27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

RUFIJI BADO TABU KWA IGP SIRRO

 

 

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi kufanya ziara katika wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani, kundi la wauaji limeibuka na kufanya mashambulizi, huku mtu mmoja akijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya kichwa.

Mashambulizi hayo yalitokea jana saa 7:30  mchana katika Kata ya Umwe Ikwiriri, ambako mkazi wa kijiji hicho Nurdin Kisinga  alinusurika kuuawa.

Taarifa kutoka kwa mashuhuda kijijini hapo, ambazo zimethibitishwa na Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa (CCM) na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo zimesema baada ya shambulio hilo, majeruhi huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Mchukwi wilayani humo. Hata hivyo kutokana na hali yake kuwa mbaya, alihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu, Mbunge Mchengerwa, alisema baada ya tukio hilo majeruhi huyo alikimbizwa hospitali, lakini ilipofika jioni hali yake ilizidi kuwa mbaya na kukimbizwa Muhimbili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Njwayo, aliliambia MTANZANIA kuwa kutokana na tukio hilo muda huo alikuwa akifanya mawasiliano ili kujua kinachoendelea.

 “Bado majeruhi wapo hospitali na madaktari wameniambia wanaangalia X- Ray kufahamu tatizo, baadaye atajua anaendeleaje,’’ alisema Nywayo.

Alisema majeruhi huyo alikuwa shambani kwake akivuna ufuta na ndipo tukio hilo lilipotokea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi, Onesmo Lyanga, alithibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kuwa majeruhi amepata rufaa na amekimbizwa Muhimbili.

“Ni kweli hali ya majeruhi si nzuri na  imelazimika kuendelea kupata matibabu zaidi, hivyo ameondolewa hapa Michukwi na kukimbizwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,’’ alieleza RPC Lyanga.

Juzi katika Kitongoji cha Kazamoyo, Kijiji cha Ikwiriri Kaskazini, majira ya saa nane usiku wauaji hao walimvamia Erick Mwarabu (38) ambaye ni fundi rangi na kumuua.

Mwarabu akiwa nyumbani kwake, wauaji hao walifika na kumpiga risasi shingoni, ambayo ilitokea kichwani upande wa kulia kati ya jicho na sikio na akafariki dunia papo hapo.

DC Njwayo, aliiambia MTANZANIA kuwa mwili wa marehemu umekwisha kufanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu zake.

Juzi Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Sirro alifika wilayani humo na kuzungumza na wazee, huku tukio hilo likiwa limetokea usiku wake.

Alisema pamoja na hali hiyo, atahakikisha anakomesha kundi hilo aliloliita la wahuni.

Aliwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ikiwamo kutoa taarifa dhidi ya kundi hilo la wauaji katika maeneo hayo.

Mei 21 mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, alitembelea eneo hilo na kuteta na askari wa operesheni maalumu ya kuwasaka wauaji wilayani Kibiti. 

Alisema mauaji hayo sasa yametosha, akisisitiza Serikali haitakuwa tayari kuona vitendo hivyo vikiendelea kama ilivyo Somalia.
Ziara hiyo ya ghafla ya Waziri Mwigulu ilitokana na mauaji ya mara kwa mara ya raia ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.

Mwigulu aliwataka polisi kukaa kimkamkati kuwakamata wauaji hao.

Alisema ni muhimu polisi waondokane na dhana kwamba wauaji hao wametokomea kusikojulika, bali wawakamate.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles