Ronaldo hatarini kukosa robo fainali Uefa

0
844

TURIN, ITALIA                                                                                                     

MSHAMBULIAJI wa Juventus, Cristiano Ronaldo, yupo hatarini kuukosa mchezo wa robo fainali wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Ajax, baada ya kushtakiwa kutokana na utovu wa nidhamu wakati wa ushangiliaji bao.

Mchezaji huyo anadaiwa kuonesha utovu wa nidhamu wakati akishangilia bao lake la tatu katika mchezo dhidi ya Atletico Madrid, ambapo alifunga mabao yote matatu na kuipeleka timu hiyo robo fainali.

Kutokana na hali hiyo, Atletico Madrid walipeleka malalamiko yao katika Chama cha Soka barani Ulaya, UEFA, hivyo mchezaji huyo anaweza kukumbwa na rungu ya kufungiwa baadhi ya michezo ya Ligi hiyo ya Mabingwa Ulaya.

Kamati ya Maadili na Nidhamu ya UEFA inatarajia kukaa chini kesho kwa ajili ya kujadili juu ya kitendo hicho cha Ronaldo ambacho kinadaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu.

Kitendo hicho kilichofanywa na Ronaldo kinafananishwa na kile ambacho kilifanywa na kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone, katika mchezo wa kwanza dhidi ya Juventus, ambapo Atletico Madrid walishinda mabao 2-0, lakini kocha huyo hakukumbwa na adhabu yoyote.

Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri, anaamini Ronaldo hawezi kukumbwa na adhabu yoyote kwa kuwa alichokifanya ni kitu cha kawaida na kila mchezaji ana aina yake ya ushangiliaji.

“Sioni kama kuna tatizo lolote lililofanywa na Ronaldo, kila mchezaji ana aina yake ya ushangiliaji, hivyo sioni kama anaweza kukumbwa na kifungo cha aina yoyote kama watu wanavyodhani, alikuwa kwenye furaha kutokana na aina ya mchezo, hivyo alishindwa kuzuia hisia zake kutokana na matokeo tuliyoyapata,” alisema kocha huyo.

Ajax, ambao wanatarajia kukutana na Juventus, walionesha kiwango cha hali ya juu katika hatua ya 16 na kufanikiwa kuwaondoa mabingwa watetezi, Real Madrid, ambao walichukua taji hilo mara tatu mfululizo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here