23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Saa 24 za mwisho za Mkapa kijijini Lupaso

Na ANDREW MSECHU

RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa amepumzika, amekwenda zake. 

Tanzania imempumzisha ikijivunia umahiri wa kiongozi huyo aliyezaliwa Kijiji cha Lupaso, wilayani Masasi katika Mkoa wa Mtwara, Novemba 12, 1938.

Safari ya mwisho ya Mkapa ambaye ameishi miaka 82 ya heri, imehitimishwa kwa mwili wake kupumzishwa kwenye makaburi ya familia katika kijiji  hicho alichozaliwa Jumatano Julai 29, 2020, akilala kando ya kaburi la baba yake, William Matwani.

Safari ya mwisho ya Mkapa baada ya kuwasili katika kijiji alichozaliwa haikuwa nyepesi, mapokezi ya mwili wake yalidhihirisha mapenzi ya wananchi wa nyumbani kwake kwa kiongozi huyo wa kitaifa kwa miaka 10, ambaye alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano tangu mwaka 1995 hadi alipohitimisha ngwe yake kwa mujibu wa sheria mwaka 2005.

Mkapa ambaye alifariki dunia usiku wa Alhamisi Julai 23, 2020 anahitimisha safari yake akithibitisha kuwa umma ulikuwa nyuma yake, hatua inayoambatana na mtiririko wa matukio yaliyojitokeza na kubadilisha mandhari ya mji wa Masasi tangu mwili wake ulipowasili na hatimaye kupumzishwa Julai 29.

Kwa waliobahatika kufika katika mji wa Masasi na hatimaye kijijini Lupaso, ni mashuhuda wazuri wa namna shughuli hiyo ilivyobadilisha harakati za wakazi wa mji huo, baada ya nyumba za wageni kufurika wageni kutoka maeneo yote ya nchi na nje ya nchi, hivyo kuwalazimu wageni wengine kulala kwenye magari yao.

Lakini kilichovutia zaidi ni msururu wa wakazi wa mji wa Masasi waliotembea zaidi ya kilometa 15 kuelekea Kijiji cha Lupaso wakitokea katika vijiji vya jirani na mjini Masasi kwenda kushiriki shughuli ya mazishi ya kiongozi huyo.

Msururu wa magari ya viongozi ulitawala barabara ya kwenda Lupaso, usiku kucha ulishuhudia magari hayo kwa mamia yakiingia mjini Masasi na mengine kwenda moja wka moja kijijini Lupaso.

Kwa hakika, tangu kuwasili kwa mwili wa Mkapa kijijini kwake saa 10 jioni, Jumanne Julai 28, 2020 hadi mwili wake ulipozikwa Jumatano Julai 29 na shughui kuhitimishwa saa 10 jioni, shughuli ni kama zilisimama.

USAFIRISHAJI

Kutokana na jiografia ya Kijiji cha Lupaso, ambapo hakuna magari yanayokwenda moja kwa moja, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kutumia magari yake lilikuwa kazini, kuwasaidia wananchi kutoka maeneo yote ya mji waliokuwa tayari kufika kwenye maziko hayo.

Magari hayo yalitawanywa katika kila kona ya mji na vijiji jirani, yakiwabeba wananchi kwa maelfu ambao walihitaji kushiriki maziko ya mpendwa wao.

Wengi wakivutiwa kushiriki kushuhudia namna maziko ya viongozi wa kitaifa yanavyofanyika, lakini zaidi kuona safari ya mwisho ya Mkapa.

Mmoja wa wombolezaji mfanyabiashara mdogo wa Masasi mjini, Abubakar Hussein anasema amefika kijijini hapo na kushiriki maziko baada ya kupata uhakika wa usafiri huo uliowawezesha kufika kwa urahisi.

Anasema kwa kawaida, safari ya kufika Lupaso kwa bodaboda hugharimu hadi Sh 15,000 au Sh 20,000 kwa bajaji ambapo watu hulazimika kujikusanya na kufikia wanne hivyo kuchangia gharama hizo.

“Kwa kawaida huku hakuna mabasi yanayokuja, usafiri wa bodaboda au bajaji ndio unaotumika. 

La sivyo unatemba kwa miguu umbali ambao ni mrefu kwa karibu saa mbili ili ufike, bado safari ya kurudi. Kwa hivyo kama si kupata huu usafiri wa JWTZ wengi tusingeweza kufika, ila tumefika na tumeshiriki maziko,” anasema. 

ULIPUAJI WA MIZINGA

Miongoni mwa mambo yaliyowavutia wengi ni ufyatuaji wa mizinga 21, ambayo ilikuwa ikifyatuliwa umbali wa karibu mita 30 kutoka walipokuwa wamekusanyika waombolezaji. 

Milipuko ya mizinga hiyo ambayo ilikuwa ikitoa milio mikali ya baruti iliibua ukimya miongoni mwa maelfu ya waombolezaji, ambao baadhi yao walishindwa kuihimili na kupatwa na mshtuko. 

Hata hivyo, tahadhari iliyotolewa awali kuhusu mizinga hiyo ilisaidia kuwaondoa watu wenye maradhi ya mshtuko wa moyo, lakini wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu walijikuta wakiwa na kazi ya ziada.

VIONGOZI WALIOHUDHURIA

Mazishi ya Mkapa yaliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli, ambaye alingozana na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Mawaziri wa Serikali  ya Awamu ya Tano.

Mazishi  hayo yaliyoanza saa 1 asubuhi  pia yalihudhuriwa na marais wawili wastaafu waliosalia, ambao ni Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu ya Tatu, Jakaya Kikwete. 

Mawaziri Wakuu wastaafu akiwemo Frederick Sumaye, Joseph Warioba, John Malecela na waliowahi kuwa viongozi wakati wa utawala wa Mkapa pia walihudhuria maziko hayo.

Walikuwepo pia Makamu Mwemyekiti wa CCM (bara) Philip Mangula na Katibu Mkuu Dk Bashiru Ally, mabalozi na wawakilishi wa serikali za nchi mbalimbali duniani.

KIPENZI CHA WATU

Katika ibada ya mwisho iliyofanyika nyumbani kwake katika Kijiji cha Lupaso, Askofu Gerasi Nyaisomba wa Kanisa Katoliki Jimbo la Ndanda anasema kusanyiko lililokutana katika kijiji hicho kwa ajili ya kumuaga na kushuhudia Mkapa akihifadhiwa kwenye nyumba ya milele si la bahati mbaya, bali linatokana na mapenzi yake kwa watu ambao wanarejesha kile walichokipata kwake.

Anamwelezea Mkapa kama mtu mwenye karama ya pekee, aliyejinyenyekeza kwa Mungu hadi hatua ya mwisho na kuishi maisha ya upendo kwa wengine, akiwaheshimu, kuwatumikia, kuwapigania na kuwajali.

Anasema akiwa katika mafunzo yake katika nchi mbalimbali alizopitia, Mkapa anadhihirisha kuwa alijifunza na kuishi kile anachokiamini katika mazingira yake yote, akitetea usawa wa watu na kupinga ubaguzi kwa namna zote.

Askofu Nyaisomba anasema katika utawala wake, Mkapa alihakikisha anatawala kwa haki na pale alipokosea alitambua makosa yake na kukiri, suala lililomfanya awe karibu na wananchi na watu wa kada zote.

“Kila alipoishi alijifunza kuishi kulingana na mazingira. Lakini alijali na kuheshimu toba.  

“Alifanya toba muhimu kwa kuandika kitabu chake, My Life My Purpose, hiyo ni toba ya uungwana usikivu,” anasema.

Askofu Nyasomba anasema Kanisa halitarajii kuona mtu yeyote anafika akiwa na hatimiliki ya kuwaongezea wafiwa machungu kwa njia yoyote ikiwemo kupitia mitandao ya kijamii.

Anatoa pole kwa familia ya marehemu Mkapa, kwa Rais John Magufuli, makamu wa Rais, Samia Suluhu, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais Z’bar Balozi Ali Idd, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Shein,  serikali zote mbili na Watanzania wote.

Askofu huyo aliomba kila mmoja katika tukio hilo amuone mwenzake amefanya vizuri kuliko yeye kwa kuwa ndiyo iliyokuwa hulka ya ndani ya Mkapa.

Anasema hulka yake ndiyo iliyomfanya avae uhalisia wa watu wengine na kuweka kando ubinafsi wake na mamlaka yake, akijilinganisha na watu wa kawaida ambao ndio aliokuwa akiwatumikia, huku akwaamini katika uwezo na kuwapa nafasi wale aliowateua kumsaidia ili watekeleze majukumu yao kwa uhuru lakini kwa ufanisi .

“Kwa Mkapa, katika watu aliowapatia shughuli aliamini kwamba watafanya vizuri kuliko yeye. Kwa hiyo hilo ni jambo alilojivunia, kuwapa watu majukumu huku akiamini kuwa watafanya vizuri zaidi ya namna ambavyo angefanya yeye. Hili ni suala la kulienzi,” anasema.

Anasema kifo chake kiwe ndiyo mwanzo wa kuiunganisha familia ambayo sasa ataendelea kuiombea ili iwe imara zaidi ya ilivyokuwa awali.

KIKWETE: ALIWAPENDA WATU WAKE

Akiwa katika maziko ya Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Jakaya kikwete anasema ni ngumu kupata maneno mazuri ya kumuelezea Mkapa ambaye alimfahamu kwa miaka mingi akiwa mwanafunzi na yeye Mkapa akiwa Mhariri wa magazeti ya Serikali.

Anasema alifahamiana naye kwa karibu alipofanya kazi Masasi, yeye akiwa Katibu wa CCM wilaya na Mkapa akiwa Mbunge wa Jimbo la Masasi na Waziri, lakini alichogundua ni kwamba Mkapa aliwapenda sana watu wake.

Anasema alipomfahamu, kulikuwa na mambo mawili, kwanza alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na hivyo muda mwingi alikuwa angani hivyo taabu aliyokuwa akiipata ilikuwa kuliendesha Jimbo na kukutana na wananchi  na kwamba kila alipopata nafasi alikwenda jimboni.

“Alijitahidi na alikuwa karibu sana na wananchi wake na muda wote alisikiliza matatizo yao na wakati wote aliwapa mrejesho,” anasema.

Anasema kutokana na kuwa karibu na Mkapa kipindi hicho alimpa maarifa ambayo alibaki nayo kichwani na wakati wote anaona alifaulu.

“Jambo la pili, Mkapa alikuwa kiongozi thabiti mwenye utambuzi wa mahitaji kwa watu wake. Wakati ule kulikuwa na matatizo ya ukame na mimi na Jaka Mwambi tulibuni kilimo cha muhogo. Wamakua hawakupenda sana muhogo lakini walikuwa hawana namna.

“Kwa hatua hiyo barua bubu zilikwenda kwake huku wakijaribu  kutulaumu lakini Mkapa alikuwa thabiti na alikuwa na sisi. Alikuwa kiongozi thabiti ambaye hakujali kusifiwa akitambua kuwa unaweza kusifiwa ili uharibu,” anasema Kikwete.

Anasema pamoja na kwamba kuna wakati walijikuta wakigongana na kuwa washindani kwenye kuwania urais mwaka 1995 lakini Mkapa hakuwa na kinyongo na alikuwa na moyo thabiti hata kumteua kuwa Waziri wake wa Mambo ya Nje na hata baadaye alipompokea urais mwaka 2005 alimsaidia  na kama kuna jambo hakusubiri amfuate.

“Alikuwa ni nguzo ya kuegemea, kiongozi aliyependa sana Watanzania. Alichukia watu kuwa maskini hivyo alilipa kiapumbele suala la uchumi. Yeye ndiye aliyetengeneza Dira ya 2025 kuwa Tanzania iwe nchi ya uchumi wa kati wa pato la wastani wa Dola 3,000 kwa kila Mtanzania.

“Sasa hivi tuko katika Dola 1,080 sasa tuna safari kwenda kufikia Dola 3000. Alitengeneza mipango wa kwanza ikiwa ni kuibua fursa za uchumi, wa pili Tanzania ya viwanda ambao Magufuli kaukamata na sasa uko kwenye mikono salama,” anasema.

Mwinyi: NI RAFIKI WA KWELI

Kwa upande wake, Rais wa Awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi anasema amepoteza rafiki wa kweli, mcheshi na mpenda kazi, baba wa familia na ndugu.

Anasema katika hali ya namna hii, binadamu humuishia ya kusema na kurejea maneno ya Mtume Muhamad akisema kuwa binadamu kwa maumbile yake ni mkosaji, hivyo Mkapa kama mwanadamu inawezekana kuna mambo aliyokosea au kuna watu aliowahi kuwakosea katika umri wake.

Anasema katika hali kama hiyo huenda amekosea kwa namna yoyote, kwa hiyo kama amekosa Mwenyezi Mungu amuwie radhi.

“Nasimama hapa kutoa rambirambi kwa mama Mkapa, watoto wake na kwa watu wote wa mkoa huu kwa kuondokewa na ndugu. Mkapa alikuwa mtu mzuri sana, mwema sana, mbahili sana lakini mtenda kazi mzuri sana asiyekuwa na mzaha.

“Kila kiongozi kafanya kazi yake kuwaondolea watu wake matatizo kwa kadri ya uwezo wake na mimi ningependa nimuongezee dua mdogo wetu. “Leo wakati wakimuaga nimeona jambo dogo lakini limeniathiri sana, nimeona watu wote wamevaa viatu.

“Katika udogo wangu nimevaa viatu mara mbili, mara ya kwanza nilipokwenda jandoni, mara ya pili nilipokuwa na miaka 13  baada ya kuuza karafuu nikanunua viatu na nikahakikisha visiishe, nikavifunga na kuviweka begani, hiyo ndiyo kazi ya kiongozi kuinua matatizo ya watu na kuyabeba, ambayo pia ilikuwa tabia ya Mkapa,” anasema.

DK SHEIN: TUNAMUENZI KW AKULINDA MUUNGANO

Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anasema kusanyiko lililohudhuria maziko ya Mkapa lilikuwa na dhumuni kuu la kumsindikiza marehemu katika safari yake ya mwisho na wananchi wa Zanzibar wanaungana na Watanzania wote, wananchi wa Mtwara hususan Masasi katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza kifo cha mtu muhimu aliyeacha alama katika Taifa.

“Takribani siku sita zilizopita Taifa liliingia katika machozi, ila ni vyema kwenda mbele za Mungu na kumuombea amsitiri mahali pema,” anasema.

Dk. Shein anasema Mkapa aliyahifadhi na kuyatunza Mapinduzi ya Zanzibar, aliuhifadhi na kuulinda Muungano kwa vitendo hivyo ni sahihi kumuunga mkono kwa vitendo 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles