23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

RUSHWA ITAISHA KWA KUSHUGHULIKIA TATIZO LA MSINGI

Na Christian Bwaya na  Gidion Obeid


MWAKA 2017 Shirika la Transparency International – linalojikita katika masuala ya uwazi wa serikali – lilitoa ripoti inayoonyesha kupungua kwa kiwango cha rushwa hapa nchini.

Pamoja na kufurahia taarifa hiyo, bado tutakubaliana kuwa bado katika shughuli zetu za kila siku tunakumbana na mazingira ya rushwa. Tunapopita barabarani, tunapokwenda hospitalini, maofisini kupata huduma, tunakutana na mazingira ya rushwa.

Ni shauku ya wapenda maendeleo wote, si tu kuona rushwa imepungua, lakini pia kuona tunaimaliza kabisa. Hata hivyo, bado zipo chembe chembe za rushwa katika jamii kuonesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kutokomeza tatizo la rushwa. Swali la kujiuliza ni je, tunashughulikia tatizo la msingi linalosababisha rushwa nchini?

Mwandishi wa kitabu cha ‘The mindset of rich’ ameandika: “Kama haupendezwi na matunda ya mti, badilisha mizizi yake.” Maana yake ni kwamba kama ukitaka kubadilisha matokeo ya jambo fulani lazima ugundue kwanza msingi wake. Kama kuna jambo kwenye maisha yako haulipendi, lakini kila mara linaendelea kujitokeza hata kama haulipendi inawezekana chanzo cha tatizo haujafahamu. Hapo ndipo utajikuta unajaribu kubadilisha matunda ya mti kwa kubadilisha matawi ya mti, bila kuwaza kubadilisha mizizi.

Matatizo mengi ya kijamii, hasa kwenye nchi zinazoendelea kama ya kwetu, ni matatizo ya kimtazamo au kifikra.  Yaani ukiwa na mtazamo sahihi kuhusu jambo fulani utakachokifanya kitaongozwa na mtazamo wako, na hata matokeo utakayoyapata yatakuwa yamesababishwa na mtazamo wako. Tumesikia mara nyingi, kwa mfano; watu wakiwalaumu waliopokea rushwa, lakini ni mara chache watoa rushwa wamelaumiwa. Hivi kusingekuwa na watoa rushwa, wapokea rushwa wangekuwapo?

Rushwa ni ishara ya tatizo pana la kijamii, tatizo la kimtazamo. Kama wananchi wenyewe hawataichukia rushwa kwa vitendo, kazi yote inayofanyika na serikali ni bure. Kama tutaendelea kukubali utamaduni wa wananchi kuichukulia rushwa kama utaratibu wa kawaida wa maisha, tatizo hili haliwezi kuisha. Tutasikia ripoti za kutia matumaini hapa na pale, lakini baada ya muda tutarudi kule kule tulikotoka.

Tunaweza kumaliza rushwa kama tutashughulikia tatizo la msingi. Mahali pa kuanzia ni kubadilisha mitazamo yetu kuhusu vitu vinavyofanya maisha yawe ya thamani. Kwa mfano; badala ya kuwaheshimu watu kwa kuwa na vitu kama nyumba au magari ya kifahari, tujenge utamaduni wa kuwaheshimu watu kwa sababu ya tabia zao njema. Tuwajengee watoto wetu tabia ya kuwaheshimu watu kwa kuwa na tabia njema. Tuanze kuwatunuku watu kwa mchango mkubwa wa maendeleo walioufanya kwenye jamii.

Kama tumekuwa na tuzo za waigizaji bora Tanzania, waimbaji bora, warembo, kwa nini isiwezekane kuwapa tuzo watu walioleta mchango mkubwa katika jamii? Kwanini tusiwatambue watu kwa kazi kubwa walizozifanya katika kubadilisha maisha ya watu wetu? Tukianza kufanya hivi, tukaanza kuwatambua watu kwa mambo mema waliyoyafanya, watoto wetu watajifunza kuthamini watu kwa mchango wao katika jamii.

Badala ya kujenga kizazi cha watu wanaotafuta umaarufu kwa vitu visivyo na maana, tunaweza kujenga kizazi cha watu watakaokuwa wanaishi ili kutoa mchango kwenye maendeleo ya jamii. Hili litawezekana tu kama tutaacha kuheshimu matajiri kwa sababu ya fedha zao.

Vijana wengi wanashuhudia watu wenye mali ndio wanaothaminiwa. Watu wenye kujipatia utajiri wa haraka katika umri mdogo ndio wanaopewa heshima. Matokeo yake, inajengeka dhana vichwani mwao kwamba ili uheshimike kwenye jamii inayokuzunguka, lazima uwe na vitu. Mawazo ya vijana yanajielekeza kwenye kuwaza namna ya kupata fedha kuliko kuleta mchango katika jamii. Mawazo kama haya ndiyo yanayochochea watu kufikiria kutumia njia zisizo na maadili kujipatia fedha. Hivi ndivyo tatizo la rushwa linavyozidi kushamiri.

Tuwafundishe watoto wetu kwamba heshima haiko kwenye fedha nyingi alizo nazo mtu, bali mchango anaoutoa mtu kwenye maendeleo ya taifa. Tukifanya hivyo, watu wataelekeza nguvu zao kuleta mchango chanya kwenye jamii na hawatakuwa na shinikizo la kushiriki vitendo vya rushwa kama njia ya mkato ya kutambuliwa na jamii.

Mwandishi wa makala haya ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ushirika (MOCU).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles