Na Hadija Omary, Lindi
Hatua ya Sarikali kupitia Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kumkabidhi, Mkandarasi Helem Contruction Company Limited, Mradi wa maji kwa katika Ukanda wa Navanga kumetajwa huewenda ikasaidia kunusuru kuvunjika kwa ndoa za wakazi wa Kijiji hicho.
Mradi huo wa ukanda wa Navanga unaotajwa kugharimu Sh Bilioni 4.3 unalenga kunufaisha wakazi 17,015 kutoka vijiji 8 vilivyopo kata ya Kitumbikwela, Navanga, Nachunyu, Sudi na Mnolela umekabidhiwa mbele ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ambae pia ni Mbunge wa jimbo hilo, Nape Nnauye.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Nape licha ya kumshukuru Rais Samia Suluhu kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, amemtaka Mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo kutekeleza kwa muda uliopangwa.
Nape amesema mradi huo ambao umeanza rasmi mara tu baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, unatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita.
“Nimemueleza Mkandarasi, kama kuna kazi ambayo hatakiwi kuchezea ni kazi ya jimbo la Mtama, ukichezea kazi ya jimboni kwa Nape huo ndio mwisho wa kupata kazi popote tena bora tuambiane mapema kabla mambo hayajahalibika na fitina hiyo sishindwi nitaanzia kwa rais mpaka wizarani,” amesema Nape.
Hata hivyo, Nape amewaondoa hofu wananchi ambao hawajafikiwa na mradi huo kwa awamu ya kwanza ambapo amesema baada ya serikali kuu kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo hatua inayofuata ni kwa Halmashauri kumalizia katika maeneo macheche yaliyosalia.
“Vijiji vilivyotajwa sio vyote vitamalizika, kwa maana ya kwamba tulivyovitaja vipo ambavyo havijatajwa kwa hivyo kwenye awamu hii ya kwanza havitapata maji kwa awamu hii, lakini ni kazi yangu mimi kwa kushirikiana na madiwani ambapo kazi ya kwanza ilikuwa ni hii ya Sh bilioni 4.3 ambapo kwa sisi kama halmashauri tusingeweza.
“Lakini kuyasogeza kwenye vijiji na vitongoji vilivyobaki ni kazi ya Halmashauri mimi na madiwani tutatenga fedha tuyavute maji haya ambayo Mama yetu Samia ametuletea sasa tuyaporomoshe kwenye maeneo mengine ambayo hayakutajwa,” amesema Nape.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga ameeleza namna serikali ilivyojipanga kumaliza tatizo la maji safi na salama katika halmashauri hiyo ya Mtama ambapo alieleza kuwa kwa kipindi cha miezi sita halmashauri hiyo imepokie zaidi ya Sh bilioni 10 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa (RUWASA), Mhandisi William Swilla amesema kukamilika kwa mradi huo utasaidia wananchi wa maeneo hayo kuongeza chachu ya kufanya shughuli za kimaendeleo badala ya kutafuta maji kama ilivyo sasa.
Amesema wananchi hao kwa kipindi kirefu wamekabiliwa na changamoto ya maji safi na salama ambapo kwa kutambua hilo serikali kupitia wakala huo ilifanya usanifu wa mradi huo mwaka 2020 na kukamilika mwaka 2021 ambapo sasa Mkandarasi amekabidhiwa rasmi mradi huo kwa ajili ya kuanza utekelezaji.
Nao baadhi ya wananchi hao wameeleza changamoto wanazokabilianazo kwa kukosa huduma ya maji karibu na maeneo yao kuwa ni pamoja na ndoa zao kuwa hatarini kuvunjika kutokana na waume zao kukosa imani na wake zao pindi wanapokwenda kutafuta maji.
“Suala hili la maji katika kata hii ya Navanga bado ni changamoto kubwa kwani tunalazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji napengine tunapotoka kwenda katika maeneo hayo kwa kuwa tunatumia muda mrefu wanaume wetu wanakosa imani kuwa uwenda tunatumia mwanya huo kusaliti ndoa zetu,’’ amesema Mazukuni Ally.