Saa nne ngumu za kumfanyia upasuaji wa moyo mtoto mchanga

0
1319

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

AGOSTI, mwaka huu Marietha John (si jina lake halisi), alijaaliwa kujifungua mtoto wa kiume katika Hospitali ya Seriani iliyopo mkoani Arusha.

Huyo ni mtoto wake wa pili ambaye alijifungua kwa njia ya upasuaji.

Anasema furaha ya kupata mtoto iliingiwa dosari hasa alipokuwa akimtazama usoni mwanawe kwani alionesha hali isiyo ya kawaida.

“Kila nilipomtazama usoni, niliona rangi ya bluu katika midomo yake, sikuelewa alikuwa na tatizo gani, alikuwa akilia kwa muda mrefu na mapigo yake ya moyo yalikuwa yanakwenda kasi,” anasimulia.

Anasema akiwa bado yupo hospitalini, madaktari wakiendelea kufuatilia hali yake na mwanawe, wiki mbili tangu alipojifungua madaktari walibaini jambo.

“Alikuja daktari mmoja kuniangalia, akamchukua na mwanangu kumuangalia, kisha akaondoka naye kwenda kwenye chumba cha madaktari wa watoto.

“Huko walikwenda kumchunguza na aliporudi alinieleza kile walichokibaini kwamba mwanangu anakabiliwa na tatizo la moyo,” anasimulia.

Anasema daktari huyo alimshauri ni vema kuwahi mapema Dar es Salaam kwa matibabu zaidi ya kibingwa.

“Walinipa rufaa ilibidi tusafiri kwa kutumia ndege kuja Dar es Salaam, tukaja moja kwa moja hapa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) nakuanza uchunguzi,” anasema.

Anasema baada ya uchunguzi uliofanywa na jopo la madaktari wa JKCI walithibitisha kweli alizaliwa na tatizo la moyo.

“Wakanieleza matibabu yake ni upasuaji basi nikawa naomba Mungu ufanyike kwa wepesi ili mwanangu apone, jambo ambalo limefanikiwa,” anasema huku akitabasamu.

Daktari

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto JKCI, Naiz Majani, anasema imekuwa bahati kubwa kwa mtoto huyo kuwa hai hadi sasa.

“Tumemfanyia upasuaji akiwa na umri wa wiki tano, alizaliwa na tatizo la kuziba kwa mshipa mkubwa unaopeleka damu kwenye mapafu kitaalamu unaitwa (Pulmonary Atresia Intact Septum),” anasema.

Anasema kuziba kwa mshipa huo wa damu kulizuia damu kwenda kwenye mapafu na kupunguza kabisa uwezo wa damu yake kusafishwa.

Anasema takwimu zinaonesha nusu ya watoto wanaozaliwa na tatizo hilo duniani hufariki dunia wakiwa na umri wa wiki mbili.

“Wanapovuka umri huo bado zaidi ya asilimia 90  hupoteza maisha wanapofikia umri wa miezi sita, ndiyo maana tunasema imekuwa bahati kubwa kwa mtoto huyu kuishi,” anasema na kuongeza:

“Hapa nchini, kwa sasa hakuna mtaalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto ambaye amewahi kufanikiwa kuokoa maisha ya mtoto aliyezaliwa na tatizo hilo.

“Ni mara ya kwanza na ni historia ya pekee ambayo JKCI tumeiandika, kuweza kufanya upasuaji huu tukishirikiana na madaktari bingwa wenzetu kutoka Shirika la Kimataifa la Mending Kids la nchini Marekani na Italia,” anasema.

Dk. Naiz anasema tatizo hilo ni miongoni mwa matatizo makubwa ya magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo.

“Takwimu zinaonesha asilimia tatu ya watoto wote wanaozaliwa duniani huzaliwa wakiwa na tatizo hili,” anasema.

