23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

SABABU YA MKUDE KUPORWA UNAHODHA YABAINIKA

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya uongozi wa Simba kumtangaza beki Method Mwanjale kuwa nahodha wa timu hiyo, MTANZANIA limebaini sababu za Jonas Mkude kuvuliwa cheo hicho.

Katika mabadiliko hayo yaliyotangazwa juzi, kuanzia msimu ujao Mwanjale ambaye ni raia wa Zimbabwe atakuwa nahodha mkuu wa Wekundu hao, huku akisaidiwa na John Bocco na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Chanzo cha habari kutoka katika kambi ya Simba iliyoko nchini Afrika Kusini, kimeliambia gazeti hili kuwa uamuzi huo ulikuja baada ya mchezaji huyo kubainika kuposti ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram akizungumzia madai ya timu hiyo kuchapwa mabao 7-0 na timu ya Royal Eagle katika mchezo wa kirafiki.

Mkude anadaiwa kuposti ujumbe huo baada ya mchezo kati ya timu hizo kabla ya kuuondoa muda mfupi baadaye.

Kikosi cha Simba ambacho kipo nchini humo kwa maandalizi ya mechi ya Ngao ya Jamii na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kinadaiwa kupokea kichapo hicho katika mchezo uliofanyika Juni 26, kwenye Uwanja wa King Zwelithini.

“Kilichomponza Mkude ni tabia yake ya kusema ukweli ambayo mara kadhaa amejikuta akiingia matatizoni na uongozi, hata hili la kunyang’anywa unahodha ni matokeo ya kuandika Instagram kwamba, mashabiki wasiwe na shaka kwa timu yao kufunga mabao 7 katika mechi ya kirafiki.

“Unajua kitendo chake kiliwaudhi sana viongozi, ukumbuke tayari walishakanusha sasa yeye akawa kama anawaumbua na kama unavyojua mkubwa ni mkubwa tu,” kilidai chanzo hicho

“Ukweli ni kwamba, hakuna kitu kingine alichofanya hadi  kusababisha kuvuliwa uongozi, mimi naweza kusema jazba ilitumika zaidi badala ya busara matokeo yake mjadala umekuwa mkubwa zaidi.”

Mkude anadaiwa kuwataka mashabiki wa Simba kutulia licha ya matokeo hayo kwa kuwa wapo kwenye michezo ya maandalizi si Ligi Kuu.

Ujumbe wa Mkude unadaiwa kusomeka hivi; Wanasimba tulieni tupo ‘pre season’, hizi goli saba hatujafungwa katika ligi na wala si mechi rasmi, bali ni mazoezi tu.”

 

Simba itashuka dimbani Agosti 23 kuikabili Yanga katika pambano la Ngao ya Jamii litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles