RONALDO: MASWALI YENU NIMEYAJIBU UWANJANI

0
774

MADRID, HISPANIA


MSHAMBULIAJI wa klabu ya Real Madrid na timu ya Taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo, amewaambia mashabiki ambao walikuwa wanamzomea kwamba amewajibu juzi mjini Cardiff, baada ya kuifungia timu hiyo mabao mawili na kutwaa ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya.

Miezi ya hivi karibuni mchezaji huyo alijikuta katika wakati mgumu baada ya baadhi ya mashabiki kumshambulia, wakidai kuwa kiwango chake kimeshuka na hana msaada ndani ya kikosi hicho.

Katika mchezo wa juzi wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus, aliweza kutoa mchango mkubwa, huku akifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 4-1 na kufanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara mbili mfululizo.

Baada ya kufunga mabao hayo, ambayo yamemfanya achukue tuzo ya mfungaji bora wa michuano kwa jumla ya mabao 12, huku mpinzani wake, Lionel Messi wa Barcelona akiwa na mabao 11.

“Ninaamini nitakuwa nimewajibu wale wote ambao walikuwa wananikosoa mara kwa mara, sidhani kama watakuwa na maneno tena kwa kuwa nimewajibu uwanjani kwenye mchezo muhimu.

“Huu ni msimu mwingine wa kushangaza, kumaliza msimu huku tukichukua ubingwa wa Klabu bingwa Ulaya pamoja na kuvunja rekodi kwangu ni zaidi ya furaha.

“Ninaamini sisi ni timu ya kwanza kuweza kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo katika michuano hii mikubwa na nimeweza kufunga mabao mawili, hii ni rekodi nyingine kwangu, tumestahili kuwa mabingwa na nimestahili kuwa mfungaji bora wa michuano hii.

“Nilikuwa na maandalizi mazuri katika kuhakikisha ninaisaidia timu, lakini kuna wakati ninashangaa kuona watu wakiwa wanaongea juu ya uwezo wao na mimi siwezi kuwajibu kwa mdomo, ila ninawajibu kwa vitendo uwanjani kama nilivyofanya,” alisema Ronaldo.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo amemmwagia sifa kocha wake, Zinedine Zidane, kwa maneno yake ya mwisho wakati wa mapumziko, huku timu hizo zikiwa 1-1, lakini anadai kocha huyo aliwapa maneno ya kuwajenga katika kipindi cha pili.

“Baada ya mapumziko Zidane aliongea na sisi na kutupatia uhakika wa ushindi, alisema timu yetu ni bora zaidi ya wapinzani, alituaminisha hivyo na tukaamini. Napenda kuwashukuru mashabiki wote kwa sapoti yao tangu mwanzo, lengo letu kwa sasa ni kuhakikisha tunachukua tena taji hilo msimu ujao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here