NAIROBI, KENYA
NAIBU Rais William Ruto ametakiwa kuilipa fidia Mamlaka ya Anga ya Kenya (KCAA) kwa kupora kiwanja cha wakala huyo wa serikali, ambamo amejenga hoteli yake ya kifahari ya Weston.
Katika siku yake ya mwisho kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Ardhi (NLC), Abigael Mbagaya alisema kwa mujibu wa maamuzi yao, mmiliki wa Hoteli ya Weston anapaswa kulipa fidia kwa watu wa Kenya kwa thamani ya sasa ya ardhi hiyo.
“Fidia hizo zitaiwezesha KCAA kununua ardhi ya ukubwa kama huo katika eneo jirani,” Mbagaya alisema wakati wa mahojiano na kituo cha televisheni cha Citizen mjini hapa juzi. Maneno yake ni kinyume na yale, ambayo Dk. Ruto, aliyasema kuwa mmiliki wa awali aliyemuuzia ardhi hiyo ndiye atakayelipa fidia.
“Mipango ya fidia imepangwa kikatiba kurudisha ardhi kwa Mamlaka ya Anga ya Kenya kwa kuwabana wale waliotuuzia ardhi walipe,” Ruto alikaririwa akisema katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Katika mahojiano hayo, Dk Ruto kwa mara ya kwanza alikiri kuwa ardhi hiyo ilipatikana isivyo halali, akisema Weston ni mnunuzi asiye na hatia kwa vile aliipata kutoka mtu mwingine aliyeimiliki kiharamu.
Hata hivyo, Mbagaya alisema si jukumu la NLC kuanza kuwasaka wamiliki wa awali wa ardhi hiyo yenye utata. “Weston lazima ilipe fidia.
Iwapo Dk. Ruto anataka, anaweza kuwasaka watu waliomuuzia ardhi hiyo. Hicho ndicho tunachofanya,” alisema. “Je, tunaweza kuingia msituni kuwatafuta wamiliki wa awali? Hapana, jukumu letu ni kuwaendea waliopo sasa.
Na hao wanaweza kuwasaka wenyewe wale wa awali,” alisema Mbagaya alisema NLC , ambayo muhula wake wa miaka sita chini ya uenyekiti wa Dk Muhammad Swazuri ulimalizika siku hiyo ya juzi, imeshakabidhi wataalamu kazi ya kutathimini thamani ya Weston kwa kuangalia kiasi gani wanatakiwa kulipa fidia.
“Tumewaamuru wataalamu wafanya tathimini kwa kiwango cha sasa cha soko,” alisema. Alipoulizwa sababu ya Weston kutobomolewa kama ilivyotokea majengo mengine yaliyopatikana isivyo halali mjini Nairobi, Mbagaya alisema kila kesi iliamuriwa kwa vigezo vyake.
Hata hivyo, uamuzi wa NLC dhidi ya Ruto haukufurahisha wengi kwa kile kinachodaiwa kumlinda, lakini Mbagaya ameutetea kuwa umefanyika kwa mujibu wa sheria.