Kulwa Mzee-Dar es salaam
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetumia saa tatu kusikiliza mvutano kati ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, wadhamini na mawakili wa Jamhuri wanaotaka dhamana za washtakiwa hao zifutwe.
Imesema wahusika katika kesi hiyo wametumia mwaka mmoja na nusu kubishania suala la dhamana hali inayosikitisha kwani muda unapotea.
Mvutano huo ulianza saa tano asubuhi jana hadi saa nane mchana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba ambapo Jamhuri wanataka washtakiwa wafutiwe dhamana ama hati zao za kusafiria zishikiliwe, huku wenyewe wakipinga kwa madai walienda Afrika Kusini kwenye matibabu baada ya kuomba ruhusa mahakamani.
Mahakama iliwataka wadhamini wa Mdee na Bulaya kujieleza kwanini dhamana zao zisichukuliwe na washtakiwa wajieleze kwanini wasifutiwe dhamana kwa kukiuka masharti ya dhamana kwa kusafiri nje ya nchi bila kibali.
Fares Lobison na Martha Charles ambao ni wadhamini wa Mdee, kwa nyakati tofauti walidai kwamba wajibu wao ni kuhakikisha mshtakiwa anafika mahakamani siku ya kesi na alifika.
Wanadai walifahamishwa kwamba barua iliwasilishwa mahakamani kutoka kwa daktari wa Aga Khan ya ruhusa ya kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.
Nao Joel Mwakalebela na Neshukulwa Tungaraza ambao ni wadhamini wa Bulaya, kwa nyakati tofauti walidai Bulaya aliwapigia simu akiwafahamisha kwamba anamsindikiza Mdee kwenye matibabu na tayari alishatoa taarifa mahakamani.
Walidai bado wana nia ya kumdhamini mshtakiwa huyo, hivyo wanaomba asifutiwe dhamana.
Mdee akijieleza alidai hali yake ya kiafya inafahamika mahakamani na hata kuna wakati Hakimu Simba amekuwa akimwuliza anavyoendelea.
Anadai aliwahi kutoa taarifa za awali kwamba anakwenda kwenye matibabu wakati akiwa katika kesi nyingine namba 228 ya mwaka 2017 baada ya kubaini kwamba safari yake inaweza kuathiri kesi zote mbili.
“Mheshimiwa hakimu, nilitoa taarifa Novemba 25 na Desemba 18 mwaka jana, nilielekezwa kuandika barua ya ruhusa na nilipopata uhakika wa lini naenda kupata matibabu, Januari sita daktari wangu wa Aga Khan aliandika barua kwa Hakimu Mfawidhi.
“Daktari alieleza kwamba natakiwa kupata matibabu ya ziada nje ya nchi, wao kama hospitali ya ndani hawana uwezo huo, aliomba niongozane na Bulaya sababu anafahamika na madaktari ndani na nje ya nchi kutokana na mazingira ya matibabu yangu.
“Mama yangu ni mtu mzima, nilipopata barua tarehe saba nilimpa wakili wangu, nikajiridhisha kwamba mahakama inayo taarifa,” alidai Mdee na kuomba kutoa vielelezo vya tiketi na hati ya kusafiria inayoonyesha kwamba Januari 10 mwaka huu alienda Afrika Kusini kwa kutumia ndege ya Shirika la Kenya na walipofika Kenya walihamia katika ndege nyingine iliyowafikisha safari yao.
Alidai kuwa kwa ushauri wa daktari alitakiwa aendelee kuwepo Afrika Kusini, lakini kutokana na makando kando ya kesi hiyo aliamua kukatisha matibabu aje kuhudhuria.
Bulaya akijitetea alidai taarifa za kusafiri na Mdee ziliifikia mahakama na kwamba iliamuliwa amsindikize kutokana na tatizo alilokuwa nalo, mama yake ni mtu mzima na Mdee amezaliwa mwanamke peke yake.
Mshtakiwa huyo alitoa vielelezo vya tiketi na hati yake ya kusafiria ikionyesha alienda nchini Afrika Kusini.
Akijibu Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai sababu zilizotolewa hazina msingi, walitoka nje ya nchi bila kibali cha mahakama, kabla ya kuondoka walipaswa kujiridhisha kama walipata ridhaa ya mahakama.
Akiongezea hoja, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai Hospitali ya Aga Khan haina mamlaka ya kuandika barua ya kuwaombea ruhusa washtakiwa na washtakiwa walitakiwa kutoa nyaraka za matibabu.
“Kuna hoja kwamba mahakama inafahamu tatizo la Mdee, niseme kwamba nikiwa upande wa Jamhuri sina ufahamu Mdee anasumbuliwa na nini.
“Ni rai yetu kwamba washtakiwa wafutiwe dhamana, kama itaonekana hoja hazijitoshelezi kuwafutia mahakama ishikilie hati zao za kusafiria ili watakapohitaji kusafiri wafuate utaratibu wa kuomba ruhusa na wapewe karipio kali washtakiwa wote,” alidai Nchimbi.
Wakili wa utetezi, John Mallya alidai ombi la kuchukua dhamana za wadhamini limeondolewa sababu halikujadiliwa wakati Jamhuri wakitoa hoja zao.
Alidai kabla ya kufutwa kwa dhamana ama kushikiliwa kwa hati za kusafiria, kinachoanza kufanyika ni kuchukuliwa kwa dhamana za wadhamini, ombi ambalo waliliondoa.
“Tunapinga maombi hayo, kwanza hawakusema wameyaleta chini ya kifungu kipi cha sheria, pili washtakiwa waliomba ruhusa ya kwenda Afrika Kusini kwenye matibabu,” alidai Mallya na kuomba maombi hayo yatupwe kwani hayana msingi wowote.
Hakimu Simba alisema anasikitishwa na kesi hiyo kwani karibu mwaka mmoja na nusu wamekuwa wakibishania masuala ya dhamana.
Aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 31 kutoa uamuzi wa kuwafutia dhamana ama kutowafutia dhamana washtakiwa hao.
Leo kesi inaendelea kwa ajili ya upande wa utetezi kuleta mashahidi.
Katika kesi hiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake nane wakiwamo Mdee na Bulaya, wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi, kukusanyika na kuandamana bila kibali Februari 16 mwaka 2018.