Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Rostam Aziz ameiomba radhi Mahakama kufuatia kauli yake aliyoitoa Juni 26, mwaka huu dhidi ya muhimili huo nchini.
Rostam ameomba radhi leo Julai 4, 2023 nyumbani kwake jijini Dar es Salaam katika mkutano na Waandishi wa Habari ikiwa ni saa chache tu baada ya Chama cha Majaji na Mahakimu nchini(JMAT) kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari kikimtaka Mfanyabiashara huyo kuthibitisha tuhuma alizozitoa dhidi ya mahakama au aombe radhi hadharani kama alivyofanya wakati wa kutoa tuhuma hizo.
“Itakumbukwa Juni 26, kwa sababu ya kutambua na kuheshimu hadhi na wajibu wa kikatiba wa mahakama, ningependa kusema yafuatayo, ningependa kuuhakikishia umma kwamba wakati nikizungumzia uwekezaji, halikuwa kusudio langu kudharau mahakama zetu, kama nilifanya hivyo ilikuwa ni kuteleza kwa ulimi.
“Maana kusudio langu lilikuwa likilenga kuhusu kuhusu uwekezaji nchini na maana yangu ilikuwa ni kwamba, ili tupate uwekezaji nchini hatuna budi kuendana na taratibu zinazoongoza uwekezaji duniani.
“Tanzania ni mwanachama wa Excite ambao ni utaratibu unaongoza nchi zote katika kujaribu kuleta uwekezaji katika nchi zao ambao ambao uliundwa Machi 18, 1965 na Oktoba 1966 ukaanza kutumia katika nchi mbalimbali duniani,” amesema Rostam na kuongeza kuwa:
“Kusudio langu lilikuwa kwamba ili tulete uwekezaji na kuwashawishi wawekezaji waje nchini mwetu hatuna budi kutumia sheria hii ambayon inatumika dunia nzima, na kusudio langu lilikuwa, usipofanya hivyo huwezi kupata wawekezaji kwani wawekezaji wanahitaji mahala pa kwenda kama kutakuwa na mgogoro.
“Na sheria yake iko wazi kabisa kwamba mnapokuwa na mgogoro mnaenda mahala ambapo majaji wake hawatoki katika nchi husika, hilo ndilo lilikuwa kusudio langu, kwa hiyo ningependa kusema kwamba dhumuni langu ilikuwa ni kuwaelimisha wale ambao wanasema kwanini tukiwa na mgogoro tunakwenda nchi nyingine kusuluhishwa, huu ndiyo utaratibu wa dunia nzima siyo Tanzania.
“Uispofanya hivyo maana yake hamna uwekezaji utakuja Tanzania hatua mbayo itaathiri maendeleo, hivyo kama nimekwaza sehemu yoyote ile ninaomba ieleweke hivyo, kwani ndiyo lilikuwa kusudio langu,” amesema Rostam.
Rostam alisema nini?
Juni 26, mwaka huu mbele ya waandishi wa habari Rostam alisema kuwa: “Hakuna mwekezaji atawekeza kwenye nchi ambayo kesi ikipelekwa hapo Kisutu kiongozi yeyote anaweza kupiga simu akaielekeza mahakama nini cha kufanya,” alisema Rostam kwenye mkutano huo.
Kauli hiyo ya Rostam ilikuja baada ya kurejea faida za uwekezaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari, akirejea mkataba wa ushirikiano uliosainiwa na Serikali ya Tanzania na Dubai kuhusu uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini.