24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Sababu JPM kutumia treni kwenda kuzindua Stiegler’s Gorge

Na Bakari Kimwanga-MOROGORO

RAIS Dk. John Magufuli ametumia treni ya Tazara kwenda Kisaki ambako leo anatarajiwa kuzindua ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Stiegler’s Gorge.

Akizungumza baada ya kushuka kwenye treni, alisema ameamua kutumia usafiri huo ili kujua changamoto zinazowakabili wananchi wa Kijiji cha Kisaki na azitafutie suluhisho la haraka.

Alisema hayuko tayari kuona wananchi wa Kisaki ambao wamezungukwa na mradi huo wakiwa hawana barabara na huduma za afya.

Akizungumza na wananchi katika mkutano uliofanyika Stesheni ya Kisaki, alisema amelazimika kumkatisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo, ambaye alikuwa akizungumza masuala ya manispaa wakati kijiji hicho hakina zahanati.

Alisema anashangazwa zahanati kujengwa eneo jingine huku kijiji hicho kikiwa hakina huduma hiyo.

“Kwa sababu leo tupo Kisaki, tukifika mjini tutazungumza ya mjini, leo (jana) tupo Kisaki tunazungumza ya watu wa Kisaki.

 “Ndugu zangu nataka niwahakikishie tangu mliponichagua na mkachagua waheshimiwa wabunge, tukawaletea wakuu wa mikoa wazuri, wakuu wa wilaya, na watendaji wengine wa Serikali, ninataka niwahakikishie tuko pamoja.

“Ninajua wananchi wa Kisaki ni wakulima wazuri, ni wachapakazi wazuri, ninajua pia mnasumbuliwa na wanyama wa porini, sasa nimesikia kilio chenu.

“ Nimeamua kuja na treni kutoka Dar es Salaam mpaka hapa Kisaki kwa makusudi, ninajua mji wa Kisaki unakua kwa haraka, unahitaji mipango mipya.

“Hapa nitatoa Sh milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hapa Kisaki. Ni lazima hospitali ya Kisaki iwe kubwa kwa sababu tuna mradi mkubwa wa pale Stiegler’s, ni kilomita 55 hadi 60 kutoka hapa, ili watu

watakaokuwa wanatoka kule wanakuja hapa,” alisema Rais Magufuli.

Alisema njia ya kubakiza fedha zinazogharimia mradi huo eneo hilo ni kuchapa kazi kwa kuwa na vyakula vya kutosha, matunda na mahindi, matikiti maji, viazi ambavyo vitakuwa vikiuzwa eneo la mradi.

“Mradi utakapoanza muweze kuuza kwa sababu vyakula mlivyonavyo havitoshi, sababu watakaoajiriwa pale ni maelfu ya wafanyakazi, ninajua mnaweza msipate ajira wote, lakini asilimia kubwa mtapata ajira.

“Mtakapofanikiwa kupata ajira pale, ninaomba msiende kuiba vifaa vya ujenzi, mradi huu ni ukombozi kwa eneo hili, mkiutumia vizuri mtakuwa mmejikomboa kiuchumi,” alisema Rais Magufuli.

Mradi huo unaogharimu Sh trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake, ulianza Juni 15 na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 15 na unatarajiwa kukamilika 2022.

Akizungumzia mafanikio ya mradi huo jana, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abassi, alisema ulikuwa ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambayo imekaa miaka 40 bila kutimia.

“Huu ni mradi, ulikuwa ni lazima kutekelezwa, hata kama awamu zote na hii ya sasa, ipo siku ungetekelezwa tu,” alisema Dk. Abassi.

Alisema licha ya faida za mradi huo kwa uchumi wa viwanda, utasaidia kupunguza gharama za umeme kwani uzalishaji wa umeme wa maji ni rahisi kuliko vyanzo vingine vyote.

“Wakati uniti moja ya umeme wa maji ni Sh 36, uniti moja ya umeme wa joto ardhi ni Sh 147, umeme wa mafuta Sh 546, makaa ya mawe Sh 118, upepo Sh 103 na umeme wa jua Sh 103.5,” alisema Dk. Abassi.

Kuhusu madai ya kuwapo kwa athari za mazingira, alisema hakuna mradi wowote duniani usiogusa mazingira na Tanzania ipo vizuri katika utunzaji wake, na hakuna athari itatokea kwa wanyama na mimea.

Alisema mradi huo unajengwa katika sehemu ya Pori la Akiba la Selous ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000.

Msemaji huyo wa Serikali, alisema kuwa eneo litakalotumika kwa mradi huo ikiwamo ujenzi wa bwawa kubwa la kisasa, havitazidi asilimia 4 katika eneo la Selous.

“Wanaopinga mradi huu tuwasamehe tu, lakini tujue kwamba wapingaji walikuwapo tangu enzi za manabii, hata tusingeutekeleza mradi huu, wapo ambao wangehoji kwanini hatujauanza.

“Serikali inaendelea kuhakikisha maandalizi muhimu ya mradi yako sawa na sasa mkandarasi anakwenda na kasi tunayoihitaji,” alisema Dk. Abassi.

Eneo hilo la mradi alikabidhiwa mkandarasi Arab Contractors ambayo inaundwa na kampuni za Osman A. Osman & Co na Elsewedy Electric zote za nchini Misri.

Makamu Rais wa Kampuni ya Arab Contractors, Wael Hamdy, alisema umuhimu wa ujenzi wa mradi huo si kwa Tanzania bali kwa Bara la Afrika kwa ujumla.

Alisema kwa niaba ya Serikali ya Misri watahakikisha  wanatekeleza mradi huo kwa kasi, kwani waliwahi kupingwa hata walipojenga Bwawa la Azuan.

Hamdy alisema mataifa mengi yalipinga ingawa Tanzania kupitia Mwalimu Nyerere waliwaunga mkono Misri na sasa wamekuwa na uhakika wa niashati ya kutosha ya umeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles