27.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 4, 2023

Contact us: [email protected]

Sababu wanaume kutooa wanawake wenye fedha

Na MWANDISHI WETU

UMEWAHI kumwona profesa mwanamke aliyeolewa na mwanamume mwenye elimu ya darasa la saba? Inaweza kuwa vigumu lakini si ajabu kusikia profesa mwanamume amemwoa mwanamke wa darasa la saba. 

Pia, ni nadra kwa mwanamke tajiri kuwa na uhusiano wa kudumu na mwanamume fukara ingawa kinyume chake inaweza kuwa kawaida. 

Kwa kuchunguza namna wanaume na wanawake wanavyohusiana katika jamii, jambo moja ni dhahiri. Wanawake wenye mafanikio, iwe kielimu, kiuchumi na kiroho wanakuwa na wakati mgumu kuanzisha na kudumisha uhusiano wa kudumu na wanaume wasio na mafanikio makubwa. 

Hata wanaume wenye mafanikio nao husita kuwa na uhusiano wa kudumu na wanawake wenye mafanikio kama yale waliyonayo wao. Jambo la kushangaza kidogo ni kuwa wanaume hawa wenye elimu kubwa, uwezo wa kifedha na hata hadhi kubwa katika jamii, wanavutiwa na wanawake wasio na mafanikio. Ni nadra kwao kuvutiwa na kuanzisha uhusiano endelevu na wanawake wanaofanana nao kimafanikio. 

Kwa mfano, ni rahisi kusikia mwanamume mwenye kiwango cha juu cha elimu, amevutiwa na mwanamke mwenye kiwango cha chini kidogo cha elimu. Inakuwa vigumu kwa mwanamke mwenye kiwango cha juu cha elimu kuanzisha na kuendeleza uhusiano na mwanamume mwenye kiwango cha chini cha elimu. 

Inapotokea, mathalani mwanamke anamzidi au analingana kiwango cha elimu na mwanamume anayempenda, basi utakuta mwanamume huyo ana namna ya kufidia tofauti hiyo ya kielimu. Kama si uchumi, basi itakuwa ni umri, madaraka, hadhi au umaarufu alionao katika jamii. 

Kusema hivyo haimaanishi kuwa wanaume hawawezi kabisa kuanzisha na hata kuendeleza uhusiano wa kimapenzi na wanawake waliowazidi mafanikio. Kilicho dhahiri ni kwamba uwezekano wa uhusiano wa namna hiyo kutokea ni mdogo. 

Inapotokea hata kwa nadra, jamii humshangaa mwanamume anayethubutu kuvunja utamaduni huo wa kumzidi mwanamke. Sababu inayotajwa ni kuwa wanawake wenye mafanikio hawana nidhamu ya ndoa. 

Ni dhahiri kuwa nafsi za wanaume wengi zinahitaji kujisikia kuwa kichwa cha familia. Wanahitaji wawe na sauti inayosikika, yenye uwezo wa kuelekeza na hata kudhibiti namna mambo yanavyokwenda kwenye familia.  

Kwa sababu hiyo, imejengeka dhana kuwa mwanamke mwenye mafanikio anakuwa na uwezekano mdogo wa kunyenyekea chini ya mamlaka haya ya mwanamume tofauti na mwanamke asiye na mafanikio. 

Kwamba, wanawake wanapopata elimu, hawawi tayari kuwa chini ya utawala wa mwanamume. Hofu hiyo huwanyima wanaume hali ya kujiamini na kuthubutu kuanzisha na kudumisha uhusiano na wanawake wenye mafanikio.

Hata hivyo, dhana hii inaweza isiwe sahihi. Hakuna uthibitisho kuwa mamlaka ya mwanamume yanayompa hadhi ya kichwa cha familia yanategemea hali yake ya kiuchumi, kielimu na umri.  

Kwa mfano, wapo wanawake wasio na mafanikio yoyote lakini wanaweza kutishia mamlaka ya wanaume. Wanaweza wasiwe na elimu, fedha wala umaarufu mkubwa katika jamii lakini bado wakawa tishio la kweli kweli kwa wanaume wengi. 

Ingawa kwa haraka tunaweza kufikiri tatizo ni mwanamke, ukichunguza kwa makini unaweza kugundua kuwa tatizo kubwa linaweza kuwa hali ya wanaume kutokujiamini.

Hata katika mazingira ambayo ni kweli wanawake wenye mafanikio wanaonekana kutishia mamlaka ya wanaume, pengine tatizo halisi si mafanikio waliyonayo wanawake hao. Tatizo linaweza kuwa ni namna wanaume wenyewe wanavyochukulia dhana ya mamlaka yao katika familia. Tutalitazama suala hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles