Na Clara Matimo, Mwanza
Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa pikipiki 13 zenye thamani ya Sh milioni 42.185,000 kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa) kupitia Vyombo vya Watoa Huduma Ngazi ya Jamii (CBWSOs) lengo likiwa ni kuwawezesha kusimamia skimu za maji na kuhakikisha zinatoa huduma endelevu kwa wananchi.
Akizungumza jijini hapa leo Juni 29, mwaka huu wakati wa hafla ya kukabidhiwa pikipiki hizo na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, Kaimu Meneja wa Ruwasa mkoani hapa, Mhandisi Daudi Amlima, amesema pikipiki hizo zote ziko ngazi ya wilaya kwa ajili ya kuhakikisha usimamizi wa mairadi ya maji na utoaji wa huduma hiyo kwenye skimu unaimarishwa.
“Kwa kupokea pikipiki hizi 13 ambazo zitakuwa ni msaada mkubwa katika kusimamia utoaji wa huduma bora ya maji kwa wananchi waishio vijijini zinafanya Ruwasa Mkoa wa Mwanza Kuwa na pikipiki 22 zinazotembea kwani awali tulikuwa nazo 17 kati ya hizo tisa tu ndiyo zilikuwa zinatembea nane ziko katika matengenezo makubwa na madogo,”amesema Mhandisi Amlima.
Ameeleza kwamba kwa sasa mkoa wa Mwanza unatoa huduma ya maji safi na salama kwa asilimi 68 tu ya wakazi waishio maeneo ya vijijini lengo nimkufikia asilimia 88 ifikapo mwaka 2025 ambayo ni zaidi ya matakwa ya ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
“Serikali imekuwa na jukumu kubwa la kujenga miradi ya maji vijijini kupitia Ruwasa lengo ni kuwafikishia huduma ya maji wananchi wake katika mwaka wa fedha 2021/2022 Ruwasa Mkoa wa Mwanza imesaini mikataba 51 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 83.8 itakayohudumia zaidi ya watu 560,000 sawa na asilimia 20 ya wananchi wanaoishi vijijini,”amesema.
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza, Marwa Kisibo na Maiga Busagi, CBWSOs, wamesema pikipiki hizo zitawasaidia kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili katika kutoa huduma kwa wananchi kwani baadhi ya maeneo ya vijijini hayana usafiri wa magari na mengine hayafikiki kwa urahisi hata kwa gari.
Kwa upande wake Mhandisi Gabriel, aliwataka wasimamizi wa vyombo hivyo vya usafiri wahakikishe vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuongeza ufanisi katika kutoa huduma ya maji kwa wananchi na wale watakaozitumia kinyume watachukuliwa hatua za kisheria.
Pia amewataka kuzitunza ili zitumike kwa muda mrefu katika kusimamia miradi na skimu za maji, wahakikishe maduhuli ya maji yanakusanywa kwa kuzingatia bei elekezi zilizotangazwa na serikali bila kuwabambikizia wananchi gharama, matengenezo ya skimu za maji yanafanyika kwa uharaka kuwafikia wateja kwa wakati, kutatua changamoto zao kadri zinavyojitokeza.
Amemuagiza meneja wa Ruwasa kusimamia matengezezo ya pikipiki nane kwa haraka ili ziweze kuongeza wigo wa kutoa huduma kwa wananchi vijijini huku akiwataka watendaji katika ngazi zote na wananchi kuendelea kupanga, kusanifu , kusimamia ujenzi wa miradi, uendeshaji wa skimu za maji na kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji, mazingira na uendelevu wa miradi kwa weledi na uadilifu ili dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo iweze kutimia kwa wakati.
“Pia nawataka wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya maji ndani ya mkoa huu kuhakikisha wanaitekeleza kwa ubora na kwa mujibu wa mikataba waliosaini ikamilike kwa wakati kulingana na makubaliano kwani watakaokiuka mikataba na kutekeleza miradi kwa viwango visivyoridhisha watachukuliwa hatua lengo ni kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi hiyo,”amesema.