katika eneo hilo kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika maendeleo ya SADC kama silaha muhimu ya kufanikisha ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu katika katika SADC na kuchochea ustawi wa maisha ya watu wake.

Anaamini mafanikio ya utekelezaji wa mkakati na mpango wa uendelezaji wa viwanda wa SADC, unahitaji uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali zitakazosaidia ukuaji wa haraka wa viwanda, hivyo taasisi za fedha za maendeleo kwa ushirikiano na sekta binafsi zitashiriki kikamilifu katika kukusanya nguvu ya upatikanaji wa rasilimali fedha.

Kufeni anasema kuna umuhimu wa DFIs kuchukua jukumu la upatikanaji wa rasilimali fedha kuhakikisha ufikiaji wa malengo ya maendeeo ya kitaifa na kikanda chini ya mpango mkakati elekezi wa maendeeo wa SADC (2015-2020).

“Ili kuzalisha ajira na kuondoa umasikini na kuweka usawa miongoni mwa wananchi, ni lazima kuwa na uchumi unaotegemea viwanda zaidi, ndio maana tumekuja hapa Tanzania kuona nini inafanya kukuza sekta hii muhimu,” anasema.

Anaeleza kuwa kwa sasa wako kwenye mchakato wa kuanzisha mfuko maalumu utakaokuwa na jukumu la kuibua na kuandaa maandiko ya miradi ya maendeleo.

Mfuko huu utakuwa ukipata fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali vya ndani na nje ya SADC ikiwamo taasisi za kifedha za kimataifa.

Miongoni mwa maeneo yanayolengwa na DFRC ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu mizuri katika maeneo ya uwekezaji kama vile barabara na miundombinu ya maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Taifa(NDC), Ramson Mwilangali, anasema wamekuwa sehemu ya uanzishwaji wa chombo hicho na kwa sababu wao ndiyo wenye mamlaka ya kupokea na kufanyia uchambuzi miradi mbalimbali, kunarahisisha upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi hususani iliyoandikwa kwa kuzingatia matakwa ya DFRC.

Anasema wanapopokea miradi na kuifanyia uchambuzi, huelekezwa katika taasisi za fedha za maendeleo za ndani ambako zinaweza kupata uwezeshaji kama fedha zinapatikana na ikiwa hakuna fedha taasisi hizo zinawasiliana na taasisi nyingine ndani ya SADC kupata ufadhili.

Anasema DFRC imesaidia katika uandishi, uchambuzi wa miradi na namna ya kuendesha miradi hiyo kwa kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa DFIs za nchi wanachama.

Anasema kwa Tanzania utekelezaji wa maendeleo ya viwanda unaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2021 unaolenga kufikia uchumi wa viwanda.

Moja ya hatua kubwa zilizofikiwa na mtandao huu wa kifedha ni kuwezesha DFI ya taifa moja kuweza kushirikiana na nyingine kutoka taifa jingine kuweza kupata fedha za kufanikisha utekelezaji wa mradi Fulani, jambo linalopunguza changamoto ya ukosefu wa fedha kwa miradi mbalimbali.

Kwa ushahidi hai, Patrick Mongela anasema mtandao wa DFRC umesaidia katika uandikaji wa mradi wa bwawa la maji la Kidunda unaolenga kupunguza adha ya ukosefu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya jirani, huku ukitarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 300 hadi kukamilika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Francis Assenga, anasema kupitia mkutano wa mwaka huu walilenga mawazo ya wadau mbalimbali ndani ya jumuiya ili kuondoa vikwazo vinavyokwamisha maendeleo ya viwanda.

Mkurugenzi wa Mipango na Ushirika wa Benki ya TIB Maendeleo, Patrick Mongela, anasema DFI zimesaidia kurahisisha upatikanaji wa fedha za miradi kutokana na kutoa mikopo ya gharama nafuu tofauti na benki za kibiashara.

Anasema taasisi hizo zinatoa fedha za miradi hata kama utekelezaji wa mradi husika haujaanza ambapo benki za kibiashara ni lazima mradi uwe umeanza utekelezaji.

“Sisi tunatoa hata msaada wa kutayarisha maandiko ya mradi ili kuuwezesha kuwa na ufanisi, kwa sababu sisi hatufanyi hivyo kwa lengo la kupata faida,” anasema Mongela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles