27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

ROSE MLAY: VIFO VYA UZAZI VINAMALIZA NGUVU KAZI

Na Jovina Bujulu – MAELEZO

UTEPE mweupe duniani ni alama ya uwakilishi ya kuwakumbuka wakina mama waliofariki kutokana na matatizo ya mimba, uchungu na uzazi. Utepe mweupe unashughulikia matatizo ambayo yanaweza kuepukika.

Hapa nchini, asasi ya kiraia ya Muungano wa Utepe Mweupe ndiyo inashugulikia huduma mbalimbali za afya na kuhamasisha jamii kuwajibika ili kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.

Mratibu wa Kitaifa wa asasi hii, Rose Mlay anasema kuwa lengo la kuanzishwa kwake ni kushawishi kuimarika kwa huduma za afya, kwa mama na mtoto.

Anasema lengo la asasi hii ni kuifanya Tanzania kuwa taifa ambalo haki ya mama na mtoto kuwa salama wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua linazingatiwa.

Inakadiriwa kuwa wanawake 8,000 duniani hufariki kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi. Idadi hii ni kubwa kwa viwango vyovyote vile na ina madhara makubwa kijamii na kiuchumi.

Utafiti wa demokrasia ya afya wa mwaka 2010, ulionyesha kuwa wanawake 24 na watoto wachanga 144 hufariki kila siku. Kutokana na juhudi za serikali, Muungano wa Utepe mweupe na wadau wake, vifo hivyo vilipungua kwa wajawazito 600 na watoto chini ya mwezi mmoja. Vifo 1,000 vilipungua ikilinganishwa na mwaka 2013 ambapo wajawazito waliopoteza maisha walikuwa 8,500 na watoto 48,000 kwa mwaka.

“Vifo hivyo vina madhara makubwa kwa kijamii na kiuchumi kwani wanaokufa ni nguvu kazi ya taifa,” anasema Mlay.

Sababu za vifo hivyo ni pamoja na uduni wa huduma za afya, utaratibu wa kujifungulia nyumbani, gharama zinazoambatana na huduma hizo, kifafa cha mimba na mapigo ya moyo kuwa juu.

Katika maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe yaliyofanyika mwaka jana, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan aliwasihi wanawake kujiunga na mfuko wa jamii wa huduma ya bima ya afya ili kuondokana na ukosefu wa fedha wakati wa kujifungua, maana huduma hii inatolewa kwa utaratibu maalum bila kulipa fedha taslimu.

Samia aliwataka wananchi kuachana na mila potofu hasa ukeketaji ambao unasababisha tatizo la kutoka damu nyingi hatimaye kusababisha vifo wakati wa kujifungua.

Vikwazo vingine vya kufikiwa uzazi salama nchini ni pamoja na vituo vingi vya afya kukosa huduma za awali na za dharura, kama upasuaji na damu salama, umeme wa uhakika, hasa vijijini na upungufu wa watumishi wa afya wenye ujuzi na stadi, upungufu wa vifaa, tiba na dawa muhimu.

Changamoto nyingine ni pamoja na kuwanyima watoto wa kike elimu, kuwaozesha watoto katika umri mdogo, kuwanyima wanawake fursa ya kumiliki uchumi, hivyo kuwafanya kushindwa kufikia huduma bora za afya hususani wakati wa kujifungua na kuishia kuhudumiwa na wakunga wa jadi ambao hawawezi kuhimili matatizo makubwa ya uzazi pindi yanapojitokeza.

Naye Ofisa Mawasiliano wa asasi hiyo, Anna Sawaki anasema kuwa wanafanya kazi kwa karibu na kundi la wabunge 22 wakiongozwa na Mbunge wa Peramiho, Janista Mhagama kushawishi watunga sera waongeze bajeti ya Wizara ya Afya ili kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto na kutoa elimu ya uzazi ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Mikakati inayofanywa na Muungano wa Utepe Mweupe ni pamoja na kushirikiana na mashirika mbalimbali kuhakikisha kampeni hii inawafikia walengwa. Mfano ni asasi ya AFRICARE ambayo itajenga chumba cha upasuaji mkoani Rukwa na asasi ya Benjamini Mkapa ambayo imeendelea kutoa mafunzo ya huduma za afya na asasi nyingine ambazo zinasaidia kuimarisha miundombinu kama umeme na maji.

Baadhi ya wananchi wameipongeza asasi hii na kushauri elimu ya uzazi itolewe kwa msukumo zaidi hasa kwa wanawake wa vijijini. Pia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeshauriwa kufuatilia kwa karibu hospitali za binafsi ambazo nyingine huajiri watumishi wasio na utaalamu wa kutosha, jambo ambalo ni kikwazo kwa wajawazito kipindi cha kujifungua.

Kila ifikapo Machi 15 Muungano wa Utepe Mweupe hufanya maadhimisho ambapo hufanya shughuli mbalimbali, kama vile kutoa ushauri wa afya ya uzazi, na upimaji wa magonjwa mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles