25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Sababu ya Trump kutoingia vitani dhidi ya Iran

>>Wasiwasi mkubwa kwa Marekani ni bei ya mafuta, ambayo inaweza kupanda kwa kiasi kikubwa endapo tu itaingia kwenye vita na Iran, moja kati ya mataifa yenye utajiri mkubwa wa nishati hiyo.

 HASSAN DAUDI Na MITANDAO

KINACHOENDELEA sasa katika siasa za kimataifa ni tishio la kuibuka kwa vita kati ya Marekani na Iran. Ni baada ya ndege ya kivita ya Marekani kulipuliwa siku chache zilizopita ilipoingia katika mpaka wa Iran.

Kumekuwapo na uhusiano mbovu kati ya nchi hizo mbili kwa miaka mingi sasa, na hivi karibuni Rais wa Marekani Donald Trump, alisma kuwa Iran ingeachana mara moja na mpango wake wa silaha za nyuklia.

“Haikubaliki wao kuwa na silaha za nyuklia. Hatutaiacha Iran iwe na silaha za nyuklia. Ikiwa watakubali, basi (Iran) litakuwa taifa tajiri. Watakuwa na furaha na nitakuwa rafiki yao mkubwa. Nafikiri itakuwa hivyo,” anasema Rais Trump.

Baada ya ndege ya Marekani kutunguliwa, ndipo alipoibuka Rais Donald Trump na kusema alitaka kuishambulia Iran lakini alisitisha uamuzi wake huo baada ya kugundua kuwa angesababisha vifo vya wananchi 150.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha NBC, Rais Trump aliifafanua kauli yake hiyo aliyoitoa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Nilifikiria kuhusu hilo (shambulio) kwa sekunde, ndipo nikaposema ‘unajua nini, waliilipua ndege isiyo na abiria lakini sisi tutaua watu 150 ndani ya nusu saa tu baada ya kauli yangu ya kuruhusu. Sikupenda iwe hivyo, sikudhani kuwa ingekuwa sahihi.”

Licha ya kuachana na mpango wake huo, bado wachambuzi wa siasa wanaamini kuna moshi unaofuka kati ya pande hizo, hivyo huenda ulimwengu ukashuhudia mataifa hayo yakiingia vitani katika siku za usoni na hoja hiyo inajengwa na sababu mbalimbali.

Mosi, kwa muda mrefu, Rais Trump amekuwa akifahamika kuwa ni kiongozi anayependa kuhofiwa na wapinzani wake. Wengi wataikumbuka kauli yake ya mwaka juzi, alipowaambia Korea Kaskazini kwamba angewawashia moto ambao haujawahi kushuhudiwa tangu kuanza kwa ulimwengu.

Rais wa Iran, Hassan Rouhan

Kama ni mfuatiliaji mzuri wa siasa za kimataifa, basi utakumbuka kuwa kauli hiyo aliwahi pia kuitoa dhidi ya Iran miezi mingi iliyopita.

Pili, aina ya washauri alionao Rais Trump wanaweza kusababisha Marekani iishambulie Iran hivyo, kuzuka kwa vita kati ya nchi hizo. Kwa kumtolea mfano, hivi sasa mshauri wake wa masuala ya usalama ni John Bolton.

Haijasahaulika kuwa Bolton amekuwa akiishinikiza kwa muda mrefu Marekani kuisambaratisha Iran. Ukiacha huyo, yupo Katibu Mkuu wa Serikali ya Marekani, Mike Pompeo, ambaye ni shabiki mkubwa wa sera zinazoikandamiza Iran.

Lakini pia, ibaki kwenye kumbukumbu kuwa Rais Trump pia amekuwa akipata shinikizo kubwa kutoka kwa waumini wa Dini ya Kikiristo nchini Marekani, ambao wamekuwa wakitetea sera za ukandamizaji dhidi ya Iran.

Tangu utawala wa Rais Bush, viongozi wa dini hiyo walikuwa wakimlazimisha kuishambulia Iran, baadaye walimkosa vikali Barack Obama kwa majaribio ya kukutana mezani na Iran, ikiwa haijasahaulika pia mwaka jana walimpongeza Trump kwa kitendo chake cha kujitoa katika mazungumzo ya mpango wa nyuklia.

Tatu, Rais Trump anaweza kuishambulia Iran kwa lengo la kutunza heshima yake mbele ya Wamarekani. Haijasahaulika kwamba wakati wa kampeni alisema hakuna shambulio la kisiasa dhidi yake litakaloachwa bila kujibiwa.

Aliwaahidi wapiga kura wake kwamba atakapochokozwa, atajibu, tena kwa kishindo kikubwa zaidi ya kile kilichofika dhidi yake.

Hata hivyo, kwa jicho la tatu, wapo wachambuzi walioibua hoja kwamba si rahisi kumuona Rais Trump akithubutu kuinua silaha zake kuishambulia Iran. Sababu za madai hayo ni kama ifuatavyo:

Tayari kiongozi huyo ameonekana kukinzana na alichokifanya aliyekuwa rais wa 43 wa Marekani, George W. Bush, kule Iraq. Mara kadhaa Rais Trump amekuwa akiponda uamuzi wa kulivamia taifa hilo la Kiarabu, akisema uamuzi huo ulikuwa wa hovyo.

Aidha, haijasahaulika kuwa kwa vipindi viwili ambavyo Marekani ilikuwa kwenye vita Mashariki ya Kati, si tu idadi kubwa ya wanajeshi wake walipoteza maisha, bali pia iliwagharimu kiasi kikubwa cha fedha, hivyo kuyumbisha uchumi wa nchi hiyo.

“Vita dhidi ya Iran itakuwa ni kosa kubwa,” anasema Seneta Tim Kaine katika mdahalo wa hivi karibuni na kuongeza:

“Baada ya miaka 18 ya vita mbili kule Mashariki ya Kati, zote tukituma vikosi vyetu, hatutakiwi kuingia kwenye ya tatu.”

Rais Trump alianza kulisema hilo mwaka 2016, wakati wa mdahalo wa Chama cha Republican, kabla ya kuirudia kauli yake baada ya kushinda kiti cha urais, alipodai ni uamuzi mbovu kuwahi kufanywa na rais yeyote katika historia ya Marekani.

Ni kwa hali hiyo basi, unaweza kuona uzito uliopo kwa Rais Trump kuishambulia Iran, akihofia atafanya kile alichokiponda katika utawala wa rais mstaafu, Bush.

Katika hatua nyingine, inaweza kuwa ngumu kuiona Marekani ikikubali kuingia vitani dhidi ya Iran kutokana na hali ya uchumi katika taifa hilo linalokabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa China.

Kipindi hiki kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwakani, ni wazi Rais Trump anafahamu wazi kuwa anachopaswa kukipa kipaumbele kwa sasa ni uchumi ili kuweza kukitetea kiti chake.

Wasiwasi mkubwa kwa Marekani ni bei ya mafuta, ambayo inaweza kupanda kwa kiasi kikubwa endapo tu itaingia kwenye vita na Iran, moja kati ya mataifa yenye utajiri mkubwa wa nishati hiyo.

“Tunatakiwa kujiweka mbali na chochote kile kitakachotuingiza katika migogoro ya muda mrefu,” anasema Laura Ingraham, mtangazaji wa vipindi vya televisheni, ambaye pia ni shabiki mkubwa wa Rais Trump.

Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, Rais Trump hajasahau kuwa moja kati ya ahadi zake ni kutoiingiza Marekani katika matatizo na mataifa mengine, kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Bush.

Kikiwa kimebaki kipindi kisichozidi mwaka mmoja, anahitaji kuipuuza Iran kwa kuwa endapo ataishambulia, basi atakuwa amekiuka ahadi aliyowapa wananchi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles