26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

SAA NNE ZA LOWASSA POLISI

Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema ,Edward Lowassa, akishuka kwenye gari lake katika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam jana kuitikia wito wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DCI) kwa mahojiano. PICHA NA JUMANNE JUMA.

NORA DAMIAN Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, jana alihojiwa kwa saa nne  katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI).

Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alihojiwa   Dar es Salaam jana huku akituhumiwa kutoa maneno ya uchochezi.

Inadaiwa kiongozi hiyo alitoa maneno hayo ya uchochezi Jumamosi  Juni 24, mwaka huu, wakati wa futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika mahojiano hayo yalifanyika katika ofisi ya DCI  Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam, Mwanasheria wa Lowassa, Peter Kibatala alisema mteja wake alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi kuhusiana na matamshi aliyoyatoa wakati wa futari hiyo.

“Lowassa alipokea wito kutoka ofisi ya DCI kwamba aripoti leo (jana) saa 4.00 asubuhi.  Mahojiano yalijikita katika kile kinachodaiwa kwamba ni kauli za uchochezi.

“Amechukuliwa maelezo yake ya onyo na amejidhamini mwenyewe, atatakiwa kurudi tena polisi kesho (leo),” alisema Kibatala.

Lowassa aliwasili polisi saa 3:58 asubuhi akiwa ameongoza na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji na wanasheria kadhaa.

Hata hivyo aliingia ndani na Wakili Kibatala huku watu wengine akiwamo Dk. Mashinji wakizuiliwa getini.

Alitoka saa 8:05 mchana na kwenda nyumbani kwake Masaki.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa katika mahojiano hayo, Lowassa aliwekewa mikanda ya video mbalimbali kuhusu matamshi aliyotoa wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 yanayohusu ahadi yake ya kuwatoa kizuini masheikh wa Jumuiya ya Mihadhara (Uamsho).

Baada ya kuwekewa video hizo alitakiwa kueleza kwa kina kauli zake hizo zilikuwa na maana gani kwa usalama wa nchi.

Pamoja na hali hiyo inaelezwa kuwa bado Lowassa alisimamia msimamo wake wa kuona  hakuna sehemu aliyotamka uchochezi.

NYUMBANI

Saa 8:53 mchana, Lowassa alizungumza na waandishi wa habari na kuwataka wanachama wa Chadema wasiwe na hofu kwa sababu  alikuwa anatekeleza sera ya chama chake.

“Nilikwenda polisi na kuhojiwa juu ya hotuba niliyoitoa kwa Waitara wakati wa futari, kuna watu wameitafsiri kwamba ni uchochezi. Polisi wana shaka hivyo wana haki ya kunihoji.

“Niwahakikishie wanachama wenzangu hatujafanya kosa lolote, tulikuwa tunatekeleza sera ya chama chetu, wakae salama wasubiri taratibu zifuatwe,” alisema Lowassa.

Hata hivyo hakuwa tayari kujibu maswali zaidi ya waandishi wa habari kwa kile alichodai kuwa atakuwa anaingilia kesi hiyo.

“Siwezi kutoa ‘details’ za mazungumzo kwa sasa nitakuwa nje ya utaratibu na nitaonekana naingilia kesi, tusubiri wakati mwingine nitaongea zaidi,” alisema.

KATIBU MKUU CHADEMA

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji, alisema ingawa si jambo baya kuitwa na kuhojiwa polisi lakini alishauri mahojiano yawe ya haki.

“Tunaunga mkono hotuba yake kwa sababu sheria za nchi yetu zinazuia kumuweka mtu ndani kwa muda mrefu kama hana kesi.

“Taifa limeridhia mikataba mbalimbali ya haki za binadamu na katiba inatoa uhuru kwa mtu kuishi huru na kutochukuliwa mhalifu mpaka itakapothibitishwa.

“Lakini sasa ni miaka minne watu wako ndani ushahidi haujakamilika,” alisema Dk. Mashinji.

SHEIKH KATIMBA

Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Sheikh Rajabu Katimba, alisema walishtushwa baada ya kusikia Lowassa ameitwa kuhojiwa polisi kwa sababu  alizungumza kwa nia njema.

“Lowassa alizungumza kwa nia njema na wala si uchochezi, ni muda mrefu masheikh wako ndani… kuwa mtuhumiwa aina maana kwamba umetenda kosa.

“Tunamuunga mkono Rais Dk. Magufuli katika mambo mbalimbali anayoyafanya lakini tunandelea kumuomba kama wale masheikh walioko ndani hawana hatia waachiwe,” alisema Sheikh Katimba.

ULINZI MKALI POLISI

Hali ya usalama iliimarishwa kabla na baada ya Lowassa kuwasili Makao Makuu ya Polisi.

Tangu jana asubuhi, polisi waliimarisha ulinzi katika maeneo ya Posta Mpya na Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam.

Katika barabara zote za kuingia Makao Makuu ya Polisi, kulikuwa na askari wa kutuliza ghasia waliokuwa kwenye magari huku wengine wakirandaranda mtaani.

Pia yalikuwapo magari yenye maji ya kuwasha ambayo yaliegeshwa katika Mtaa wa Ohio na eneo la Posta Mpya jirani na Kanisa la Mtakatifu Albano.

Kwa wakati wote huo hakuna mtu aliyeruhusiwa kukatiza katika maeneo jirani na ofisi hizo.

Waandishi wa habari walilazimika kukaa katika kituo cha mafuta cha GBP jirani na Posta Mpya, wengine walikaa jirani na jengo la Golden Jubilee na baadhi walipiga kambi karibu na hoteli ya Serena.

ALICHOSEMA KWENYE FUTARI

Juni 24  mwaka huu, Lowassa alimtaka Rais Dk. John Magufuli kutafakari hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki) maarufu ‘Uamsho’ wanaosota gerezani kwa miaka minne sasa bila kesi kuamuriwa.

Masheikh hao ambao wamefunguliwa kesi ya ugaidi, awali kesi yao ilikuwa ikiendeshwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar lakini  baadaye ilihamishiwa katika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu   Dar es Salaam ambako inaendelea hadi sasa.

Kutokana na kusota huko kwa masheikh hao, Lowassa alisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata Uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Alisema kama masheikh hao wamefanya makosa wapelekwe mahakamani haki itendeke lakini kuendelea kuwashikilia ni fedheha kubwa kwa Taifa.

Waziri Mkuu huyo wa zamani  alisema kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli ametekeleza ahadi ya Vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuunda tume  mbili za kushughulikia mchanga wa dhahabu, hana budi kuwatoa kizuizini masheikh hao wa Uamsho.

“Nilipokuwa nagombea urais, nilizunguka nchi nzima nikiahidi kuunda tume ya kuchunguza madini ya dhahabu, bahati mbaya kura zetu walizihesabu vibaya na kutunyima kura zetu.

“Sasa niliposikia bwana mkubwa kaunda tume nikasema naam… Rais ameanza kutekeleza ahadi yetu ya Ukawa.

“Sasa nimwombe aangalie na hili la masheikh wetu, sisemi kwamba hawana makosa  lakini kuwaweka ndani miaka minne bila kesi kuamuriwa ni fedheha kwetu na kwa Serikali pia.

“Nchi gani hii, ina uhuru wa miaka 50, watu wako tena waumini wa dini, wanawekwa ndani bila kesi kwa sababu ya tofauti ya itikadi.

“Tuwaombee masheikh wetu wale watoke, lakini na niyinyi masheikh mliopo hapa zungumzeni mfanye nini, msiwe baridi sana, pengine kuna lugha watakayoweza kuwasikia,” alisema Lowassa.

Uamsho

Mwaka 2011 viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki), wakiongozwa na Sheikh Farid Hadi Ahmed (41) walikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kusababisha uharibifu wa mali za watu na Serikali na kuhatarisha usalama wa taifa.

Mara kadhaa wamekuwa wakifikishwa mahakama Hakimu Mkazi Kisutu chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto, wakishitakiwa kwa ugaidi.

Mbali na kina Farid, kesi za ugaidi zaidi ya 20 zinaendelea mahakamani zikiwahusisha  washtakiwa zaidi ya 60.

Viongozi hao walioshtakiwa ni Masheikh Farid Hadi Ahmed (41), Msellem Ali Msellem (52), Mussa Juma Issa (37), Azzan Khalid Hamdan (48) na Suleiman Juma Suleiman (66).

Wengine ni Khamis Ali Suleiman (59), Hassan Bakar Suleiman (39), Gharib Ahmad Omar (39), Abdallah Said Ali (48) na Fikirini Majaliwa Fikirini (48), wote kutoka Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles