26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Sababu mikoa mitano kuongoza kwa utajiri

ANDREW MSECHU –Dar es Salaam

RIPOTI ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhusu kiwango cha umasikini wa kipato kwa Tanzania bara kwa mwaka 2017/18, imeainisha mikoa inayoongoza kwa utajiri na ile masikini, huku wataalamu wakisema eneo lenye rasilimali nyingi haimaanishi watu wake watakuwa matajiri.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mikoa inayoongoza kwa kiwango kidogo cha umasikini ni Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Dar es Salaam asilimia 92 ya wakazi wake wana kipato zaidi ya dola moja ya Marekani kwa siku, ikifuatiwa na Kilimanjaro (90%), Njombe (87%), Morogoro (80.7%) na Songwe (79.3%).

Mikoa inayoongoza kwa umasikini nchini ni Rukwa ambao watu wenye kipato hicho cha zaidi ya dola moja ya Marekani kwa siku ni asilimia 45, ikifuatiwa na Simiyu (39.2%), Lindi (38%), Geita (37.5%), Mwanza (34.6%), Kigoma (34.5%), Tabora (34.5%) na Singida (34%).

Wataalamu wa uchumi walisema licha ya mikoa iliyoonekana masikini kuwa na rasilimali nyingi, suala la watu kujituma na mgawanyo keki ya taifa  ni muhimu kutazamwa.

Kwa mujibu wa NBS, umasikini na utajiri vimepimwa kwa kuangalia wastani wa viwango vya matumizi ya familia kwa mwezi ambapo kwa Dar es Salaam wastani wa matumizi ya familia moja ni Sh 720,946 wakati Rukwa ni Sh 268,041.

Vipimo hivyo vilichukuliwa pia katika wastani wa bidhaa za chakula kwa mwezi na zisizo za chakula, ambazo hutumiwa na mtu mzima kwa kipindi hicho.

Vingine vilivyotumika ni uwezo wa familia kupata chakula kinachozalishwa na familia yenyewe na matumizi ya bidhaa na huduma nyingine, ikiwemo mavazi, usafiri, mawasiliano, afya na elimu.

“Hii haijumuishi kodi na matumizi mengine yahusuyo makazi, na wala haiangalii matumizi yaliyopo kwenye matukio kama ya harusi, mazishi na wala haiangalii matumizi katika vifaa vya kisasa, ikiwemo magari na televisheni,” inasema ripoti hiyo.

Mstari wa umasikini unaoangaliwa katika suala la chakula unaegemea zaidi uwezo wa hifadhi ya chakula, ikizingatiwa aina ya chakula kilichotumiwa kwa asilimia 10 hadi 50 ya idadi ya watu.

Gharama halisi ya chakula kwa mujibu wa mstari wa umasikini ni Sh 1,109.53 kwa mtu mzima kwa siku sawa na Sh 33,748 kwa mwezi.

Katika mstari wa umasikini, mahitaji muhimu yanaangaliwa kama mahitaji ya ziada yasiyo ya chakula, ikiwemo mavazi, usafiri, elimu na afya ambayo kwa jumla yanapewa wastani wa Sh 49,320 kwa mtu mzima kwa mwezi.

 “Mahitaji ya muhimu katika hali ya umasikini unaangalia mlinganisho wa matumizi ya mahitaji muhimu ya kila kichwa kwa mwezi katika idadi ya watu iliyopo, ikilinganishwa na matumizi ya chakula pekee ambayo hutumika pia kuangalia umasikini kwa kichwa.

 “Kina cha umasikini unaonesha kiwango cha wastani namna familia masikini zilivyo kutoka katika mstari wa umasikini. Kinaangalia matumizi halisi ya wanafamilia katika mstari wa umasikini ikilinganishwa na jamii nzima,” inasema ripoti hiyo.

NBS inaeleza umasikini unaonekana kutokana na idadi ya rasilimali zilizopo, zinazoweza kutumiwa na mtu mzima, ikilinganishwa na namna zinavyoweza kupunguza umasikini, ikikadiriwa kwamba watu wote walio masikini wanashabihiana katika matumizi yao chini ya mstari wa umasikini.

Katika ripoti hiyo, NBS inaeleza kwa mwaka 2017/18 ilibaini kuwa wastani wa matumizi kwa familia kwa mwezi kwa Tanzania Bara ilikuwa ni Sh 416,927, huku maeneo ya mijini matumizi yalikuwa makubwa yanayofikia Sh 534,619 na vijijini yalifikia Sh 361,956.

Ripoti hiyo ilieleza pia umasikini katika matumizi muhimu ulipungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 kwa mwaka 2017/18 na katika chakula ulipungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia 8.0 mwaka 2017/18.

WASEMAVYO WATAALAMU

Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, Profesa Honest Ngowi, alisema mikoa hii inayoonekana kuwa masikini ni ile yenye rasilimali nyingi, madini na mazao.

Profesa Ngowi alisema rasilimali ni jambo jingine na maendeleo ni jambo jingine, ndiyo maana mikoa kama Geita na mingineyo ina rasilimali nyingi, lakini bado watu wake si matajiri.

 “Kuna nchi kama Israel na Ubelgiji ambao hawana rasilimali, lakini unakuta nchi kama Israel ambayo ina jangwa ndiyo inayoongoza kulisha dunia. Sasa hapo kuna mambo mtambuka, namna watu wanavyowezeshwa kukabiliana na mazingira yao.

“Hapa tunaona pia kuna suala la mgawanyo wa keki ya taifa, kuna maeneo yanapata mgawo mkubwa na mengine yanaminywa, lakini si suala ambalo mimi nalishabikia, katika maeneo yote watu wanatakiwa wasisubiri Serikali iwaletee mgawo,” alisema Profesa Ngowi.

Alisema suala la msingi watu wafanye kazi kwa juhudi, watafute mbinu za kujisaidia na wajiendeleze katika maeneo yao.

“Suala la msingi watu waangalie namna watakavyomiliki rasilimali kwenye maeneo yao na kuishinikiza Serikali iandae sera zinazowasaidia,” alisema.

Mtaalamu mwingine wa uchumi, Profesa Haji Semboja, alisema matokeo hayo yanaweza kuwa yanaakisi kile ambacho watafiti walikitarajia, lakini kuna haja ya kuangalia zaidi uhalisia wa utajiri na rasilimali zilizopo katika mikoa.

Profesa Semboja alisema kwa tafsiri sahihi, umasikini ni hali ya kukosa fursa na kushindwa kutumia fursa kwa faida ya ustawi wa watu katika maendeleo yao.

Alisema fursa zinazotakiwa kuangaliwa wakati wa kutafsiri umasikini na utajiri wa watu katika maeneo ni suala la rasilimali zilizopo, uwekezaji, uwezeshaji, biashara, matumizi na uwezo wa watu kuweka akiba, suala ambalo watafiti wengi wamekuwa wakilikwepa.

“Ni kweli, uko umasikini wa kipato, wa hali pia. Utaratibu uliowekwa na mataifa mengi wanaangalia kwa uwiano wa uwezo wa kupata na kutumia dola moja ya Marekani. Huu unaangalia uwezo wa watu kutafuta, kupata na kutumia dola kwa siku.

“Tafsiri hii haiangalii uwezo wa mtu kwa namna anavyojitathmini na kujithamini, hauangalii utajiri wa mashamba na rasilimali nyingine, hauangalii ukoo wenu mko wengi au wachache kiasi gani, hauangalii uhusiano wa ndugu na mengineyo,” alisema Profesa Semboja.

Alisema wapo watu ambao wana utajiri mkubwa wa mashamba na mifugo na wana uwezo mkubwa wanaouona wao unawaridhisha kuliko kushika dola mkononi, kwa kuwa wanaweza kula, kunywa na kulala vizuri.

Profesa Semboja alisema ni vyema pia waangaliwe watu kwa hali zao, kuridhika kwao na namna wanavyochukulia maisha yao kwa kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo hata matumizi yake hayajarasimishwa, lakini wananchi wanaendelea kunufaika nazo bila kujali mikoa wanayotoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,206FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles