RUGEMALIRA, SETHI WA ESCROW KIZIMBANI LEO

0
726

Na MWANDISHI WETU

Kesi ya uhujumi uchumi na kuisababishia hasara serikali ya Sh bilioni 309.5 inayowakabili Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engeneering na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL, James Rugemalira na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Limited (PAP), Habinder Seth Sigh, inatarajiwa kutajwa leo  tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Rugemalira na Sethi walifikishwa mahakamani Juni 19 mwaka huu na kusomewa mashtaka sita yakiwamo ya uhujumu uchumi.

Wanatuhumiwa kula njama, kughushi, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 (Sh bilioni 309.5.

Wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014  Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 18,  2011 na Machi 19, 2014  Dar es Salaam, wakiwa si watumishi wa umma na wakisaidiana na watumishi wa umma walitekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la nne, mtuhumiwa Seth anadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika mtaa wa Ohio Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 ya usajili wa makampuni na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi Kitalu namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki, Dar es Salaam wakati si kweli.

Seth anadaiwa kutoa nyaraka hiyo ya usajili wa kampuni kwa ofisa Msajili wa Makampuni, Seka Kasera, kwa nia ya kuoneysha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau.

Katika shtaka jingine, washtakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 28/29, 2011 na Januari 23,2014 makao makuu ya benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la St. Joseph, kwa ulaghai, walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Sh 309, 461,300,158.27.

Iliendelea kudaiwa kuwa katika shtaka la kusababisha hasara, washtakiwa hao wanadaiwa, Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati Kinondoni, kwa vitendo vyao, waliisababishia Serikali hasara ya Sh 309,461,300,158.27.

Walirudishwa rumande hadi leo kwa kuwa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza au kutoa dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here