25.4 C
Dar es Salaam
Thursday, January 20, 2022

Ruto ‘asahaulika’ tena hafla ya kiserikali 

NAIROBI, KENYA

KWA siku ya pili mfululizo itifaki katika hafla za kiserikali haikufuatwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuhutubia, huku naibu wake William Ruto akisahaulika.

Tukio hilo lilitokea wakati wa ufunguzi wa Kanisa Katoliki, katika Kaunti ya Kiambu baada ya Kardinali John Njue, ambaye aliongoza ibada hiyo kumwalika Rais Kenyatta kuhutubia.

Njue alisema Rais Kenyatta alikuwa na haraka ya kuondoka kwenda shughuli nyingine, ambapo baada ya hotuba hiyo Rais na viongozi wengine akiwemo Ruto walitoka nje wakati wa ufunguzi rasmi wa kanisa hilo kisha kuondoka.

Dk. Ruto na wengine baadaye walirudi kanisani hapo, ambapo alihutubia waumini hao.

Kwa mujibu wa itifaki ni Naibu Rais anayepaswa kumwalika Rais, ambaye hotuba yake ndiyo huwa kilele cha sherehe zozote zile anazohudhuria.

Lakini katika tukio hilo ilishangaza Rais kualikwa na Kadinali Njue mbele ya Ruto kisha kuhutubia, badala ya kualikwa na naibu wake.

Tukio jingine ni pale Wakenya walipojiuliza maswali mitandaoni wakati Waziri wa Ulinzi, Raychelle Omamo aliposoma hotuba ya Rais Kenyatta kwenye hafla ambayo Ruto alikuwepo wakati wa kusimikwa kwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kisumu ya Kanisa Katoliki, Philip Anyolo.

Kulingana na itifaki, Dk. Ruto anapokuwa kwenye hafla ndiye humwakilisha rais kwa wadhifa wake kama naibu wake.

Kwa sababu hiyo, wengi walitarajia ndiye atakayesoma hotuba ya rais, lakini hilo halikutokea na badala yake Dk. Ruto aliyekaribishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuhutubia alimkaribisha Omamo kusoma hotuba ya Rais.

Kwenye hotuba zao tofauti, wote wawili walitoa wito wa umoja na amani. “Mahali watu wanapopanda chuki, tutapanda upendo. Mahali wanapopanda migawanyiko, tutapanda umoja kwani mwishowe hiyo ndiyo itatuwezesha kuendeleza mbele nchi yetu,” alisema Rais.

Aliongeza: “Naomba kila mmoja wenu kujiunga nasi katika harakati hizi za kuleta amani na kujenga taifa lenye ufanisi na umoja,” alisema.

Kwenye hotuba yake, Dk. Ruto alionekana kuhimiza kutulizwa kwa joto la kisiasa lililosababishwa na mjadala kuhusu azma yake ya kumrithi Rais Kenyatta mwaka 2022.

Mjadala huo ulikolezwa baada ya aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee aliyejiuzulu, David Murathe kudai hapakuwepo makubaliano yoyote kwamba jamii ya Mlima Kenya itamuunga mkono Ruto uchaguzi wa 2022.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
175,434FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles