24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RUWASA Simiyu yawataka wananchi kutunza miundombinu ya miradi ya maji

Na Samwel Mwanga, Simiyu

WAKALA wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Mkoa wa Simiyu imewataka wananchi kutunza na kuilinda miundo mbinu ya miradi ya maji iliyotekelezwa na Ruwasa mkoani humo.

Meneja wa Ruwasa mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mariamu Majala amesema hayo baada ya kutembelea mradi wa maji wa Sengerema katika kijiji cha Mhango wilayani Bariadi ambao umekamilika na kuanza kutoa maji.

Ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji katika kijiji cha Mwandu Itinje wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu ukiwa unaendelea chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (Ruwasa).Picha Na Samwel Mwanga.

Amesema kuwa kwa sasa Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa maji.

Mhandisi Majala amesema kwa kipindi ambacho Rais Samia Suluhu ameingia madarakani hadi sasa wameweza kupokea kiasi cha Sh Bilioni 15 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika wilaya zote za mkoa huu.

“Serikali kwa sasa imekuwa ikitupatia fedha za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji katika mkoa wetu wa Simiyu na miradi hiyo imetekelezwa katika wilaya za Maswa, Bariadi, Itilima, Busega na Meatu.

“Tangu Rais Samia aingie madarakani kwa mwaka mmoja sasa, tumeshapokea kiasi cha Sh bilioni 15 kutekeleza miradi ya maji na kwa sasa ipo iliyokamilika na kutoa huduma za kwa wananchi na mingine iko katika hatua ya ukamilishaji,” amesema Mhandisi Majala.

Amesema Ruwasa katika mkoa huo unatekeleza miradi saba inayotokana na fedha za Ustawi wa Taifa kwa Maendeleo katika kupambana na Maambukizi ya UVIKO-19 kwa lengo la kuongeza hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa huo.

Aidha, Mhandisi Majala amesema kwa sasa wameshasaini mikataba 36 katika miradi 41 ya maji katika mkoa huo na kwa mwaka wa bajeti 2021/2022 walitengewa Sh bilioni 23 kwa ajili ya shughuli za utekelezaji wa miradi ya maji mkoani humo.

Amesema miradi yote hiyo itakapokamilika itaongeza hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya vijijini kwa asilimia 16.2 na kufikia asilimia 83 na hiyo itasaidia kufikia lengo la upatikanaji wa maji vijijini kwa asilimia 85 kwa mwaka 2025 kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Pia, Mhandisi Majala ametumia fursa hiyo kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kuweza kuwapatia fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwa lengo la kumtua mama ndoo kichwani.

Naye Mkuu wa wilaya ya Itilima, Faudhia Salum amesema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kutekeleza miradi ya maji hivyo ni vizuri miradi hii ikikamilika ilindwe na itunzwe maana ujenzi wake ni gharama sana tofauti na baadhi ya wananchi wanavyofikiria wanapoona maji yamewafikia majumbani.

“Ni lazima tuilinde na kuitunza hii miradi ya maji inapokamilika kwa kuwa serikali inatoa fedha nyingi sana ambazo ni kodi ambayo sisi wananchi tunailipa wengine hawajui hayo wanapoona tu maji yamewafikia majumbani,” amesema Faudhia.

Upande wake Mkuu wa wilaya ya Busega, Gabriel Zakaria amesema kuwa katika wilaya hiyo wanatumia nguvu zote za vyombo vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha walinda miundombinu ya maji na atakayebainika kukiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Sisi wilaya ya Busega hatuna utani na kulinda miundombinu ya maji tumetoa elimu kwa wananchi  juu ya ulinzi wa miundo mbinu hii ya maji na sasa tunatumia vyombo vya ulinzi na usalama kuwashughulikia wananchi ambao watabainika kufanya hujuma yoyote katika miradi ya maji,” amesema Zakaria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles