KIGALI, RWANDA
NCHINI Rwanda kina mama walioambukizwa virusi vya Ukimwi wanaweza kujifungua na kunyonyesha watoto wao bila kuwaambukiza.
Hii ni baada ya Serikali ya nchi hiyo kuzindua kampeni ya kusaidia akinamama walio na virusi vya HIV kuwanyonyesha watoto wao bila kuwaambukiza Ukimwi.
Kampeni hiyo inafanyika katika hospitali na vituo vya afya kote nchini humo.
Mwandishi wa BBC, Yves Bucana aliyetembelea kituo cha afya cha Remera mjini Kigali, anasema misururu mirefu ya kina mama wanaoishi na virusi vya Ukimwi haiishi, baadhi wanaonekana wajawazito, wengine wanabeba watoto wao.
“Wanafika kupata ushauri nasaha kuhusu namna ya kujilinda kuambukiza watoto wao ilhali kina mama waliokwishajifungua wakifika kumwona daktari ili wafanyiwe ukaguzi wa jinsi wanavyofuata utaratibu wa kuwalinda kuambukiza watoto zao,” alisema.
Katika mpango ulioanzishwa na Serikali wa kusaidia akinamama wajawazito na wanaonyonyesha kuweza kuwahudumia watoto wao na kuwalinda na maambukizi ya HIV.
”Tunawasaidia kina mama kuwa na afya njema pamoja na watoto wao. Tunapima kinga yake ya mwili kuona kwamba haijapungua pamoja na kiwango cha virusi alivyonavyo.
“Tunamfanyia vipimo kadri mtoto anavyokua. Hii haiwezi kumzuia mtoto kunyonya, hakika asilimia 99 ya watoto hawapati maambukizo yoyote,” alisema muhudumu mmoja wa kituo hicho.
Mama wenye virusi vya HIV wanashauriwa kufuata masharti na ushauri wa daktari ili kuepuka kuwaambukiza watoto wao kupitia maziwa ya mama.
Mama mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake katika taarifa hii ameiambia BBC kuwa vipimo alivyofanyiwa kabla ya kujifungua vilibainisha kwamba ana virusi vya ukimwi lakini alifuatiliwa kwa karibu na daktari hadi alipojifungua.
”Sasa mtoto wangu ametimiza umri wa miezi tisa na hana maambukizi yoyote, na jambo muhimu lilikuwa ni kumwokoa mwanangu na ili kutimiza hilo ni lazima ufuate masharti na ushauri wa daktari,” alisema.
”Masharti ni magumu lakini lazima kuyafuata yaani saa ya kumeza dawa kwako wewe na pia kwa mtoto wako, usizidishe hata dakika moja. Lazima kutembea na dawa ikiwa unahisi saa ya kutumia dawa itafika ukiwa haupo nyumbani, ujue una hatari sana ya kujifungua mtoto na ushindwe.
“Kumnyonyesha mtoto ni raha kitu muhimu kwasababu mzazi anahisi upendo wa mtoto wake na vile vile mtoto anahisi upendo wa mamake wakati wa kumnyonyesha,” alisema.
Uwonkunda Fatuma ni muuguzi anayefuatilia kila siku kina mana wenye kuwa na virusi vya Ukimwi katika mpango huu anasema japo masharti ni magumu lakini si kwamba hayawezekani.
”Hatari ya mama kuambukiza mtoto wake ni kubwa sana, mtoto akiwa na maradhi ya vidonda vya mdomoni ni rahisi sana kuambukizwa Ukimwi wakati ananyonya… tunamshauri mama kuchunguza kila wakati mdomoni mwa mtoto na kusitisha kumnyonyesha kwa muda ikiwa mtoto ana ugonjwa huo ili kwanza mtoto atibiwe.
“Kwa muda wa miezi 24 tunamfanyia vipimo vya mwisho, tukikuta mtoto hana tatizo inamaanisha kwamba mama yake alifuata masharti vizuri na tukamruhusu kuendelea kutumia dawa kwengineko hata nyumbani,” alisema Fatuma.
Wataalamu wa afya wanasema ni muhimu wa kujifungua mtoto katika kituo cha afya cha ngazi ya juu ni kuwepo kwa dawa za kuzuia maambukizi ya virusi na pia mbinu salama za kuzaa zinatolewa, ili kuzuia maambukizi ya ukimwi kutoka kwa mama hadi kwa mtoto.
Hakuna takwimu rasmi za akinamama wanaojifungua wakiwa na virusi vya Ukimwi nchini Rwanda kutokana na kwamba kuna wachache wanaojifungua bila kufika hospitali.
Hata hivyo kulingana na idara ya afya ya Rwanda, takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto 100,000 wanaozaliwa ni 150 tu wanaokutwa na virusi vya Ukimwi.
Katika nchi nyingine ya Afrika Mashariki, Kenya takwimu za mwaka 2018 zinaonyesha kupungua kwa maambukizi ya mama kwa mtoto ya virusi vya Ukimwi kutoka asilimia 14 hadi 11 miongoni mwa wajawazito wanaoishi na virusi hivyo, kulingana na ripoti juu ya maendeleo katika kukabiliana na ukimwi, iliyoandaliwa na Wizara ya Afya.
Nchini Tanzania pia kumekuwa na kampeni kadhaa za afya ya mama na mtoto na kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi.