31.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU YA PUTIN KUTOJIBU MAPIGO MASHAMBULIZI YA MAGHARIBI SYRIA                                                                          

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


ALIKABILIWA na chaguo mbili; kukabiliana kijeshi na Marekani, Uingereza na Ufaransa au kusindikiza kwa macho bila kuchukua hatua wakati mshirika wake Syria akipigwa mabomu na Wamagharibi hao.

Lakini kati ya machaguo hayo mawili, Rais wa Urusi Vladimir Putin kinyume na ilivyotarajiwa na wengi hata Wamagharibi wenyewe waliojawa na hofu, aliamua kuchagua lenye mwelekeo wa amani.

Mwitikio huo wa uangalifu unaweza kuitia doa taswira yake kama kiongozi mbabe na mwenye nguvu zaidi duniani huku wengine wakimhesabu ‘kumbe mwoga’, taswira ambayo yeye mwenyewe anaichukia!.

Lakini pia kiuhalisia kilichotokea, hakitaathiri mafanikio yake nchini Syria wala kudhoofisha kwa mamlaka na ushawishi wake nyumbani nchini Urusi.

Ikulu ya Urusi, Kremlin ilikuwa imeionya Washington kuwa Urusi itakabili vikali shambulio lolote litakalogusa askari wake waliopo Syria.

Magharibi ziliheshimu mstari huo mwekundu kwa kuitaarifu juu ya shambulio lao la Jumamosi nchini humo, kama ilivyotokea mwaka mmoja uliopita wakati ziliposhambulia jeshi la anga la Syria.

Ikumbukwe kipindi hicho Urusi ilibakia kimya lakini safari hii ilikuwa imetishia ikiapa kwa ‘miungu yote’ itajibu mapigo.

Awali dunia ilihisi pengine itashuhudia vita, ambayo haikupata kutokea duniani baina ya pande mbili zenye nguvu kubwa za nyuklia, ikapata ahueni kuwa angalau sasa hakuna vita hiyo ya tatu ya dunia.

Hata hivyo, ahueni hiyo inaweza ikawa ya muda kwa vile mashambulizi yaliyofanywa na Magharibi wengi hawaamini kama yamefanikiwa makusudio yake kama yanavyojigamba.

Utawala  wa Rais Donald Trump wa Marekani uliweka  wazi kuwa  mashambulizi dhidi  ya mpango wa  silaha za sumu wa  Syria yalikuwa  na  lengo moja;

Kumzuia Rais wa Syria, Bashar al-Assad  kutumia silaha  kama hizo tena dhidi ya raia kama ilivyotokea Aprili 7 katika Mji  wa Douma, ambako watu zaidi ya 80 wengi wao wakiwa wanawake na watoto waliuawa. Urusi inasisitiza wataalamu wake hawakuona dalili za sumu.

Kwa sasa kilichoonekana wazi ni Marekani, Uingereza na Ufaransa zilikuwa waangalifu mno hasa kutokana na tisho la Urusi pamoja na kuepuka lawama za Jumuiya ya kimataifa, zikilenga maeneo, ambayo yanahusishwa na utengenezaji na uhifadhi wa silaha za sumu tu nchini humo.

Ni kwa vile mataifa hayo hasa Marekani yana rekodi mbaya katika nchi mbalimbali, ambako zimezusha vita kama vile Irak, Afghanistan na Pakistan ambako mashambulizi yao mara nyingi hayakosi kuua raia wengi wasio na hatia.

Lakini Idadi ya raia walioathirika na mashambulizi ya Jumamosi nchini Syria kufikia sasa na baada ya tathmini ya yaliyojiri ni kama vile kimsingi hakuna.

“Pamoja na washirika wetu, tulihakikisha Warussia wametahadharishwa kabla,” alisema Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Florence Parly.

Putin alilaani mashambulizi ya Jumamosi kuwa kitendo cha uchokozi ambacho kitasababisha janga la kibinadamu nchini Syria na kina uwezekano mkubwa wa kubomoa mfumo mzima wa uhusiano wa kimataifa.”

Aliikosoa Washington na washirika wake kwa kushambulia bila kusubiri wakaguzi kutoka shirika la kimataifa la silaha za kemikali kuitembelea Douma, nje kidogo ya Mji Mkuu Damascus.

Jeshi la Urusi lilisema kwamba mifumo yake ya ulinzi katika kambi mbili nchini Syria iliweza kuangusha sehemu ya makombora lakini haikujibu mapigo.