 

Kwanini hufa mapema

Kibaiolojia ili binadamu aweze kuishi huhitaji kuvuta hewa ya oksjeni ndani ya mwili wake na kutoa nje hewa ya kabondaioksaidi.

Kitendo hicho hufanyika kupitia mfumo wa upumuaji ambao huhusisha viungo kadhaa vya mwili hasa pua, koo na mapafu.

Mtandao wa WikiPedia unaeleza mapafu ni ogani kuu ya mfumo wa upumuaji wa mwili, ni sehemu inayoingiza hewa ya oksjeni mwilini.

Hewa hiyo husafiri kwenda kwenye seli za mwili kupitia damu, binadamu ana mapafu mawili, moja upande wa kulia na jingine kushoto.

Kupitia ogani hiyo binadamu huvuta hewa ndani ambayo husafishwa na kusafirishwa kwenda katika seli za mwili kupitia damu.

Ndani ya mapafu kuna viputo vidogo, damu huzunguka ndani ya viputo kupitia mishipa midogo ya damu iliyotenganishwa na nafasi kwa ngozi nyembamba mno.

Mtandao huo unaeleza hewa ya oksijeni huweza pia kupita kwenye ngozi hiyo na kuingia katika damu inapopokewa na seli za damu nyekundu.

Dk. Naiz anasema kwa kuwa mshipa unaohusika unakuwa umeziba hivyo damu hushindwa kufika kwenye mapafu kwa ajili ya kusafishwa kabla ya kusafirishwa kwenye mwili.

“Ndiyo maana mtoto hufariki mapema, kwa sababu anazaliwa mshipa mkubwa unaopeleka damu kwenye mapafu ukiwa umeziba, inakuwa haina uwezo wa kufika huko kupokea hewa safi.

“Hivyo, kwenye mshipa wa mtoto huyo kulikuwa kumebakia kimrija kidogo kinachopaswa kusafirisha damu kwenda kwenye mapafu yake kupokea hewa ya oksijeni.

“Japo takwimu zinaonesha ni tatizo linalojitokeza mara chache ila linapotokea huwa lina madhara makubwa kwa sababu hupunguza uwezekano wa mtoto kuishi.

“Matatizo ya moyo ya kuzaliwa kwa watoto yapo mengi lakini kuna ambayo hata akiishi miaka minne au mitano huweza kutibiwa na kupona ila kwa tatizo hili la kuziba kwa mshipa huo wa damu anapaswa kutibiwa mapema vinginevyo anapoteza maisha,” anasema.

Anasema hata wale ambao hufanyiwa upasuaji huhitaji kufuatiliwa kwa ukaribu maendeleo ya hali zao.

“Ufuatiliaji umegawanywa kwa vipindi maalumu, kwa kuanzia ndani ya saa 24 tangu alipofanyiwa, tunaangalia hali yake, kwani ndani ya saa hizo huweza kupoteza maisha.

“Kwa sababu damu yake ilikuwa haifiki kwenye mapafu, hivyo kwa kuzibua mshipa huo inakuwa kama vile mmeingiza kitu kigeni kwenye mapafu yake.

“Kuna mambo hujitokeza, kwa mfano kuhema kwa haraka kuliko watoto wengi hivyo, lazima afuatiliwe, mtoto tuliyemfanyia upasuaji alivuka salama kipindi hicho, imetupa faraja mno,” anasema.

Anasema wataendelea kufuatiliwa kwa ukaribu hadi atakapofikisha umri wa miaka 15.

“Wenzetu wametueleza katika nchi zao asilimia 80 watoto waliofanyiwa upasuaji wa aina hii maendeleo yao ni mazuri,” anabainisha.

 

Ulivyofanyika

Dk. Naiz anasema haikuwa kazi rahisi kufanikisha upasuaji huo ambao ulichukua zaidi ya saa nne kukamilika.

“Kwanza ilibidi tujadiliane njia gani tutumie kufungua mshipa huo, kati ya upasuaji au tiba mionzi,” anasema.

Anasema ilionekana kwa njia ya upasuaji pekee ilikuwa ngumu kidogo kwani mtoto huyo umri wake ulikuwa mdogo na mishipa yake ya damu ilikuwa midogo.

“Kumtibu kwa mionzi pekee napo bado ilikuwa ni changamoto, mishipa ilikuwa midogo na alikuwa na kilogramu 3.9 tu,” anabainisha.

Dk. Naiz anasema kwa kawaida tiba ya mionzi huhitajika mtoto kuwa na angalau kuanzia kilogramu sita.

“Tulikaa na kujadili hatimaye tukaamua tutumie njia zote mbili kumtibu, tukafanikiwa sasa damu ya mtoto ina uwezo wa kuzunguka vizuri kwenda kusafishwa kwenye mapafu yake, tunajisikia fahari,” anasema.

 

Visababishi

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto JKCI, Theofil Ludovick, anasema upasuaji huo ulifanyika Septemba 26, mwaka huu kwa kutumia mtambo maalumu wa ‘Cathlab.’

“Magonjwa mengi ya moyo wanayozaliwa nayo watoto chanzo chake hakijulikani, hata hivyo vipo viashiria ambavyo hutajwa kuwa huenda vimesababisha hali hiyo kutokea.

Anataja visababishi hivyo kuwa ni pamoja na ulaji usiofaa kabla na wakati wa ujauzito, unywaji pombe, uvutaji sigara na mjamzito kutozingatia chanjo au dawa maalumu zinazosaidia kumkomaza mtoto akiwa tumboni.

Anasema Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kati ya watoto 100 mmoja huzaliwa na ugonjwa wa moyo.

“Kwa Tanzania, changamoto tunayoona ni uchelewaji wa kugundulika kwa watoto hawa, ama kutokana na umbali wa makazi wanakozaliwa hasa vijijini, wachache hupata huduma kama huyu, wengi hupoteza maisha,” anasema.

 

Dalili

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo JKCI, Samwel Rweyemamu anasema ni mara chache mtoto huonesha dalili.

“Kasi ya upumuaji ipo juu kuliko kawaida, tunaweza kubaini kwa kutumia kifaa maalumu kuyasikiliza, huwa wanashindwa kunyonya vema, hunyonya na kuacha au kuhema pindi wanaponyonya,” anasema.

Anasema hali hiyo hutokea kwa sababu huwa wanatumia nguvu kubwa kunyonya.

“Anapotumia nguvu kwa sababu huhitaji oksijeni ili aweze kuendelea kunyonya, lakini kwa kuwa damu yake safi na chafu inachanganyika hubadilika rangi kuwa ya bluu, hali hiyo itaonekana wazi kwa wepesi kwenye midomo yake, ulimi na mikononi,” anabainisha.

 

Wizara

Septemba 29, kila mwaka Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Moyo Duniani ambayo hupewa kauli mbiu tofauti tofauti, ambapo mwaka huu ilikuwa ni ‘Moyo wako, Moyo wangu.’

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, anasema magonjwa ya moyo yapo kundi la magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Haya yanaweza kuyaepuka kwa jamii kupewa elimu sahihi, hasa kuzingatia mtindo bora wa maisha, kuepuka unywaji pombe, ulaji unaofaa na kufanya mazoezi.

“Changamoto iliyopo ni kwamba watu hawajui kula, wanakula bora chakula na si chakula bora, lazima tuwaelimishe.

“Tumetoa maagizo kwa vituo vya afya, zahanati na hospitali za serikali kuhakikisha wanatumia televisheni zilizofungwa katika vituo vyao kutoa elimu ya afya kwa jamii,” anasema.

Anasema tayari kitengo cha elimu ya afya kwa jamii kimeandaa nakala za ‘Cd na flash’ zenye jumbe za elimu ya afya.

“Tupo pia katika mazungumzo na SUMATRA (Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini) tunataka elimu hiyo itolewe pia ndani ya mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani,” anasema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here