24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RUWASA ongezeni kasi usimamizi miradi ya maji-DC Maswa

Na Samwel Mwanga, Maswa

MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira(RUWASA) wilayani humo kuongeza kasi ya Usimamizi wa Miradi ya Maji inayotekelezwa chini ya Ruwasa ili wananchi wanufaike nayo kwa kupata maji safi na salama.

Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge(wa pili kutoka kushoto)akiangalia moja ya vituo vya kuchotea maji katika kijiji cha Isanga wilayani humo vilivyojengwa na Ruwasa.(Picha Na Samwel Mwanga).

Kaminyoge ametoa kauli hiyo leo Juni 22, 2022 mjini Maswa baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maji inayotekelezwa na Ruwasa kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa miradi hiyo akiwa ameambatana na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Mbaragane-Sulu, Masanwa, Isanga na Inenwa-Kizungu.

Amesema kuwa serikali imetoa fedha nyingi wilayani humo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji hasa ya maeneo ya vijijini ili kumshusha mama ndoo kichwani.

Kaminyoge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo amesema utekelezaji wa miradi yote hiyo ikiwemo ile ya fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19  ni vizuri ikasimamiwa ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora kulingana na thamani ya fedha zilizotolewa.

“Miradi hii yote ya maji ambayo Ruwasa mnaisimamia ikiwemo ile ya fedha za Uviko ni vizuri sasa mkaisimamia kwa kasi kubwa ili  iweze kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora kulingana na fedha zilizotolewa na serikali ya Awamu ya sita,” amesema Kaminyonge.

Amesema kuwa miradi ya maji ya fedha za Uviko-19  kwa nchi mzima imepangwa kukamilika ifikapo Juni 30, mwaka huu hivyo ambayo bado haijakamilika katika wilaya hiyo ni lazima ikamilike ila ile miradi mingine ifikapo mwezi Agosti, Mwaka huu iwe imekamilika.

Aidha, amesema miradi iliyo mingi ya maji katika wilaya hiyo inayotekelezwa na Wakandarasi inashindwa kukamilika kwa wakati kutokana na baadhi ya vifaa yakiwemo mabomba kununuliwa na Ruwasa makao mkuu jambo ambalo linachelewesha utekelezaji wa miradi hiyo.

“Huu utaratibu wa mabomba kununuliwa na Ruwasa makao makuu halafu yatumwe kwa Mkandarasi umekuwa ukichelewesha utekelezaji wa miradi maana kuna maeneo mitaro ya kuweka mabomba ili iweze kupeleka maji kwa wananchi imechimbwa ila bomba ndizo hazipo,hivyo nashauri Wizara ya maji kuangalia upya utaratibu huo,” amesema amesema.

Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha amesema licha ya changamoto chache zilizopo wameweza kukabiliana nazo kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli zilizobaki ili miradi hiyo yote ikamilike kwa muda ambao wamepangiwa.

Amesema kwa sasa watatumia muda mwingi wa kazi zao kuitembelea na kuikagua miradi hiyo ili wananchi waweze kupata maji safi na salama.

“Mkuu wa wilaya nikuhakikishie mimi pamoja na timu yangu ya Ruwasa wilayani Maswa tutatumia muda wetu mwingi kuitembelea na kuikagua miradi hii ambayo inaendelea kujengwa ili wananchi wapate maji safi na salama hivyo hatutakaa ofisini hadi miradi yote hii ya maji ikamilike,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles