25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Rugemalira aamsha upya mzimu wa Escrow

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MKURUGENZI wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira, amemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), akimwomba kumwachia huru ili washirikiane kupata Sh trilioni 37 anazoidai Benki ya Standard Chartered na pia Serikali itapata kodi ya zaidi ya Sh trilioni sita.

Wakati Rugemalira akidai hayo, aliyekuwa mmiliki mwenza katika kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Sethi, ameandika barua kwa DPP akikubali kurejesha fedha kulingana na makubaliano watakayokuwa wamekubaliana.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi kwamba kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa na anaomba tarehe nyingine.

Naye Wakili wa Rugemalira, Michael Ngalo alidai mteja wake aliandika barua kwenda kwa DPP, lakini hawajapata majibu, hivyo aliomba upande wa Jamhuri kusaidia yapatikane.

Baada ya Wakili Ngalo kueleza hayo, Wakili wa Serikali Wankyo alieleza kwamba  ni kweli barua imepokewa na inafanyiwa kazi, majibu atapewa.

Alidai kuhusu upelelezi bado haujakamilika na hawawezi kuahidi ni lini utakamilika.

BARUA YA RUGEMALIRA

Rugemalira aliandika barua Oktoba 4, mwaka huu kwenda kwa DPP na kupokewa Oktoba 5, akiomba aachiwe huru ili aweze kushirikiana na Serikali kupata Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered na washirika wake.

Mshtakiwa huyo ameainisha vielelezo kadhaa vinavyoonyesha Standard Chartered ilivyohusika katika sakata la IPTL.

Miongoni mwa vielelezo hivyo ni gharama zilizokuwa zinatozwa na IPTL dola za Marekani 1.06 kwa kWh ni za chini kuliko zilizokuwa zinatozwa na Songas dola za Marekani 4.31 kwa kWh.

Kielelezo kingine ni barua aliyomwandikia Gavana wa Benki Kuu (BoT) Januari 17 mwaka huu akiomba majina ya watu waliolipwa Sh 144,947,669,844.2 zilizokuwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow kati ya Julai 5, 2006 na Machi 19 mwaka 2014.

Wakati sakata la Escrow lilivyoingia bungeni mwaka 2014 na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa akauti hiyo kwa maelezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilielezwa kuwa fedha za Rugemalira zilikuwa kwenye akaunti ya Benki ya Mkombozi ambazo baadhi aligawa kwa watu waliotajwa.

 Pia inaelezwa fedha nyingine za PAP, ziliwekwa katika akaunti ya kampuni hiyo ya Sethi ambapo taarifa ya PAC bungeni ilisema zilisombwa kwa sandarusi na watu ambao hawakutajwa na sasa Rugemalira anataka majina ya watu hao kuwekwa wazi.

Pia katika barua yake hiyo kwa DPP, Rugemalira pia anadai alieleza PAP kukiri kulipwa na Benki Kuu Sh 164,513,630,314.15 na dola za Marekani 22,198,544.60 na si Sh 309,461,300,158.27 na dola za Marekani 22,198,544,.60 kama ilivyokuwa katika hati ya mashtaka kwenye kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2017.

Aliambatanisha pia nakala ya barua ya BoT yenye kumbukumbu namba NC.130/170/01 iliyoandikwa Februari 18, 2018 (2019) ikiwa ni majibu ya barua yake ya Januari 19, 2019.

Kiambatanisho kingine ni cha gazeti la Financial Times la Julai 20/21 2019 lililotoa taarifa kuwa wadau wameituhumu Benki ya Standard Chartered kwa Serikali ya Marekani kwa kutoa dola bilioni 57 isivyo halali na benki hiyo ilifikia makubaliano na mamlaka za nchi hiyo kwa kukubali kulipa faini ya dola bilioni moja.

“Ninatumaini kwa maelezo hayo yaliyoainishwa katika nyaraka hizi zilizotolewa na ofisi yako kati ya Juni 18, 2019 na Julai 22 2019 utaweza kutumia mamlaka yako chini ya kifungu cha 29(6) cha Sheria ya Makosa ya Uhujumu Uchumi kuniachia huru katika kesi ya uhujumu uchumi namba 27 ya mwaka 2017 ili niendelee na juhudi zangu za kuisaidia Jamhuri kurejesha zaidi ya Sh trilioni 37 kutoka Benki ya Standard Chartered,” alieleza.

Alieleza hana tatizo na Jamhuri kwa kuwekwa mahabusu kwa muda wote aliokaa huko, kwa kuwa anaamini hatua hiyo ilichukuliwa kwa Jamhuri kupotoshwa na Benki ya Standard Chartered.

Alimuomba DPP kutumia mamlaka yake aliyopewa katika Kifungu cha 29(6) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2016 kuagiza aachiwe huru ili achukue hatua katika kesi zake dhidi ya Benki ya Standard Chartered kupitia Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.

“Iwapo nitaondolewa mashtaka yanayonikabili, itaniwezesha kuendelea na kesi nilizozifungua dhidi ya Standard Chartered na washirika wake ambapo nadai Sh trilioni 20, kiasi ambacho kitaiwezesha TRA kukusanya kodi  kutoka kwenye hiyo fedha Sh trilioni 6,” alisema.

Katika barua yake, alieleza kuwa viambatishi vingine ni nakala ya tozo iliyokuwa imeandaliwa na Tanesco ikionyesha tozo zilizotakiwa kutozwa na IPTL, ambazo zilikuwa ndogo kuliko za kampuni nyingine.

Ameainisha pia kuwa tozo nyingine ni ya taarifa ya Dk. Camilo Schutte ya Oktoka 12, 2012 kwenda Benki ya Standard Chartered (SCB), Benki ya Standard Chartered (Hong Kong) Ltd (SCBHK) na Benki ya Standard Chartered Tanzania Ltd (SCBTZ) kuwa iwapo hawataondoa malalamiko yao ya kisheria dhidi ya Tanesco katika kesi ya ICSD namba ARB/10/20, Kampuni ya VIP itaibua madai ya zaidi ya dola milioni 485 kama gharama za usumbufu.

Pia ameambatanisha nakala ya taarifa yake kwa Benki ya Standard Chartered Tanzania Ltd na Jamhuri ya Juni 11, 2013 ikieleza kuwa VIP imechukua hatua ya kukata rufaa kwenye mahakama ya juu ya New York nchini Marekani kwa madai hayo ya dola milioni 485.

Ameambatanisha pia nakala ya Kampuni ya VIP yenye kumbukumbu namba Ref: VIPEM: JB/41/2013 kwenda kwa Gavana wa BoT ya Desemba 5,2013 kutoiruhusu PAP kulipwa fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow kutoka BoT kwa niaba ya IPTL.

Nyingine ni nakala ya barua yenye kumbukumbu namba NC.53/135/085 ya Desemba 12, 2013 kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Beno Ndulu ikimweleza Rugemalira kuwa kwa hati ya mahakama iliyotolewa Septemba 5, 2013 Serikali na IPTL malipo yote yameshatolewa kwenye akaunti ya Escrow na kuhamishiwa IPTL Novemba 28, 2013.

MASHTAKA YANAYOWAKABILI

Vigogo hao walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Juni 19, 2017, wakikabiliwa na mashtaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha.

Rugemarila, ambaye  ni Mkurugenzi wa VIP na mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL na Sethi ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa PAP, wanadaiwa kutenda makosa hayo katika Jiji la Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh bilioni 309.

Washtakiwa wanadaiwa  kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014  Dar es Salaam walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Katika shtaka la kujihusisha na mtandao, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam wakiwa si watumishi wa umma,  walitekeleza mtandao wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

 Sethi anadaiwa  Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Dar es Salaam, akiwa na nia ya ulaghai, alighushi fomu namba 14 a ya usajili wa kampuni  na kuonyesha yeye ni Mtanzania anayeishi kiwanja namba 887 Mtaa wa Mrikau Masaki wakati akijua ni uongo.

Baada ya kusikilizwa maelezo hayo ya pande zote, Hakimu Shahidi aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 24, kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles