24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rugemalira acharuka mahakamani

Kulwa Mzee – Dar es Salaam

MFANYABIASHARA James Rugemalira amevunja ukimya mahakamani, akidai upelelezi wa kesi inayowakabili hautakamilika hadi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) washughulikie barua aliyowaandikia kuonyesha jinsi Benki ya Standard Chartered Hong Kong ilivyokuwa inakwepa kodi na ushuru wa forodha.

Rugemalira alidai hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili yeye na Mkurugenzi wa IPTL, Habinder Sethi ilipokuwa inatajwa.

Alieleza hayo baada ya Wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo kudai kesi ilipangwa kwa kutajwa na upelelezi haujakamilika.

Rugemalira aliomba kuzungumza mwenyewe bila kuwakilishwa na wakili na aliporuhusiwa, alidai Januari 24, mwaka huu alizungumza na mwakilishi wa Takukuru alipotembelea gerezani na akamkabidhi nakala ya barua  aliyoandika kwenda kwa Kamishna wa TRA, lakini hadi sasa hajapata jibu lolote.

“Mheshimiwa hakimu, naomba kesi ikitajwa upande wa mashtaka walete jibu kwa sababu wanaostahili kushtakiwa katika kesi hii ni benki hiyo na ninashangaa kuona wengine wanaongezwa katika kesi kwa madai upelelezi haujakamilika.

“Upelelezi wa kesi hii hautakamilika, na ili ukamilike Takukuru wafuatilie hiyo barua,” alidai Rugemalira.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 13 kwa kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Mbali na Rugemalira na Sethi, mshtakiwa mwingine ni aliyekuwa Mwanasheria wa Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 27/2017, Makandege anakabiliwa na mashtaka matano, yakiwamo ya kuisababishia Serikali hasara ya dola za Marekani 980,000 na utakatishaji wa fedha.

Alisomewa mashtaka hayo Desemba 20 mwaka jana baada ya kuunganishwa na washtakiwa Sethi na Rugemalira katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Miongoni mwa mashtaka hayo, Makandege anadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Pia anadaiwa kuongoza genge la uhalifu katika nchi hizo, akiwa si mtumishi wa Serikali, akishirikiana na watumishi wa umma kwa kuratibu na kufadhili mpango wa uhalifu.

Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, Makandege anadaiwa kati ya Januari 23, 2014 na Februari 2014, alijipatia dola 380,000 katika Benki ya Stanbic iliyopo Kinondoni na dola 600,000 katika Benki ya UBL Bank (T) Ltd iliyopo Wilaya ya Ilala, fedha zilizotoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa nyakati tofauti.

Kwa upande wa washtakiwa Sethi na Rugemalira,  walifikishwa mahakamani hapo na zaidi ya miaka miwili wamekaa rumande kutokana na upelelezi wa kesi yao kutokamilika.  

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27. Kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017. 

Washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Katika mashtaka ya kujipatia fedha, inadaiwa kwamba  kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.  

Pia washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja wanadaiwa walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni Dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles