Upendo Fundisha, Mbeya
Serikali imevitaka Vyama vya Ushirika na Vyama wa Akiba na Mikopo (Saccos) nchini kuwekeza kwenye viwanda vikubwa ili kukuza uchumi wao na nchi kwa ujumla.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika wakati akizindua maonyesho ya maadhimisho ya vyama vya ushirika duniani ambapo kitaifa yanafanyika mkoani Mbeya.
“Viwanda hivyo vitasaidia kubadilisha mfumo wa maisha ya wazalishaji kwani bidhaa nyingi za mazao zitakidhi viwango vya ubora na kukamata soko la kimataifa,” amesema Ntinika ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini, Theresia Chitumbi, amesema vyama hivyo vinakabiliwa na changamoto ya elimu ya fedha hivyo kushindwa kufikia malengo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Kahama Cooperative Union, Emmanuel Charahani, ameiomba Serikali kuwasaidia kutafuta masoko ya bidhaa zao kwani uwezo wa kuanzisha viwanda wanao kulingana na mitaji wanayoimiliki kuwa zaidi ya Sh bilioni 30.