Na JANETH MUSHI,
-ARUSHA
ZIKIWA zimepita siku 53 tangu kukamatwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), anayeshikiliwa katika mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo jijini hapa baada ya kukosa dhamana, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imepanga kusikiliza rufaa yake ya maombi ya dhamana Desemba 28, mwaka huu.
Rufaa hiyo namba 126 ya mwaka huu, iliyokatwa na mawakili wa Lema wakiongozwa na Sheck Mfinanga, inatarajiwa kusikilizwa na Jaji Salma Maghimbi wa mahakama hiyo saa tatu asubuhi.
Kukatwa kwa rufaa hiyo kunatokana na uamuzi wa mahakama hiyo uliotolewa Desemba 20, mwaka huu na Jaji Dk. Modesta Opiyo, aliyekubali maombi namba 69 ya Lema ya kuomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa ya dhamana yake ambapo alitoa siku 10 kwa mleta maombi (Lema), kuwasilisha notisi hiyo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Wakili Mfinanga, alisema lengo la rufaa hiyo ni kupinga na kudai haki ya dhamana ya Lema aliyonyimwa kutokana na makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Novemba 8, mwaka huu.
Mfinanga alisema wameamua kukata rufaa hiyo kujua ni kwanini Lema amekosa dhamana ambayo awali katika mahakama hiyo alipewa na kuwa hawaridhiki na uamuzi uliotolewa na Hakimu Kamugisha ambako alitupilia mbali pingamizi la dhamana lililokuwa limewekwa na Mawakili wa Serikali waliotaka mshtakiwa asipewe dhamana.
Alidai kuwa Hakimu Kamugisha alisema inampa Lema dhamana kwa masharti mahakama hiyo itakayoweka, ila kabla hajamalizia kutoa uamuzi wake Mawakili wa Serikali wameandaa notisi ya rufaa juu ya uamuzi huo na hoja hiyo ikaridhiwa na mahakama.
Wakili huyo alidai kuwa hayo ni makosa kisheria kwa mahakama kukubali maombi ya Mawakili wa Serikali kabla haijamaliza kutoa uamuzi wake na mahakama hiyo kuamua kumnyima Lema haki yake ya dhamana wakati tayari ilishaamua kumpa dhamana kabla ya kukatwa rufaa.
“Tunapinga mahakama ya chini kutokumwachia huru wakati ilishampa dhamana, hayo ni makosa ya kisheria na tunatarajia kuwa na hoja sita za rufaa hiyo ambapo baada ya Jaji Maghimbi kusikiliza pande zote mbili ataamua kama Lema atapewa dhamana au la,” alisema Mfinanga.