Iwapo mpambano ungetokea haingekuwa rahisi kuzuia maafa, mwelekeo wa hatari, ambao ulilinganishwa kwa kiasi kikubwa na mgogoro wa makombora wa Cuba mwaka 1962, wakati dunia almanusura iingie katika vita ya nyuklia.

Mitandao ya jamii ya Urusi ilijaa kauli za kizalendo lakini ikimshutumu vikali Putin kwa kushindwa kumlinda mshirika wake Syria.

Katika jimbo ililolimega kutoka Ukraine la Crimea, waandamaji walichoma picha za viongozi wakuu wa Marekani, Ufaransa na Uingereza, ambayo Waziri wake Mkuu Theresa May mapema wiki hii alikabiliwa na hasira za wabunge kwa kuipeleka nchi vitani bila ridhaa yao.

Hata hivyo, udhibiti mkubwa wa Kremlin katika vyombo vya habari ulimsaidia Putin kuepuka hasara kubwa kwa taswira yake aipendayo ya kiongozi mbabe na mwenye nguvu duniani.

Lakini pia, msimamo wake wa uangalifu umesaidia kukuza umaarufu zaidi katikati ya wasiwasi wa vita ulioikumba Urusi yenyewe na dunia kwa ujumla.

Katika siku za karibuni vyombo vya habari vya serikali nchini humo vimekuwa vikitoa angalizo kwa raia kujiandaa na uwezekano wa vita, vikitoa mbinu za kujilinda iwapo utatokea mgogoro wa nyuklia.

Vyombo hivyo pia hasa vya serikali au vyenye uhusiano nayo vilimlinganisha Rais Putin na Rais Trump; vikimweleza Putin kama kiongozi mwenye sifa zote za urais na mwenye maamuzi makini kwa dunia.

Vikamtaja Trump kama kiongozi anayetawaliwa na pupa pasipo kufikiria kuhusu maamuzi yake na ambaye ni rahisi kuiingiza dunia katika machafuko.

Kremlin pia inatumia mgogoro huo kujenga taswira ya kichokozi ya Magharibi jinsi walivyokaribhia kuiingiza dunia katika machafuko na namna wanavyokiuka sheria za kimataifa ikiwamo kuishambulia Syria bila ridhaa ya Umoja wa Mataifa.

Maofisa wa Urusi na wabunge wanalinganisha hilo na uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Irak mwaka 2003 kwa madai utawala wa Rais Saddam Hussein umetengeneza silaha za maangamizi, tuhuma ambazo zilikuja thibitika kuwa uongo na ambazo zinaifedhehesha Marekani na Uingereza hadi leo hii.

Wachambuzi wa mambo nchini Urusi walieleza kuwa Trump na May walizindua shambulio hilo ili kupoteza mwelekeo wa matatizo ya kisiasa yanayowakabili nyumbani.

Uchambuzi huo unaweza ukawa na ukweli kwa sasa Ufaransa inaisihi Marekani isiondoe askari wake kutoka Syria kama ilivyopanga, Marekani ikisisitiza haina mpango wa kuendelea kuwa huko.

Msimamo huu wa Marekani unaonesha kwamba haina nia au ari ya kuendeleza mgogoro wa mrefu nchini humo na kilichotokea Jumamosi basi tu- kuionesha dunia ile Marekani ya kipolisi duniani bado ipo!.

Katika mgogoro wa sasa, Putin ameishia kuitisha mkutano wa dharura katika Baraza la usalama la Umoja wa Matarifa.

Hakuna hatua za kijeshi zilizotangazwa mara moja lakini kuna ashirio la dhahiri kwa Marekani na washirika wake kuwa Urusi inaweza kuisaidia Syria dhana za kivita ikiwamo za kujilinda ukizingatia Moscow kwa muda mrefu imekuwa ikizingatia maombi ya Magharibi ya kutoipatia Damascus makombora. Lakini sasa bila shaka itafikiria hilo upya.

Lakini pia uangalifu wa Putin katika mgogoro huu unatokana na taifa lake kuwa mwenyeji wa Michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika siku 58 zijazo katika viwanja mbalimbali nchini Urusi.

Kwa hali hiyo hangependa kuhatarisha au kuvuruga maandalizi ya michuano hiyo mikubwa kuliko yote duniani ukizingatia mzozo wake wa karibuni na Uingereza kuhusu kulishwa sumu kwa kachero wake wa zamani nchini humo ulitishia kuyavuruga.

Uingereza ilitishia kushawishi washirika wake waisuse michuano hiyo huku ikifuta mpango wa awali wa ukoo wa Kifalme kuhudhuria sherehe za ufunguzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles